Makaburi ya pamoja Sudan Kusini yazua maswali mazito, Tume ya UN yataka uchunguzi huru
Makaburi ya pamoja Sudan Kusini yazua maswali mazito, Tume ya UN yataka uchunguzi huru
Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu nchini Sudan Kusini imetoa wito wa uchunguzi wa haraka na wa kina kufuatia kugunduliwa kwa mabaki ya binadamu katika Jimbo la Jonglei, ikionya kuwa huenda kuna gharama kubwa zaidi ya kibinadamu ya ghasia zinazoendelea kuliko inavyofahamika.
Katika taarifa iliyotolewa leo tarehe 17 Aprili 2026 mjini Juba na Geneva, tume hiyo imesema mabaki hayo yaligunduliwa wakati wa ujenzi wa barabara, huku mazingira ya vifo na mazishi yake yakibaki kuwa kitendawili.
Ripoti za makaburi zazua maswali mazito
Kwa mujibu wa taarifa za awali, miili hiyo huenda ni ya wapiganaji waliouawa katika mapigano ya awali, lakini uwezekano wa kuwepo kwa raia au waathirika wa ukiukaji wa haki za binadamu haujaondolewa.
Ugunduzi huo unakuja wakati mapigano mapya yakiripotiwa katika maeneo kama Akobo, ambako mapambano kati ya vikosi vya jeshi la ulizi la serikali ya Sudan na SPLA-IO yamekuwa yakibadilisha udhibiti wa maeneo.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Yasmin Sooka, amesema:
“Ugunduzi wa mabaki ya binadamu katika eneo la mgogoro ni jambo nyeti sana. Ni muhimu kushughulikia maeneo haya kwa umakini mkubwa ili kubaini ukweli na kuhakikisha haki inatendeka.”
Uchunguzi wa kisayansi wahitajika
Tume imesisitiza umuhimu wa kulinda maeneo hayo na kufanya uchunguzi huru, wa kitaalamu na usio na upendeleo, ikiwemo uchunguzi wa kisayansi, kwa kuzingatia viwango vya kimataifa kama 'Minnesota Protocol'.
Kamishna Barney Afako ameonya kuwa kushindwa kufuata taratibu kunaweza kusababisha kupotea kwa ushahidi muhimu unaoweza kusaidia kuwabaini wahusika, wakiwemo viongozi wa juu.
Hofu ya kuongezeka kwa ukiukaji
Tume imeonya kuwa kurejea kwa mapigano kunaashiria kudorora kwa makubaliano ya amani na huenda kukasababisha kuongezeka kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na uhalifu wa halaiki.
Aidha, imesisitiza kuwa chini ya sheria za kimataifa, mamlaka zina wajibu wa kuchunguza vifo vinavyoshukiwa kuwa vya kinyume cha sheria na kuhakikisha uwajibikaji.
Kamishna Carlos Castresana Fernández amesema, “familia zina haki ya kujua hatima ya ndugu zao. Haya si majukumu ya hiari bali ni wajibu wa kisheria.”
Wito wa hatua za haraka
Tume imetoa wito kwa mamlaka za Sudan Kusini kuruhusu uchunguzi huru na kushirikiana na wataalamu wa kimataifa ili kuhakikisha ukweli unafahamika na haki inatendeka.
Imesisitiza kuwa kulinda ushahidi, kufanya uchunguzi wa kitaalamu na kuwawajibisha wahusika ni hatua muhimu katika kuzuia kuendelea kwa ukiukaji na kurejesha imani ya wananchi.