Kukata tamaa na kusaka matumaini katikati ya vifusi Gaza
Kukata tamaa na kusaka matumaini katikati ya vifusi Gaza
Kuelekea siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari duniani Mei 3 mwaka huu tunarejelea chapisho la mwezi Agosti mwaka jana la simulizi ya mwandishi wa habari wa Umoja wa Mataifa aliyeko, Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, kumulika harakati zake za kila siku za kuishi eneo hilo na kulinda familia yake, sambamba na kuripoti hofu na zahma zinazoletwa na mzozo ulioanza tarehe 7 mwezi Oktoba mwaka 2023.
Kitendo cha mwanahabari huyo kutekeleza jukumu lake katika mazingira hayo kimekuwa jukumu lisilokoma katika eneo lililozongwa na vita.
Chapisho hili ni la Agosti 2025
Takriban miezi 21 imepita tangu mashambulizi yaliyoanzishwa na wanamgambo wa kipalestina wa dhidi ya Israeli tarehe 7 Oktoba, 2023 na kisha Israeli kujibu mashambulizi, hali iliyosababisha mzozo mkali unaoendelea hadi sasa.
Maelfu ya watu wamefariki dunia na sehemu kubwa ya Gaza imeharibiwa kwa kiasi kikubwa, lakini maisha lazima yaendelee, kulingana na mwandishi huyo, ambaye jina lake linahifadhiliwa kwa sababu za kiusalama.
Wanaoishi hapa Gaza hawahitaji maelezo marefu kuelewa maana ya vita hivi. Inatosha kusikiliza kwa dakika chache: Ndege zinanguruma bila kukoma angani, na mashambulizi kutoka angani hunyamazisha kila kitu isipokuwa hofu ambayo, ingawa haionekani, hujaza kila nafasi kati ya mahema yetu na kuingia ndani ya miili yetu.
Hatuna uhakika wa kuiona kesho
Usiku, kuna giza totoro isipokuwa miale ya milipuko ya mabomu.
Tunalala tukijua kwamba kuamka si jambo la uhakika.
Kila asubuhi huko Gaza ni jaribio jipya la kuishi, na kila jioni ni changamoto ya kusalia hai. Huu ndio ukweli mgumu tunaouishi.
Mimi ni mmoja wa zaidi ya Wapalestina milioni mbili wanaoishi katika mzigo wa kuhamahama. Ninaandika habari kuhuzu vita na kukata tamaa huku nikipitia uchungu wake wote.
Tangu nyumba yetu iharibiwe Novemba 2023, hema limekuwa hifadhi yetu. Familia yangu, ambayo hapo awali ilikuwa sehemu ya dunia yangu ya faragha, sasa imekuwa sehemu ya hadithi ninazoshiriki na dunia.
Mtindo wa maisha umebadilika
Hapa, maisha ni rahisi na ya kusikitisha.
Kulala juu ya ardhi ngumu, kupika kwa kuni na jitihada za kuchosha za kutafuta kipande cha mkate si chaguo tena, bali ni mtindo wa maisha uliolazimishwa na ukatili wa vita.
Ninapoangalia uso wa mwanangu mkubwa, ambaye bado hajafikisha umri wa miaka 14, naona taswira ya vita vilivyoiba utoto wake na kumwekea mizigo mikubwa kuliko umri wake.
Amekuwa mtaalamu wa njia za kusambaza maji, kubishania bei ya mkate na kubeba galoni nzito za maji. Najivunia sana ujasiri wake, lakini pia nahisi maumivu ya kutokuwa na uwezo kwa sababu siwezi kumlinda dhidi ya yanayotokea karibu nasi.
Chemchemi ya matumaini
Mke wangu anajaribu kuunda chemchemi ya matumaini kwa watoto wetu wengine. Binti zangu wawili wakubwa wanaendelea kujifunza mtandaoni wakati intaneti inapopatikana kwa vipindi, na kusoma vitabu vyovyote vinavyopatikana.
Binti yangu mdogo huchora kwenye vipande vilivyochakaa vya karatasi ngumu, huku mwanangu mdogo zaidi, mwenye umri wa miaka minne, hana kumbukumbu ya chochote isipokuwa sauti ya milipuko.
Tunasimama bila msaada mbele ya maswali yake yasiyo na hatia. Hakuna shule, hakuna elimu, bali ni juhudi za dhati za kudumisha mwanga wa utoto ndani yao, mbele ya uhalisia mkali.
Zaidi ya watoto 625,000 hapa Gaza wamenyimwa elimu.
