Baraza Kuu lajadili matumizi ya kura ya turufu katika mswada wa azimio kuhusu Mashariki ya Kati April 7
Baraza Kuu lajadili matumizi ya kura ya turufu katika mswada wa azimio kuhusu Mashariki ya Kati April 7
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekutana leo jijini New York Marekani kujadili matumizi ya kura ya turufu au “Veto” katika mswada wa azimio lililowasilishwa tarehe 7 Aprili kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati ikiwemo usafiri salama kwenye Mlango Bahari wa Hormuz.
Mswada huo wa azimio Aprili 7 uliungwa mkono na wajumbe wengi wa Baraza la Usalama isipokuwaUrusi na China ambao walitumia kura ya turufu kuupinga na hivyo kutopitishwa.
Mjadala wa Hormuz hautaishia kwa kura ya turufu: Rais wa Baraza Kuu
Kutokana na kushindwa kwa Baraza la Usalama kuunga mkono juhudi za kuhakikisha usafiri salama na usiozuiliwa katika Mlango Bahari wa Hormuz, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, akizungumza katika mkutano wa Baraza Kuu hii leo amesema sasa Baraza Kuu lina nafasi na wajibu wa kuhakikisha mjadala kuhusu uhuru wa usafiri hauishii kwenye kura ya turufu.
Bi. Baerbock ameongeza kuwa nchi wanachama zina fursa ya kuzungumzia mzozo unaoendelea, kuwawajibisha wajumbe wa Baraza la Usalama, na kuzikumbusha pande zote wajibu wao chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.
“Hakuna jambo la kinadharia kuhusu kuheshimu sheria za kimataifa,” amesema. “Kinachotokea katika eneo moja kina athari katika maeneo yote.”
Athari za kiuchumi na kibinadamu zazidi kuongezeka
Bi. Baerbock amebainisha kuwa bei za mafuta zimepanda kwa zaidi ya asilimia 40, huku usumbufu unaohusiana na mzozo huo ukiondoa hadi mapipa milioni 1.5 kutoka katika usambazaji wa dunia.
Aidha, usumbufu wa mbolea umeongeza ukosefu wa chakula kwa mamilioni ya watu walio katika mazingira magumu.
Shirika la Kimataifa la Fedha Duniani IMF pia imepunguza matarajio ya ukuaji wa uchumi wa 2026 na kuonya hatari ya mdororo wa uchumi duniani.
“Tunachoshuhudia si mgogoro mmoja, bali ni mkusanyiko wa migogoro mingi inayokutana,” alisema Baerbock, akirejelea pia mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia na kibiashara ambayo ni kinyume na sheria za kimataifa.
Urusi yafafanua kwa nini ilitumia kura ya turufu
Urusi ilipiga kura ya turufu dhidi ya rasimu ya azimio kuhusu hali ya Mlango wa Hormuz na maeneo jirani, kwa mujibu wa Naibu Balozi wa Kudumu wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa Anna Evstigneeva.
Amelaani kile alichokiita uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, akisema unakiuka Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, na kwamba baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama wamepuuza chanzo halisi cha mzozo.
Akieleza sababu ya kura ya turufu, amesema Baraza lilikuwa linaombwa “kuwasha taa ya kijani au kuidhinisha” kwa matumizi ya hatua fulani za ulinzi kwa kisingizio cha kuhakikisha usalama wa usafiri wa baharini.
Ameonya kuwa hatua hiyo ingekuwa “ruhusa kamil ya kuendelea kwa hali ya sasa na kuongezeka kwa mvutano”.
Rasimu mbadala ya “uwiano” yawasilishwa
Urusi na China ziliwasilisha rasimu mbadala iliyolenga kufanikisha suluhisho la mazungumzo, kwa msaada wa nchi kadhaa zikiwemo Pakistan.
Balozi huyo amesema hati hiyo kwa sasa iko “What’s in Blue” kwenye meza ya Baraza la Usalama, ikimaanisha kuwa imekamilika na iko tayari kupigiwa kura na wanachama wa Baraza hilo.
Fu Cong: China ‘imesimama upande sahihi wa historia’
“China inaichukulia kila kura katika Baraza la Usalama kwa mtazamo wa uzito, dhamira na uwajibikaji,” amesema Balozi Fu Cong Mwakililishi wa Kudumu wa China kwenye Umoja wa Mataifa, akibainisha kuwa nchi yake, pamoja na Urusi, zilipiga kura ya kupinga rasimu hiyo.
Amesema China inaipa umuhimu mkubwa rasimu iliyowasilishwa na Bahrain kwa niaba ya nchi za Ghuba, akisisitiza “Tunaelewa kikamilifu wasiwasi wao mkubwa.”
Wakati huo huo, ameeleza kuwa hatua za Baraza zinapaswa kulenga kupunguza mvutano na zisitoe “mwonekano wa uhalali kwa operesheni za kijeshi zisizoidhinishwa,” au “kutoa leseni ya matumizi ya nguvu,” hali inayoweza kuchochea zaidi mgogoro.
Kwa kutumia kura yake ya turufu, China imesema imelinda haki ya kimataifa, kulinda Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kuzuia mgogoro kupanuka na kuunda mazingira mazuri ya kusitisha mapigano kwa muda.
“kura ya China inaonesha chaguo la uwajibikaji kwa amani,” amesema. “Inasimama upande sahihi wa historia.”
Nchi za Ghuba kuwasilisha rasimu mpya
Naye Balozi Tareq Albanai Mwakilishi wa Kudumu wa Kuwait kwenye Umoja wa Mataifa, akizungumza kwa niaba ya Bahrain, Jordan, Qatar, Saudi Arabia na Emarati, amesema rasimu iliyowasilishwa tarehe 7 Aprili ilikuwa sehemu ya “hatua ya pamoja ya uwajibikaji na yenye malengo ya kushughulikia tishio la wazi na la moja kwa moja kwa amani na usalama wa kimataifa.”
Amesema inaonesha dhamira ya kufanya kazi ndani ya mifumo ya kimataifa husika.
Ameongeza kuwa juhudi “makini” zilifanyika katika mashauriano ya wiki tatu ili kufikia “maandishi yenye uwiano” yaliyozingatia wasiwasi wote, na kwamba matoleo sita yaliwasilishwa ili kutafuta muafaka.
Nchi hizo zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja na kuratibu kwa karibu na nchi wanachama kwa lengo la kuwasilisha rasimu mpya ya azimio itakayolenga kuhakikisha uhuru wa usafiri wa baharini.