IPU: Uwakilishi wa wanawake bungeni bado ni mdogo, na "deepfakes" ni changamoto kubwa
IPU: Uwakilishi wa wanawake bungeni bado ni mdogo, na "deepfakes" ni changamoto kubwa
- Ukuaji mdogo wa uwakilishi wa wanawake
- Hatari ya ‘deepfakes’ kwa wanawake
- Tofauti za kibaiolojia zisitumike kumkwamisha mtoto wa kike
- Wito wa mabadiliko ya kisheria na kikatiba
Rais wa Muungano wa Mabunge duniani, Inter-Parliamentary Union (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa licha ya jitihada za kimataifa za kusukuma usawa wa kijinsia, kasi ya ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika mabunge duniani bado ni ndogo na isiyoridhisha.
Dkt. Ackson amesema hayo hivi karibuni kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani alipohojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa baada ya kuongoza moja ya vikao vya kando vya Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70.
Amesema, “kauli mbiu ilikuwa kuhakikisha haki zinawafikia wanawake na wanaume kwa usawa, lakini hali halisi inaonesha bado kuna pengo kubwa.”
Ukuaji mdogo wa uwakilishi wa wanawake
Dkt. Ackson, amemulika chaguzi nyingi zilizofanyika duniani mwaka 2025 ambazo amesema hazikuleta mabadiliko makubwa katika uwakilishi wa wanawake bungeni. “Tumepanda kwa asilimia 0.3 tu— yaani kutoka asilimia 27.2 hadi 27.5. Hii inaonesha safari bado ni ndefu.”
Ameongeza kuwa wakati kuna maendeleo kidogo katika baadhi ya maeneo, hali imezorota katika nafasi za uongozi wa juu bungeni. Idadi ya wanawake wanaoshika nafasi za uspika imepungua kwa kiasi kikubwa.
“Hivyo kuna mahali tunaenda vizuri, lakini kwingine tunarudi nyuma,” amesisitiza.
Wito wa mabadiliko ya kisheria na kikatiba
Dkt. Ackson ametoa wito kwa nchi kuchukua hatua madhubuti zaidi, ikiwemo kufanya mabadiliko ya kisheria na kikatiba ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi za uongozi.
Ametolea mfano mfumo wa Tanzania wa kutenga angalau asilimia 30 ya viti kwa wanawake, akisema njia kama hiyo inaweza kusaidia kuongeza ushiriki wao.
“Bado hatujafikia usawa wa kweli. Tafiti zinaendelea kuonesha hilo,” amesema, akionya dhidi ya mijadala ya kupunguza au kuondoa nafasi maalum kwa wanawake.
Aidha, amesisitiza kuwa lengo si tu kuongeza idadi ya wanawake bungeni, bali kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maamuzi na mijadala ya kimataifa.
Hatari ya ‘deepfakes’ kwa wanawake
Akijibu swali kuhusu ongezeko la matumizi ya teknolojia ya “deepfakes”—picha au video bandia zinazotengenezwa kwa akili mnemba na kuweka sura ya mtu asiyehusika—Dkt. Ackson amesema teknolojia hiyo inaleta changamoto kubwa, hasa kwa wanawake.
“Watu wanadhalilishwa kwa mambo yasiyo ya kweli, lakini madhara yake ni makubwa. Uongo unapanda 'lift' ukweli unapanda ngazi," ameeleza hayo akimaanisha kuwa uongo unasambaa haraka kuliko ukweli.
Ameonya kuwa hali hiyo inaweza kuwakatisha tamaa wanawake kushiriki katika siasa, kutokana na hofu ya kudhalilishwa mtandaoni.
Hatua za IPU na changamoto ya sheria
Dkt. Ackson amesema IPU imeanza kuchukua hatua kwa kupitisha azimio linaloweka misingi ya kusaidia mabunge kutunga sheria kuhusu matumizi ya akili mnemba.
Ameeleza kuwa teknolojia hiyo ina faida na hasara, lakini matumizi mabaya yanaweza kuathiri vibaya haki za binadamu, utawala bora na hata demokrasia, hasa wakati wa uchaguzi.
“Akili Mnemba inaweza kumpa ushindi mtu ambaye hakuchaguliwa kwa kupotosha ukweli,” ameonya.
Hata hivyo, amekiri kuwa nchi nyingi bado hazijachukua hatua madhubuti kwa sababu teknolojia hiyo inabadilika kwa kasi kubwa, hali inayofanya iwe vigumu kwa watunga sheria kwenda sambamba nayo.
Tofauti za kibaiolojia zisitumike kumkwamisha mtoto wa kike
Akihitimisha mahojiano, Dkt. Ackson ametoa wito kwa jamii kubadili mtazamo kuhusu mtoto wa kike, akisisitiza umuhimu wa kumuwekea mazingira sawa na mtoto wa kiume tangu utotoni.
“Mtoto wa kike anaweza kuwa chochote anachotaka. Tusitumie tofauti za kibaiolojia kama kikwazo cha maendeleo yake,” amesema.
Amesisitiza pia umuhimu wa usawa katika ajira na malipo, pamoja na kuondoa mitazamo hasi ya kijamii inayowakwamisha wanawake.
“Jamii nzima inapaswa kuhakikisha haimzuii mwanamke au msichana kufikia ndoto zake,” amehitimisha.