Kenya tunashirikiana na mataifa jirani kutokomeza ukeketaji: Hanna Wendot Cheptumo
Kenya tunashirikiana na mataifa jirani kutokomeza ukeketaji: Hanna Wendot Cheptumo
Ukeketaji bado ni changamoto katika maeneo kadhaa duniani na takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO hadi mwaka jana kulikuwa na zaidi ya wasichana na wanawake zaidi ya milioni 230 walio hai waliokeketwa katika nchi 30 za Afika, Mashariki ya Kati na Asia. Kenya ni miogoni mwa nchi zinazopambana na changamoto hii.
Kupitia mahojiano yaliyofanyika kandoni mwa Mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani, CSW70 jijini New York, Marekani, mwezi Machi 2026, Hanna Wendot Cheptumo Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Maslahi ya Watoto wa Jamhuri ya Kenya anaeleza hatua zinazochukuliwa na nchi yake kupambana na hali hiyo ya ukeketaji.
Waziri Hanna anaeleza kwamba katika mazingira ya Afrika Mashariki, vitendo vya ukeketaji vinafanyiak katika nchi mbalimbali Jirani akitoa mfano wa Kenya na Tanzania anasema, “tukiwa wakali kidogo Kenya, wanaenda kufanya pale Tanzania na pale Tanzania (wakiwa wakali), wanavuka kuja upande huu (Kenya).” Kwa hiyo hapo ndipo ushirikiano wa kimataifa unapoingia ili kusaidia kupambana kwa pamoja na tatizo hili linaloondoa haki za mwanamke.
Tunazuia kwanza
Aidha anasema sheria kali zipo za kupambana na ukeketaji lakini kwanza wanajikita katika kuhakikisha matendo ya ukeketaji hayatokei badala ya kulenga kwenye adhabu baada ya tendo kufanyika, “tulirudi tukaona heri tuzuie kabla ukeketaji haujatendeka. Kwa hiyo tunatumia wazee wa mtaa, tunaongea nao mpaka wanaelewa na kukubali kuwa hiki kitendo ni kitu ambacho kimepitwa na wakati.” Pia wanawaeleza kuwa sheria ipo na atakayeikikuka atafungwa na pia inaweza kumpotezea kazi yake chifu au kiongozi wa hilo eneo ikiwa matendo ya ukeketaji yatafanyika katika eneo lake.
“Kwa hivyo sisi kama Kenya tumepiga hatua ya mbele sana.” Anasema , Hanna Wendot Cheptumo na kuongeza kuwa wanapiga kampeni dhidi ya ukeketaji kila wakati ili kuhakikisha hayo matendo ya ukeketaji yanakwisha.
Anahitimisha akisifu namna ambavyo ushirikiano wa kimataifa n anchi majirani wa Kenya ulivyosaidia sana katika mapambano ya mila potofu zinazovuka mipaka ya nchi kama ukeketaji.