Mashariki ya Kati: Jinamizi la kibinadamu linaendelea na athari za vita zavuka mipaka
Mashariki ya Kati: Jinamizi la kibinadamu linaendelea na athari za vita zavuka mipaka
• Amri za uhamisho zaongezeka Lebanon, ikosi vya Israel vyatoa onyo jipya kusini mwa Mto Zahrani
• Mgogoro wa kibinadamu wazidi kuongezeka, athari zafika Karibea
• Fedha za dharura zatolewa kwa Iran kupitia mfuko wa CERF
Mgogoro wa vita unaendelea kuwa mkubwa kote Mashariki ya Kati, huku operesheni za kijeshi za Israel zikiendelea nchini Lebanon baada ya mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali hizo mbili kufanyika Washington Marekani jana Jumanne.
Zaidi ya watu 2,000 nchini Lebanon wameripotiwa kuuawa tangu mapema Machi. Wakati huo huo, hali ya kutokuwa na uhakika inaendelea kuhusu njia muhimu ya usafirishaji ya Mlango Bahari wa Hormuz kufuatia vizuizi vya Marekani dhidi ya bandari za Iran, na athari za vita hivyo sasa zimefika visiwa vya Karibea.
Mahitaji yaongezeka Lebanon kufuatia amri ya uhamisho ya Israel
Jeshi la Israel limetoa tena amri ya dharura ya watu kuhama katika jamii zinazoishi kusini mwa mto Zahrani nchini Lebanon.
Onyo hilo la dharura lililotolewa kwa Kiarabu kupitia mtandao wa X leo Jumatano na Kanali wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linatangaza mashambulizi ya anga dhidi ya wapiganaji wa Hezbollah.
Wakazi wa kusini mwa Lebanon wametakiwa “kuondoka mara moja katika makazi yao na kuelekea kaskazini mwa mto huo”.
Mto Zahrani uko kaskazini mwa Mto Litani, ambao umekuwa mstari muhimu wa marejeo katika awamu zilizopita za mgogoro.
Hii inajiri wakati Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa (UNHCR), Barham Salih, akionya kuhusu kuongezeka kwa mahitaji nchini Lebanon kutokana na mapigano kati ya Israel na Hezbollah, na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuendelea kutoa msaada.
Iran: Janga la wakimbizi laongezeka huku mgogoro ukizidisha mahitaji
Kuongezeka kwa mapigano nchini Iran kumeongeza shinikizo kwa wakimbizi, huku mahitaji ya ulinzi na huduma za msaada yakiongezeka, kwa mujibu wa UNHCR.
Shirika hilo linasema simu kwa namba zake za msaada zimeongezeka sana tangu mwishoni mwa Februari, zikionesha hofu kubwa na hatari zinazobadilika miongoni mwa wakimbizi wa Afghanistan.
Masuala makuu ni pamoja na usalama, huduma za afya, ajira, hadhi ya kisheria na msaada wa afya ya akili. Wanawake na wasichana wako katika hatari kubwa zaidi, huku baadhi ya manusura wa ukatili wa kijinsia wakikosa huduma za ulinzi baada ya vituo vya polisi kufungwa kutokana na ukosefu wa usalama.
UNHCR pia inaonya juu ya hatari zinazoongezeka kwa kaya zinazoongozwa na wanawake, hasa wale waliopoteza kipato baada ya waajiri wao kukimbia.
Lebanon: Afisa wa UN asifu mazungumzo kama hatua muhimu
Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon, Jeanine Hennis-Plasschaert, amekaribisha mkutano kati ya Lebanon na Israel kama hatua muhimu kuelekea kumaliza uhasama unaoendelea.
Mkutano huo uliofanyika Washington, DC, uliashiria mawasiliano ya kwanza ya moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili katika karibu miongo mitatu, ukisimamiwa na Marekani.
Amesema ana matumaini kuwa juhudi hizo zitasaidia kuvunja mzunguko wa migogoro na kuelekea utulivu wa kudumu.
Ufurushwaji mkubwa wa watu Iran na kwingineko
Hapa ni muhtasari wa idadi ya watu waliolazimika kuhama makazi yao kutokana na vita Mashariki ya Kati tangu mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya Iran kuanza tarehe 28 Februari, kwa mujibu wa UNHCR:
• Iran: Takriban watu milioni 3.2 wamekimbia makazi yao ndani ya nchi, wengi wao Tehran ambako ni asilimia 75, huku wengine wakiwa Hormozgan, Bushehr na Khuzestan. Nchi hiyo pia inahifadhi wakimbizi milioni 1.65, wengi wao wakiwa Waafghanistan.
•Uturuki: Takriban Wairan 110,400 walikimbilia nchi jirani, hasa Uturuki, ingawa 87,600 tayari wamerudi. Wengi ni wanawake na watoto.
• Lebanon: Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao ndani ya nchi na asilimia 35 ni watoto, huku takriban watu 140,700 wakiishi katika makazi ya pamoja.
• Syria: Takriban Wasyria 236,800 na Walebanon 43,900 wamevuka kutoka Lebanon kwenda Syria. Wengi wanapanga kurejea kwa kudumu.
• Afghanistan: Takriban Waafghanistan 134,100 wamerudi kutoka Iran na Pakistan, huku 115,000 wakiendelea kuwa wakimbizi wa ndani. Wengi wao ni wanawake na watoto.
Dola milioni 12 zatolewa na CERF kusaidia Iran
Kadiri mahitaji yanavyoongezeka nchini Iran, juhudi za Umoja wa Mataifa zimetoa nyongeza ya dola milioni 12 kupitia Mfuko wa Dharura wa Kukabiliana na Majanga CERF.
Katibu Mkuu António Guterres amesema fedha hizo zitasaidia watu walio katika hali mbaya wanaohitaji msaada wa haraka.
Mfuko wa CERF ulianzishwa mwaka 2005 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha misaada ya haraka inawafikia watu waliokumbwa na majanga.
Athari za vita Mashariki ya Kati zafika Karibea
Wiki sita tangu vita kuanza Mashariki ya Kati, athari zake sasa zimefika eneo la Karibea, ambalo tayari linakabiliwa na changamoto kubwa na hofu ya janga la tabianchi linalohusishwa na El Niño.
Watafiti wa Umoja wa Mataifa wanaonya kuwa vita hasa mgogoro wa Mlango Bahari wa Hormuz vimesababisha mshtuko mkubwa wa nishati na biashara duniani, unaofanana na ule wa janga la coronavirus">COVID-19 na vita vya Ukraine mwaka 2022.
Kaya zenye kipato cha chini ndizo zitaathirika zaidi, kwa mujibu wa uchambuzi uliotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, baada ya bei ya mafuta ghafi kupanda hadi zaidi ya dola 114 kwa pipa, pamoja na gharama za usafirishaji na ucheleweshaji wa bidhaa.
Hata kama kuna makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano, wataalamu wanasema hali ya kutokuwa na uhakika bado ni kubwa na Karibea, inayotegemea sana uagizaji wa chakula, inaathirika haraka.
Wakati huo huo, wataalamu wanaonya kuwa kuna uwezekano wa asilimia 61 wa tukio la El Niño katikati ya mwaka 2026, ambalo kihistoria huleta mawimbi ya joto, ukame na upungufu wa mazao katika eneo hilo.
Kwa familia ambazo tayari zimeathiriwa na miaka ya migogoro, hali inaonekana kuwa mbaya zaidi.