Hii ni kutokana na uharibifu wa shule na ukosefu wa mazingira salama ya kujifunzia. Mustakabali wa kizazi kizima uko hatarini.
Kuwa shuhuda
Ninafanya kazi pamoja na waandishi wengine wa habari. Tunazunguka kati ya hospitali, mitaa na makazi ya muda.
Tunabeba vifaa vyetu vya uandishi wa habari si tu kurekodi matukio, bali pia kuwa sauti ya wale ambao sauti zao zimenyamazishwa.
Tunamrekodi mtoto anayeteseka kutokana na utapiamlo mkali, tunasikiliza simulizi ya mwanaume aliyepoteza kila kitu na kushuhudia machozi ya mwanamke asiyeweza kuwapatia watoto wake chakula.
Tunaandika tukio linalojirudia kila siku: Maelfu ya watu hukimbilia lori lililobeba unga. Wanafukuza malori, wakikusanya kutoka ardhini chembe za mwisho za unga.
Hawajali hatari kwa sababu tumaini la kupata kipande cha mkate ni la thamani zaidi kuliko maisha.
Kila mara, watu hujeruhiwa au kupoteza maisha katika njia za misafara hiyo na katika maeneo yenye ulinzi mkali ya usambazaji.
Tunatembea mitaani, tukisikiliza kwa makini kila sauti, kana kwamba tunasubiri mwisho kwa kila hatua tunayochukua.
Hakuna tena muda wa mshangao au huzuni, bali mvutano na wasiwasi wa kudumu ambao umekuwa sehemu ya maisha ya manusura hapa.
Huu ndio uhalisia ambao kamera hazirekodi, lakini ndio ukweli wa kila siku tunaouelezea kwa dunia.
Machozi ya wafanyakazi wa UN
Tunaandika juhudi za Umoja wa Mataifa na mashirika yake mbalimbali.
Ninawaona wafanyakazi wakilala ndani ya magari yao ili wawe karibu na vivuko, na ninawaona wenzetu wa UN wakilia wanaposikiliza simulizi za wakazi wenzangu wa Gaza.
Msaada hautoshi. Vivuko hufunguliwa na kufungwa ghafla, na baadhi ya maeneo hukosa mahitaji kwa siku kadhaa.
Maeneo ya magharibi mwa jiji la Gaza yamejaa kupita kiasi. Mahema yametapakaa kila kona, kwenye barabara za pembeni na kati ya vifusi vya nyumba zilizoharibiwa, katika hali mbaya sana.
Masoko matupu: Matunda na nyama vimebakia simulizi
Thamani ya sarafu ya ndani imetoweka. Wale walio na fedha katika akaunti zao za benki hulipa gharama ya hadi asilimia 50 ili kuzitoa, kisha hukumbana na masoko karibu matupu. Kile kinachopatikana huuzwa kwa bei ya juu kupita kiasi.
Mboga ni chache, na zinapopatikana, kilo moja inaweza kugharimu zaidi ya dola 30. Matunda na nyama ni kumbukumbu ya mbali.
Mfumo wa afya uko katika hali ya kuporomoka kabisa kwani asilimia 85 ya hospitali za Gaza hazifanyi kazi tena na huduma nyingi za kusafisha damu na tiba ya saratani zimesitishwa.
Dawa za magonjwa sugu hazipatikani. Siwezi kupata dawa kwa wazazi wangu wanaougua kisukari na shinikizo la damu, na hakuna matumaini ya upasuaji ambao ungeweza kuokoa mkono wa ndugu yangu ulioumia katika shambulio la anga.
Shahidi wa pande mbili
Wakati mwingine, najihisi nimenasa kati ya utambulisho aina mbili: mwandishi wa habari anayerekodi mateso na mwanadamu anayeyapitia.
Lakini huenda hapa ndipo nguvu ya dhamira yetu ya uandishi wa habari kutoka Ukanda wa Gaza ilipo: kuwa sauti kutoka kiini cha janga, na kuifikishia dunia uhalisia wa kinachotokea kila siku.
Kila siku huko Gaza huleta swali jipya:
Je, tutaendelea kuishi?
Je, watoto wetu wataondokana na kusaka maji?
Je, vita vitaisha?
Je, vivuko vitafunguliwa ili msaada uweze kuwasili?
Kutoka hapa, tutaendelea, kwa sababu hadithi zisizosimuliwa hufa, na kwa sababu kila mtoto, mwanamke na mwanaume huko Gaza anastahili kusikika.
Mimi ni mwandishi wa habari.
Mimi ni baba.
Mimi ni mkimbizi wa ndani.
Na mimi ni shahidi wa kila kitu.