UN: Sintofahamu ya hali ya usalama yaendelea kughubika Mlango Bahari wa Hormuz
UN: Sintofahamu ya hali ya usalama yaendelea kughubika Mlango Bahari wa Hormuz
Katikati ya madai na kuyakanusha kuhusu mashambulizi na makabiliano katika Mlango muhimu wa Bahari wa Hormuz kati ya Iran na Marekani, maafisa wa masuala ya bahari wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kuzitaka meli kuchukua “tahadhari ya hali ya juu.”
Shirika la kimataifa la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Bahari IMO limesema “Tunafahamu kuhusu taarifa hizo lakini hatuna maelezo zaidi. Tunaendelea kuzihimiza meli zote kuchukua tahadhari ya hali ya juu katika eneo hilo.” IMO imeyasema hayo huku ikiendelea kuthibitisha taarifa za mashambulizi ya hivi karibuni na maonyo ya kiusalama yaliyotolewa kwa meli za biashara.
Kwa mujibu wa kituo cha kimataifa cha usalama wa baharini cha UKMTO, meli moja ya kubeba mafuta iliripotiwa kupigwa na makombora yasiyojulikana yalikotoka kaskazini mwa Fujairah huko Enarati leo tarehe 4 Mei, huku meli nyingine ya mizigo ikishambuliwa na boti ndogo kadhaa karibu na Iran siku moja kabla.
Meli nyingine katika eneo hilo zimeelekezwa kupitia redio kuondoka katika maeneo yao ya kutia nanga, hali inayoonesha mazingira tete ya kiusalama.
Tangu mwishoni mwa Februari, IMO inasema takriban matukio 41 yaliyohusisha meli zinazofanya kazi ndani na karibu na Ghuba ya Uarabuni, Mlango Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Oman yameripotiwa kwa UKMTO.
Iran leo Jumatatu imedai kuwa ilishambulia meli ya kijeshi ya Marekani na kuizuia kuingia katika mlango huo wa bahari, lakini Marekani ilikanusha kuwa hakuna shambulio lililotokea.
Jana Jumapili, Donald Trump aliandika kuwa Marekani itasaidia meli ambazo zimekwama katika mlango huo wa bahari kwa miezi kadhaa kuondoka salama.
Umoja wa Mataifa waandaa hatua za dharura
IMO inashirikiana na sekta ya usafirishaji wa majini kuandaa mipango ya dharura, ikiwemo mfumo maalum wa kuwaokoa salama wafanyakazi na meli zitakazonaswa katika eneo la mzozo.
Takribani meli 800 zinazoshiriki biashara ya kimataifa zikiwemo meli za mafuta, mizigo mikubwa na makontena zinaweza kuhusika katika operesheni hiyo ya uokoaji, huku zikiwa zinasafirisha nishati na bidhaa muhimu.
Kwa wastani wa wafanyakazi 25 kwa kila meli, hali hiyo inamaanisha kuwa karibu mabaharia 20,000 wako katika hatari ya moja kwa moja.
Ulinzi wa kijeshi pekee hautoshi
“Watu wote, mabaharia waliomo ndani ya meli katika eneo la Ghuba ya Uajemi wako hatarini iwapo mzozo utaongezeka tena,” imeonya IMO, ikieleza hatari za makombora, vipande vya mabomu vinavyoanguka na uwezekano wa upungufu wa chakula na maji ndani ya meli.
Ingawa baadhi ya mabadiliko ya wafanyakazi na urejeshwaji wa mabaharia nyumbani umefanyika huku mabaharia wapatao 450 wakisaidiwa, makumi ya maelfu bado wako baharini, wakati idadi ya jumla ya meli katika eneo hilo inakaribia 3,000.
Shirika hilo la usafiri wa baharini pia limesema kuwa kusindikizwa kwa meli na vikosi vya kijeshi pekee si suluhisho la kudumu, likitaka kupunguzwa kwa mvutano na kufikiwa kwa makubaliano ya muda mrefu yatakayohakikisha usalama wa safari za baharini.
“Ulinzi wa kijeshi kwa meli si suluhisho endelevu. Kupunguza mvutano kwa dhati na makubaliano ya muda mrefu yanayohakikisha usalama wa mabaharia ndiyo njia pekee ya kusonga mbele,” lilisema shirika hilo.
Mfumo wa afya wa Lebanon wazidi kulemewa
Wakati huo huo nchini Lebanon, mazingira dhaifu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanaendelea kuulemea mfumo wa afya ambao tayari ulikuwa dhaifu, huku mapigano ya hapa na pale na changamoto za upatikanaji wa huduma vikitatiza utoaji wa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa, mashirika ya afya na washirika wake, hali bado ni “ya hatari kubwa, hasa katika maeneo ya kusini na sehemu ambako watu waliokimbia makazi yao wanajaribu kurejea.”
Huduma za afya zimeathirika vibaya. Hospitali tatu na vituo 41 vya afya ya msingi bado havifanyi kazi, huku vingine vikitoa huduma chache tu za dharura na matibabu ya magonjwa sugu.
Vikwazo hivyo vinaongeza mzigo mkubwa kwa vituo vilivyosalia, kupunguza ubora na mwendelezo wa huduma na kuwaacha wananchi wengi bila huduma muhimu za afya.
Upungufu wa dawa watia wagonjwa hatarini
Upungufu wa dawa muhimu, ikiwemo za magonjwa yasiyo ya kuambukiza pamoja na vifaa tiba, tayari unawaweka wagonjwa walio hatarini katika mazingira magumu zaidi.
Maafisa wa afya wanaonya kuwa iwapo mapengo hayo hayatashughulikiwa, basi kutakuwa na ongezeko la madhara ya kiafya, vifo vinavyoweza kuzuilika na kuzorota zaidi kwa hali ya afya.
Licha ya changamoto hizo, washirika wa kibinadamu wanaendelea kuongeza msaada, ikiwemo uchunguzi wa kifua kikuu kwa watu waliokimbia makazi yao.
Zaidi ya watu 750 wamefanyiwa uchunguzi katika wiki za hivi karibuni, ingawa mashirika ya misaada yanaonya kuwa mwitikio wa jumla bado unakabiliwa na changamoto za ufadhili na upatikanaji wa maeneo yaliyoathirika.