Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi 4000 Beni, DRC wanufaika na mradi wa maji safi uliofadhiliwa na MONUSCO

Mwanamke mmoja huko Beni, DRC, amemwaga maji kutoka kwenye kituo cha maji kilichopangwa hivi karibuni wakati wa mradi wa maji unaofadhiliwa na MONUSCO, huku wanajamii na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakitazama.
© MONUSCO/Sébastien Kitsa Wakazi 4000 Beni, DRC wanufaika na mradi wa maji safi uliofadhiliwa na MONUSCO.

Wakazi 4000 Beni, DRC wanufaika na mradi wa maji safi uliofadhiliwa na MONUSCO

Msaada wa Kibinadamu

Suala la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa vitongoji vya Mundubiena na Kahirimunda vilivyoko takribani kilometa 20 kutoka Beni, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) sasa limepata jawabu baada ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO kukamilisha mradi wa maji safi.

Kupitia wavuti wake, MONUSCO imesema kikosi chake cha kujibu mashambulizi au (FIB) ndio kimefadhili mradi huo wenye gharama ya dola takribani 40,000, ukijumuisha kisima kimoja na mikondo sita yenye mabomba ya maji.

MONUSCO inasema kwa miaka kadhaa, upatikanaji wa maji kwenye vitongoji hivyo ulikuwa changamoto kubwa na hivyo “kukamilika kwa mradi huu kumeleta ahueni kubwa kwa kaya ambazo awali wanafamilia walilazimika kutembea umbali mrefu kusaka maji safi.”

“Maji haya ni masafi mno, hayana vijidudu. Tulikuwa tunateka maji bondeni, lakini leo hii tunakunywa maji kutoka hapa kijijini. Tunatarajia kupata idadi kubwa ya watu hapa. Ni furaha kubwa leo,” amenukuliwa Astride Kahambu Vagheni, mwanamke mkazi wa eneo hilo huku tabasamu ikiwa dhahiri kwenye uso wake.

Projekti ya benki ya maji yenye nishati ya jua huko Beni, DRC, pamoja na wafanyakazi wa MONUSCO waliohudhuria tukio la jamii chini ya mahema ya bluu.
© MONUSCO/Sébastien Kitsa Wakazi 4000 Beni, DRC wanufaika na mradi wa maji safi uliofadhiliwa na MONUSCO.

Mradi huu utalinda wanawake

Pamoja na kuboresha mazingira, mradi huu pia unalenga kulinda raia. Katika eneo hilo ambalo limegubikwa na ukosefu wa usalama, safari ndefu za kusaka maji mara nyingi hutumbukiza wanawake na wasichana kwenye mashambulizi kutoka makundi yaliyojihami.

Flavien Nzanzu Muhindo, ambaye ni Chifu wa eneo hilo amesema, “Haya maji ni muhimu sana kwa sababu yanapunguza hatari. Ukatili wa kijinsia ni miongoni mwa hatari tunazopambana nazo hivi sasa. Wanawake mara nyingi wanalazimika kusindikizwa na wanaume pindi wanapokwenda kuteka maji umbali mrefu. Tuna zaidi ya wakazi 4,000 ambao watanufaika na mradi huu.”

Miezi minne ilitumika kukamilisha mradi huu ambao unanufaisha watu ambao wengi wao wamefurushwa makwao kutokana na mapigano mashariki mwa DRC.