Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuvurugika kwa meli kupita katika mlango habari wa Hormuz kunazua wasiwasi kuhusu bei za chakula na minyororo ya usambazaji duniani

Mtazamo wa Pwani Nyekundu kwenye kisiwa cha Hormuz nchini Iran, ikionyesha pwani yenye mchanga wa rangi ya waridi na miamba nyekundu ikikutana na maji ya rangi ya turquoise chini ya anga ya bluu.
© Unsplash Mlango-Bahari wa Hormuz unaunganisha Ghuba ya Persian na Ghuba ya Oman.

Kuvurugika kwa meli kupita katika mlango habari wa Hormuz kunazua wasiwasi kuhusu bei za chakula na minyororo ya usambazaji duniani

Ukuaji wa Kiuchumi

Wakati mazungumzo ya kumaliza vita huko Mashariki ya Kati baina ya Marekani na Iran yakigonga mwamba mwishoni mwa wiki, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limeonya kuwa kuvurugika kwa meli kupita katika mlango Bahari wa Hormuz kunaleta hatari zinazoongezeka si tu kwenye nishati bali pia katika mifumo ya chakula duniani. 

Mlango Bahari wa Hormuz umefungwa tangu tarehe 28 Februari siku ambayo vita rasmi ilianza baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran na kisha Iran kujibu Mashambulizi na sasa mzozo huo umesambaa eneo zima la Mashariki ya Kati. 

Mpaka kufikia leo Aprili 13, meli bado hazijasonga kwa idadi kubwa, Iran inaruhusu meli chache kupita kwa siku. Meli za mwisho kuondoka kabla ya kizuizi kuwekwa ndio zitakuwa zinafika mahali zinapoelekea, ikimaanisha kuwa pengo halisi la usambazaji linaanza kuonekana.

Sasa kwanini mlango huu unazungumziwa sana? Nikwasababu ndiko hasa kunakopitishwa, asilimia 30 hadi 35 ya mafuta ghafi duniani, asilimia 20 ya gesi asilia inayotumika katika uzalishaji wa mbolea na sehemu kubwa ya pembejeo muhimu za kilimo, na hadi asilimia 30 ya mbolea zinazouzwa kimataifa.

Mwanamume mwenye miwani akizungumza kwenye kipaza sauti mbele ya ramani ya ulimwengu inayoonyesha tahadhari za mafuriko.
© FAO Maximo Torero, ni mchumi mkuu wa FAO

Sasa hii leo Mtaalamu Mkuu wa uchumi wa chakula wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO Máximo Torero amezungumzia athari zinazotokea kwenye sekta ya kilimo kufuatia mzozo huo wa Mashariki ya Kati. 

Maximo anasema kwanini ni muhimu sana kufungulizwa kwa mlango Bahari sasa hivi 

“Ni muhimu sana kwasababu  muda unaposonga, kila kitu kinachohusiana na kilimo kinahusiana na kalenda ya kilimo, ikiwa hatufuati kalenda ya mazao na hatuna pembejeo kwa wakati unaohitajika kwa kupanda, ina maana kwamba wazalishaji watalazimika kuzalisha kwa pembejeo chache na hapo tunaweza kuwa na mavuno machache ambayo yangeathiri msimu ujao au mwaka ujao.”

Sasa wakati juhudi za kidiplomasia zikiendelea kila mahali kuhakikisha Suluhu inapatikana, Mchumi huyu Mkuu wa FAO anasema nini serikali na wadau wengine wanapaswa kufanya kwa wakati huu? 

“Mosi tunahitaji kutafuta njia za kuepuka vikwazo vya usafirishaji nje hasa vilivyowekwa kwenye mbolea na nishati na pengine siku zijazo tutatakiwa kuondoa vikwanzo vilivyoweka  kwenye  bidhaa nyingine ....Pili, tunahitaji kutafuta njia za kusaidia kaya zilizo katika mazingira magumu na hapo ndipo serikali zinaweza kupata msaada kutoka kwa mashirika ya kifedha ili waweze kuwa na kinga kupitia programu za ulinzi wa hifadhi ya jamii . Kingine,  tunahitaji kuzingatia misaada ya  kibinadamu kwa sababu hawa hawana kinga ya kuwalinda, na bila shaka jingine ni kuwa tunahitaji kuanza kutambua vyakula mbadala, lakini hizi ni hatua za muda mfupi.”

FAO inaamini kuwa suluhu za kidiplomasia na sera sahihi zikifanyiwa kazi hivi sasa, basi zitasaidia kudhibiti hali ya sasa na kuizuia isigeuke kuwa mgogoro wa chakula duniani.