FAO: Mawaziri wa Afrika Wakutana Nouakchott Kuharakisha mapambano dhidi ya njaa
FAO: Mawaziri wa Afrika Wakutana Nouakchott Kuharakisha mapambano dhidi ya njaa
Ukuaji wa Kiuchumi
Mawaziri wa kilimo kutoka kote barani Afrika wamekutana mjini Nouakchott, mji mkuu wa Mauritania, kujadili namna ya kuharakisha juhudi za kupunguza njaa kwa msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).
Mkutano wa 34 wa FAO kwa Kanda ya Afrika (ARC34) unalenga kuweka vipaumbele vitakavyoongoza mpango kazi na bajeti ya shirika hilo kwa miaka miwili ijayo, sambamba na mikakati ya muda wa kati ya kubadilisha mifumo ya chakula na kilimo barani Afrika
Vijana na wakulima wa Afrika ni nguzo kuu
Akifungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu amesisitiza umuhimu wa kutumia nguvu ya idadi kubwa ya vijana na nafasi ya wanawake katika kilimo ili kuleta mageuzi ya sekta hiyo.
“Nimeshuhudia mwenyewe dhamira ya viongozi wa Afrika, mnepo wa wakulima wake, hasa nguvu ya wakulima wanawake, pamoja na ubunifu na nguvu ya vijana wa Afrika,” amesema.
Amebainisha kuwa ni wakati wa kubadili simulizi ya kilimo cha Afrika kutoka ile ya changamoto na utegemezi kwenda kwenye fursa na mafanikio.
Teknolojia ni suluhisho la mabadiliko
Mkurugenzi Mkuu huyo wa FAO ameeleza kuwa teknolojia mpya zinaweza kuwa chachu ya mageuzi, zikisaidia kushinda vikwazo vya muda mrefu katika uzalishaji na usambazaji wa chakula.
“Naona mustakabali tofauti ambapo teknolojia kuanzia mbegu zinazostahimili ukame hadi huduma za ugani za kidijitali zinaweza kuvuka mipaka ya changamoto za zamani,” amesema Qu.
“Lazima tufungue uwezo mkubwa wa kilimo wa Afrika, si kwa unyonyaji bali kwa ubunifu.”
“Lazima tufungue uwezo mkubwa wa kilimo wa Afrika, si kwa unyonyaji bali kwa ubunifu.”
Ameongeza kuwa kwa uwekezaji sahihi, Afrika inaweza kuwa ghala la chakula duniani, ikitumia rasilimali zake nyingi za ardhi na maji.
Mgogoro wa njaa bado ni mkubwa
Hata hivyo, changamoto bado ni kubwa, amesema Qu huku takwimu zikionesha kuwa zaidi ya mtu mmoja kati ya watano barani Afrika alikuwa anakabiliwa na utapiamlo mwaka 2024, hali inayochochewa na mabadiliko ya tabianchi, migogoro na misukosuko ya kiuchumi.
Washiriki wa mkutano wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji wa ndani wa chakula ili kupunguza utegemezi na kuongeza mnepo dhidi ya mishtuko ya kimataifa.
Ufadhili na mageuzi ya kimuundo yapewa kipaumbele
Majadiliano pia yamejikita katika kuongeza uwekezaji na kuharakisha mageuzi ya sera ili kujenga mifumo imara ya chakula na kilimo, ikiwemo utekelezaji wa mkakati wa Kampala CAADP unaolenga kuongeza uzalishaji na biashara ya mazao ndani ya Afrika.
“Lazima tufanye kilimo kivutie si kama chaguo la mwisho bali kama sekta yenye faida, teknolojia ya juu na inayokua,” amesisitiza Qu.
Kutokana na changamoto za kifedha na kupungua kwa misaada ya maendeleo, FAO imezitaka serikali na wadau kuongeza juhudi za pamoja ili kuhakikisha Afrika inafikia malengo yake ya usalama wa chakula na kujenga mustakabali imara zaidi.
Mkutano huo wa siku nne ulioanza 13 hadi 17 April umeandaliwa na serikali ya Mauritania Chini ya kaulimbiu: Kuendeleza Mabadiliko ya Mifumo ya Chakula na Kilimo Barani Afrika: Bunifu