Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Zaidi ya watoto 245 wameuawa au kujeruhiwa nchini Sudan tangu Januari hadi Machi mwaka huu

Mwanamke na watoto wake wanakaa pamoja katika makazi ya muda huko Kordofan Kusini, Sudan, waliohamishwa na mgogoro unaoendelea na wanahitaji msaada wa kibinadamu.
© UNICEF Mama na watoto wake wameketi kwenye makazi ya muda juu ya mlima huko Kordofan kusini.

UNICEF: Zaidi ya watoto 245 wameuawa au kujeruhiwa nchini Sudan tangu Januari hadi Machi mwaka huu

Amani na Usalama

Baada ya miaka mitatu ya vita nchini Sudan, watoto wameendelea kubeba mzigo mzito wa maafa hayo ambapo mashambulizi ya ndege zisizo na rubani au droni yamesababisha takriban asilimia 80 ya majeruhi na vifo vya watoto nchini humo.

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa leo mjini Port Sudan nchini Sudan na New York, Marekani, imechambua takwimu hizo ikionesha kuwa takriban watoto 160 wameuawa na wengine 85 wameachwa na ulemavu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 50 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025 huku zaidi ya watoto milioni 5 wamefurushwa makazi yao, mara nyingi kwa kujirudia.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amesema, “Kwa muda wa miaka mitatu, watoto kote Sudan wameuawa, wamejeruhiwa, na kufurushwa makazi yao kwa viwango vya kutisha. Nyumba zao, shule na hospitali zimeendelea kushambuliwa. Hakuna uhalali wa ukatili dhidi ya watoto; hii ni ishara kwamba pande zote zinazopigana zimeshindwa kabisa kulinda haki za msingi za watoto."

Mauaji sambamba na ukiukwaji wa  haki za watoto

Tangu kuanza kwa vita, Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto 5,700 kote Sudan, huku idadi kubwa ya vifo ikirekodiwa katika majimbo ya Darfur na Kordofan.

Maelfu ya familia zinaishi katika mazingira ya hatari na yaliyosongamana, huku huduma za msingi zikifikia kikomo na maeneo mengi ya nchi yakikosa misaada ya kibinadamu kutokana na ukosefu wa usalama na miundombinu iliyoharibika. Hali hii imesababisha njaa na magonjwa kusambaa kwa kasi, ambapo baa la njaa tayari limethibitishwa katika miji ya Al Fasher na Kadugli.

Hakuna lishe bora na theluthi moja ya shule zimefungwa

Uhaba wa chakula na vikwazo vya upatikanaji wa misaada vimeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya watoto wenye utapiamlo, ambapo inakadiriwa kuwa watoto milioni 4.2 watasumbuliwa na utapiamlo mkali mwaka 2026, ikiwemo kesi hatari zaidi ya 825,000 zinazoweza kusababisha vifo zisipotibiwa haraka.

Aidha, haki ya watoto kupata elimu imepata pigo kubwa kwani zaidi ya theluthi moja ya shule nchini Sudan zimefungwa, na asilimia 11 nyingine zinatumika kama hifadhi ya wakimbizi au kukaliwa na wapiganaji, hali inayowaacha watoto milioni 8 nje ya shule.

Licha ya hatari zilizopo, UNICEF imeendelea kutoa huduma za kuokoa maisha za afya, lishe, na maji, lakini mahitaji ni makubwa kuliko uwezo uliopo. Kwa mwaka 2026, shirika hilo linahitaji dola milioni 62.9 ili kuwafikia watoto milioni 7.9, lakini hadi kufikia Machi, ni asilimia 16 tu ya fedha hizo zimepatikana.

Wito kuwanusuru watoto wa Sudan

Bi.  Russell ametoa wito wa dharura kwa jamii ya kimataifa kuongeza msaada wao ili kukabiliana na mateso ya watoto nchini Sudan.

“Kulinda watoto kunahitaji pande zote kwenye mzozo kusitisha mara moja ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto na kuzingatia sheria za kimataifa, ikiwemo kuruhusu upatikanaji wa msaada wa kibinadamu kwa usalama na haraka kote nchini. Tunashukuru wafadhili wanaounga mkono kazi yetu ya kuokoa maisha, lakini mahitaji ya kibinadamu yanaendelea kuzidi ufadhili uliopo, na tunatoa wito wa dharura kwa jamii ya kimataifa kuimarisha msaada wake. Hatuwezi kupuuza mateso ya watoto nchini Sudan,” amesema Bi. Russell.