FAO : Njaa yaongezeka duniani, watu milioni 266 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula
FAO : Njaa yaongezeka duniani, watu milioni 266 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula
Ripoti mpya ya kimataifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO iliyotolewa leo 24 Aprili 2026 imebaini kuongezeka kwa mgogoro wa njaa duniani, huku zaidi ya watu milioni 266 katika nchi na maeneo 47 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.
Ripoti hiyo ya Kimataifa kuhusu Migogoro ya Chakula (GRFC) iliyozinduliwa lmjini Roma Italia inaonyesha kuwa mwaka 2025 ulishuhudia viwango vya pili vya juu zaidi vya njaa kali kuwahi kurekodiwa, jambo linaloashiria hali mbaya na ya muda mrefu.
Mgogoro mkubwa na wa muda mrefu
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kiwango cha njaa si kikubwa tu bali pia kinaongezeka kwa ukali na kudumu kwa muda mrefu.
“Tuna hali ambapo jumla ya watu milioni 266 katika nchi na maeneo 47 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula. Lakini kinachotutia wasiwasi zaidi ni kiwango cha ukali na muda mrefu wa hali hii,” amesema Rein Paulsen, Mkurugenzi wa Ofisi ya Dharura na Mnepo wa FAO.
Ripoti inaonesha kuwa karibu nusu ya maeneo yenye migogoro ya chakula pia yanakabiliwa na matatizo ya lishe, yanayosababishwa na mchanganyiko wa lishe duni, magonjwa, na kuporomoka kwa huduma muhimu.
Watoto waathirika zaidi wa utapiamlo unaoongezeka
Ripoti inaonesha hali mbaya kwa watoto, ambapo watoto milioni 35.5 walikumbwa na utapiamlo mkali mwaka 2025 pekee karibu milioni 10 kati yao wakiwa katika hali mbaya zaidi ya utapiamlo inayohatarisha maisha.
Katika maeneo yaliyoathirika zaidi kama Gaza, Myanmar, Sudan Kusini, Sudan, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC migogoro iliyojikutanisha imewasukuma watu karibu na hatari kubwa ya vifo, hasa kwa walio katika mazingira hatarishi zaidi.
Uhaba wa takwimu waficha ukubwa halisi wa tatizo
Licha ya takwimu hizi za kutisha, FAO inaonya kuwa hali halisi inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na mapungufu ya ukusanyaji wa takwimu.
“Hatuoni maboresho katika hali ya uhaba wa chakula. Tunachoshuhudia ni mapengo ya takwimu,” ameeleza Paulsen.
“Pale ambapo kuna upungufu wa takwimu, hatuwezi kuelewa kikamilifu mahitaji na hali hii itadhoofisha juhudi zetu za pamoja za kuboresha uhakika wa chakula.”
Shirika hilo linasisitiza kuwa takwimu sahihi ni muhimu ili kupanga na kutekeleza hatua madhubuti za kukabiliana na tatizo hili.
Baa la njaa lathibitishwa Gaza na Sudan
Katika mojawapo ya matokeo ya kutisha zaidi, ripoti imethibitisha kuwepo kwa baa la njaa katika maeneo mawili Gaza na Sudan ndani ya mwaka mmoja, jambo ambalo halijawahi kushuhudiwa mara nyingi.
“Baa la njaa limethibitishwa katika maeneo mawili tofauti, Ukanda wa Gaza na Sudan na hii ni hali ya kutia wasiwasi mkubwa. Baa la njaa linahusiana moja kwa moja na migogoro,” ameonya Paulsen.
Mapigano yanayoendelea, mabadiliko ya tabianchi na hali tete ya uchumi wa dunia vinaendelea kuzidisha tatizo hili.
Upungufu wa ufadhili watishia juhudi za kukabili migogoro
Ripoti pia inaonesha kuwa kupungua kwa ufadhili wa kibinadamu kunadhoofisha juhudi za kukabiliana na njaa. FAO inasisitiza kuwa mchanganyiko wa misaada ya chakula na kusaidia uzalishaji wa kilimo ni njia yenye ufanisi zaidi.
“Tunapoziunganisha njia hizi ipasavyo, matokeo chanya katika uhakika wa chakula yanaweza kuwa mara 17 zaidi kuliko kutoa msaada wa chakula pekee,” amesema Paulsen.
Wakati mahitaji yakiongezeka na rasilimali zikipungua, FAO inatoa wito wa hatua za haraka na za pamoja ili kuzuia hali isizidi kuwa mbaya na kuimarisha mifumo ya chakula duniani.