Ukuaji wa Uchumi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wakabiliwa na mtihani mpya licha ya kuimarika: IMF
Ukuaji wa Uchumi Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara wakabiliwa na mtihani mpya licha ya kuimarika: IMF
Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara iliingia mwaka 2026 ikiwa na kasi kubwa zaidi ya ukuaji wa uchumi katika zaidi ya miaka kumi, ikichochewa na mazingira mazuri ya kimataifa na mageuzi ya ndani yaliyoendelea, kulingana na Shirika la Fedha Duniani IMF.
Akizungumza katika mikutano ya majira ya chipukizi ya IMF mjini Washington Marekani, Abebe Aemro Selassie amesema kanda hiyo ilirekodi ukuaji wa asilimia 4.5 mwaka 2025, huku nchi kama Ethiopia na Nigeria zikifaidika na mageuzi muhimu ya kiuchumi, yakiwemo marekebisho ya viwango vya ubadilishaji fedha, kupunguza ruzuku, na kuimarisha sera za fedha.
Vita vya Mashariki ya Kati vyasababisha mshtuko mpya wa kiuchumi
Hata hivyo, IMF inaonya kuwa mafanikio haya sasa yako hatarini kutokana na mshtuko mpya wa nje unaotokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, ambavyo tayari vinaathiri uchumi wa Afrika.
“Vita vya Mashariki ya Kati ni mshtuko mkubwa mpya wa nje. Bei za mafuta, gesi na mbolea zimepanda. Gharama za usafirishaji zimeongezeka. Biashara na washirika wa Ghuba imevurugika. Utalii na fedha za wahamiaji zinapungua,” amesema Selassie.
“Kwa hivyo tumepunguza utabiri wetu wa ukuaji hadi asilimia 4.3 mwaka 2026 na tunatarajia mfumuko wa bei wa wastani kufikia takriban asilimia 5 ifikapo mwisho wa mwaka.”
Ameongeza kuwa hali ngumu ya kifedha duniani inaongeza shinikizo zaidi, hasa kwa nchi zinazoagiza mafuta.
Athari zisizo sawa zaongeza udhaifu
IMF imesisitiza kuwa athari za mshtuko huu hazijasambaa kwa usawa katika kanda. Nchi zinazouza mafuta zinaweza kufaidika na mapato ya juu, lakini bado ziko hatarini kutokana na mabadiliko ya bei, huku nchi zinazoagiza mafuta hasa zile maskini na dhaifu zikikabiliwa na kuzorota kwa mizania ya biashara na kupanda kwa gharama za maisha.
“Madhara kwa binadamu bila shaka yatakuwa makubwa,” ameonya Selassie, akibainisha kuwa mgogoro huu mpya unaongeza shinikizo lililosababishwa na kupungua kwa misaada ya maendeleo.
Kupungua kwa misaada rasmi ya maendeleo kunaongeza mzigo zaidi, hasa kwa nchi zenye kipato cha chini zinazotegemea fedha za nje kugharamia huduma muhimu.
Kupungua kwa misaada kunaongeza shinikizo la muda mrefu
Tofauti na migogoro ya awali ambapo misaada ilirejea baadaye, IMF imeonya kuwa kupungua kwa sasa kunaonekana kuwa ni suala la kimuundo na la muda mrefu zaidi.
Hali hii inaathiri zaidi nchi zilizo hatarini, na kupunguza uwezo wao wa kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi na kuendeleza programu muhimu za kijamii na maendeleo.
Maamuzi ya sera ni muhimu kulinda mafanikio
Katika mazingira haya, IMF inazitaka serikali kuchukua hatua madhubuti lakini zenye uwiano ili kulinda mafanikio yaliyopatikana na kusaidia makundi yaliyo hatarini.
“Nchi lazima zidhibiti matarajio ya mfumuko wa bei na kulinda walio hatarini kupitia msaada unaolengwa na wa muda maalum,” amesema Selassie.
“Mikakati ya kifedha lazima iwe na uwiano kati ya uaminifu na unyumbufu. Nchi zinazouza mafuta zinapaswa kuchukulia mapato ya ziada kama ya muda na kujenga akiba, huku nchi zinazoagiza mafuta zikilinda matumizi ya kipaumbele na kuongeza mapato ya ndani.”
Amesisitiza kuwa kuharakisha mageuzi ya kimuundo kama kuboresha utawala, mazingira ya biashara, na masoko ya fedha ni muhimu ili kuchochea ukuaji unaoongozwa na sekta binafsi.
Ukuaji wa muda mrefu wategemea tija na ubunifu
Kwa mtazamo wa muda mrefu, IMF imeeleza umuhimu wa mabadiliko ya kina ya kiuchumi ili kukabiliana na changamoto sugu kama tija ndogo, ukosefu wa ujuzi unaohitajika, na udhaifu wa sekta binafsi.
“Ukuaji wa tija ndio lengo la muda mrefu. Matumizi sahihi ya teknolojia ya akili mnemba katika kilimo, afya na huduma za umma yanaweza kuleta mabadiliko makubwa,” amesema Selassie.
“Lakini kufikia hilo kunahitaji uwekezaji katika umeme wa uhakika, miundombinu ya kidijitali na ujuzi kanda imeonesha mnepo mkubwa, na mafanikio haya yanastahili kulindwa.”
Amemalizia kwa kusema kuwa IMF iko tayari kuendelea kusaidia nchi za Afrika kupitia ufadhili, ushauri wa sera na uimarishaji wa uwezo wakati zinapokabiliana na mazingira magumu ya uchumi wa dunia.