Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la njaa na mateso vinazidi kutuangamiza, raia wa Somalia wamweleza Fletcher

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu Tom Fletcher anatembelea kliniki ya afya huko Somalia, ambapo anazungumza na mama anayemshika mtoto wake aliye na utapiamlo wakati wa uchunguzi wa matibabu.
© UNOCHA Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa uratibu wa msaada wa kibinadamu, Tom Fletcher, (wa pili kutoka kushoto) akitembelea kliniki ya afya nchini Somalia.

Janga la njaa na mateso vinazidi kutuangamiza, raia wa Somalia wamweleza Fletcher

Amani na Usalama

Wanawake na watoto waliokimbia ukame na migogoro nchini Somalia wameonya kuwa wanazidi kutumbukia katika janga la kibinadamu la njaa na mateso huku kupungua kwa ufadhili wa misaada ya kibinadamu kukiendelea kuathiri maisha ya watu kote nchini humo. Onyo lao limetolewa wakati mkuu wa masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, akihitimisha ziara yake katika kambi za wakimbizi na vituo vya afya mjini Mogadishu na Baidoa mwishoni mwa wiki.  Flora Nducha na taarifa zaidi

Katika Kituo cha afya na lishe cha Feynus mjini Mogadishu, akina mama wanasubiri huduma za afya wakiwa wamewabeba watoto wao wagonjwa mikononi. Wahudumu wa afya wanaendelea kuwachunguza watoto walioathiriwa na utapiamlo huku sauti za watoto wakilia zikisikika kila kona.

Mmoja wa kina mama hao ni Halima Abdullahi Jeylaani. Anasema alilazimika kukimbia baada ya ukame na njaa kuharibu maisha ya familia yake.

“Nilikimbia kwa sababu hakukuwa na maji wala chakula. Nilimpoteza mume wangu na watoto wangu hawakuwa na kitu cha kula.”

Tom Fletcher anaketi pamoja na kikundi cha wanawake na watoto waliohamishwa katika Kituo cha Lishe cha Youthlinksomal nje ya Mogadishu, Somalia, wakijadili athari za kupunguza fedha kwa maisha yao wakati wa vurugu na mashambulizi ya drone.
© UNOCHA Tom Fletcher wa UNOCHA anatembelea wanawake waliofurushwa na migogoro katika kituo cha lishe cha vijana nje ya Mogadishu, Somalia.

Kote nchini Somalia, mvua zilizoshindwa kunyesha kwa wakati, migogoro na watu kuyahama makazi yao vimewalazimu maelfu ya familia kuishi katika kambi za wakimbizi wa ndani zilizosongamana ambako chakula ni haba na huduma za afya zimeelemewa.

Mjini Baidoa, mama mwingine aliyekimbia makazi yake, Maryama Abdi Hussein, anasema aliwasili kambini hapo miezi mitano iliyopita baada ya ukame kuharibu mazao yao mashambani.

Mashirika ya misaada yanaonya kuwa hali inaendelea kuwa mbaya zaidi huku ufadhili wa misaada ya kibinadamu duniani ukizidi kupungua.

Mkuu wa Misaada wa Umoja wa Mataifa Tom Fletcher akihitimisha ziara yake nchini humo amesema watu wanaokabiliwa na janga hilo la kibinadamu wanafahamu wazi kuwa msaada unapungua.

“Watu wanaohitaji msaada wanafahamu kuhusu kupunguzwa kwa ufadhili. Wananiambia wanajua tumepunguza msaada. Wanajua wanaachwa nyuma kutokana na hatua hizo.Hii ni hali ya kusikitisha sana inadhihirisha nini kinatokea wakati dunia inataza upande mwingine”

Madaktari walioko mstari wa mbele wanasema idadi yawagonjwa wa utapiamlo inaongezeka, hasa miongoni mwa watoto.

Mtoto akipimwa uzito wake katika kliniki ya afya huko Garowe, Somalia.
© UNOCHA/Yao Chen Mtoto akipimwa uzito wake katika kliniki ya afya huko Garowe, Somalia.

Katika Hospitali ya Mkoa wa Bay mjini Baidoa, Dkt. Asma Aweys kutoka Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka Médecins Sans Frontières (MSF) anasema dunia inapaswa kuongeza msaada wa kifedha haraka iwezekanavyo.

“Ujumbe wangu kwa dunia ni kuhakikisha kuna msaada endelevu wa kifedha, hatua za pamoja na juhudi madhubuti ili kukabiliana na changamoto zote ambazo watu wanakabiliana nazo kila siku.”
Umoja wa Mataifa unaonya kuwa bila ufadhili wa haraka, familia nyingi zilizo hatarini nchini Somalia zinaweza kukumbwa na hali mbaya zaidi katika miezi ijayo.