Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yaidhinisha tiba ya kwanza ya malaria kwa watoto wachanga, huku ikiongeza zana za uchunguzi

Mwanamke akiwa amembeba mtoto kwa ajili ya mfanyakazi wa afya ili kumfanyia kipimo kwenye mkono wa mtoto huyo katika kambi moja nchini Malawi.
© UNICEF/Thoko Chikondi Mtoto wa miezi sita anapimwa malaria baada ya kimbunga Freddy kusababisha mafuriko na uharibifu nchini Malawi.

WHO yaidhinisha tiba ya kwanza ya malaria kwa watoto wachanga, huku ikiongeza zana za uchunguzi

Afya
  • Tiba ya mapinduzi kwa wagonjwa wadogo zaidi
  • Dawa inaitwa artemether-lumefantrine.
  • Inalenga watoto wenye uzito wa kati ya kilo 2 hadi 5
  • Awali ilikuwa vigumu sana kuwapatia matibabu
  • WHO imeidhinisha pia vipimo vitatu vipya vya haraka (RDTs) vya kubaini malaria

Leo ikiwa ni siku ya Malaria duniani habari njema ni kwamba sasa watoto wachanga na watoto wadogo hawatakuwa tena na changamoto ya tiba hidi ya malaria, kwa kuwa shirika la Afya Duniani (WHO) limechukua hatua ya kimapinduzi kwa kuidhinisha kwa mara ya kwanza tiba ya malaria iliyoundwa mahsusi kwa watoto hao na dawa hiyo si nyingine bali ni artemether-lumefantrine.

Tweet URL

Taarifa ya WHO iliyotolewa Geneva, Uswisi Aprili 24, siku moja kabla ya maadhimisho ya siku ya kutokomeza malaria duniani leo Aprili 25 inasema dawa hiyo inalenga watoto wenye uzito wa kati ya kilo 2  hadi 5, ikiziba pengo la muda mrefu katika huduma kwa kundi hili lililo hatarini.

Awali ilikuwa vipi?

Hapo awali, watoto wachanga walitibiwa kwa kutumia dawa zilizotengenezwa kwa ajili ya watoto wakubwa, hali iliyoongeza hatari ya makosa ya kipimo na madhara hatarishi. 

Uidhinishaji wa WHO unathibitisha kuwa tiba hiyo inakidhi viwango vya kimataifa vya usalama, ubora na ufanisi, na hivyo kufungua njia ya kupatikana kwa urahisi zaidi kupitia mifumo ya afya ya umma—hasa katika nchi za Afrika ambako maambukizi ya malaria ni makubwa.

Kuziba pengo muhimu la matibabu

Dawa hii mpya inatarajiwa kuwanufaisha mamilioni ya watoto wachanga wanaozaliwa kila mwaka katika maeneo yenye hatari kubwa. Kwa kuhakikisha kipimo sahihi na matumizi salama, tiba hiyo inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa madhara na vifo miongoni mwa watoto wachanga wanaoambukizwa malaria.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema, “maendeleo haya ni hatua kubwa. Ubunifu katika chanjo, uchunguzi na dawa unasaidia kubadili mwelekeo wa ugonjwa huo. Hata hivyo, dhamira endelevu ya kisiasa na ufadhili wa fedha ni muhimu ili kutokomeza malaria duniani.”

Vipimo vipya kukabili mabadiliko ya kijenetiki ya vimelea

Mbali na mafanikio ya tiba, WHO pia imeidhinisha vipimo vitatu vipya vya haraka (RDTs) ili kuboresha utambuzi wa malaria. Vipimo vilivyozoeleka hutegemea kubaini protini iitwayo HRP2 katika vimelea vya mbu Plasmodium falciparum

Hata hivyo, mabadiliko ya kijenetiki katika baadhi ya aina za vimelea yamepunguza ufanisi wa vipimo hivyo, huku matokeo hasi ya uongo yakifikia hadi asilimia 80 katika baadhi ya maeneo ya Pembe ya Afrika.

Vipimo vipya vinatambua protini mbadala, pf-LDH, ambayo haiathiriwi kirahisi na mabadiliko ya kijenetiki. WHO inapendekeza nchi zitumie vipimo hivi pale ambapo mbinu za HRP2 zinashindwa katika zaidi ya asilimia 5 ya wagonjwa wanaopimwa, ili kuhakikisha utambuzi sahihi na matibabu kwa wakati.

Maendeleo ya dunia yakikabiliwa na changamoto zinazoendelea

Taarifa hizo mpya za dawa kwa watoto na mbinu mpya za kuchunguza malaria zinaambatana na kampeni ya Siku ya Malaria Duniani 2026 yenye kaulimbiu “Tunaongozwa Kutokomeza Malaria: Sasa Tunaweza. Sasa Lazima.” 

Ingawa kumekuwa na mafanikio makubwa—ikiwemo kuzuia mabilioni ya maambukizi na kuokoa mamilioni ya maisha tangu mwaka 2000—takwimu za hivi karibuni zinaonesha juhudi za kimataifa zinapungua kasi.

Ripoti ya Malaria duniani mwaka 2025 inaonesha kuwa mwaka 2024 kulikuwa na takriban wagonjwa milioni 282 wa malaria na kati yao hao 610,000 walifariki dunia, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Sababu kama usugu wa dawa, usugu wa viuatilifu, na kupungua kwa ufadhili wa kimataifa zinatishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana.

Soma taarifa nzima hapa.

                              FAHAMU KUHUSU UHAKIKI WA AWALI WA DAWA NA CHANO

 Mpango wa WHO wa Uhakiki wa Awali (Prequalification) unalenga kuhakikisha kuwa bidhaa muhimu za afya zinazopaswa kununuliwa kimataifa zinakidhi viwango vya kimataifa vya ubora, usalama, ufanisi na utendaji.

Hatua  hii ya WHO inatokana na kwamba duniani kote, asilimia 70 ya nchi zina mifumo dhaifu au isiyotosheleza ya udhibiti au usimamizi wa dawa na chanjo. Hali ni ya kutia wasiwasi zaidi kwa bidhaa nyingine za afya, kama vile vipimo vya uchunguzi na vifaa vingine vya kitabibu.