UNMISS yaimarisha ulinzi wa amani kwa ukarabati wa barabara Malakal
UNMISS yaimarisha ulinzi wa amani kwa ukarabati wa barabara Malakal
Kufuatia mafuriko makubwa yanayoendelea kuharibu miundombinu na kukwamisha ulinzi wa amani huko jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini humo ,UNMISS unaendelea kujitahidi kukarabati miundombinu kama njia mojawapo ya kuongeza ustahimilivu na kuchochea amani.
Katika jimbo la Upper Nile, karibu na mji wa Malakal, video ya UNMISS inaonesha maeneo yaliyofurika maji, nyumba nyingi zikiwa zimetwama na wakazi wakitumia mashua ndogo kuhama.
Daniel Deng, mvuvi na kiongozi wa jamii, anaelezea hali ilivyo:
“Palikuwa na nyumba nyingi katika eneo hili, lakini mafuriko yamekuwa hivi kwa miaka mitano sasa na watu hawana furaha.”
Sasa tunaona wahandisi wa kikosi cha India wanaohudumu UNMISS wakikarabati barabara iliyoharibiwa kwa kiasi kikubwa na mafuriko. Kando ya barabara, maji ya mafuriko yanaendelea kutiririka, huku malori ya kubeba mchanga yakimwaga vifusi ili kuinua na kuimarisha njia. Maafisa wa ulinzi wamesimama pembeni wakihakikisha usalama wakati kazi ikiendelea.
Afisa wa kikosi cha uhandisi kutoka India, Meja Swamynath Gokulakannan, anaeleza hatua zilizochukuliwa:
“Kwa sababu ya maji mengi, barabara kuu ya usafirishaji haikuweza kutumika tena, hivyo timu yetu ilifanya uchunguzi kadhaa kuanzia Januari 15 na kubuni njia mpya. Tumekamilisha barabara ya kilomita 154, ikijumuisha kilomita 120 za njia mpya na kilomita 34 za barabara ya zamani ya MSR”
Baada ya tathmini ya kina ya ardhi, wahandisi walilazimika kuacha sehemu zilizokuwa chini na kujenga njia mbadala juu zaidi ili kuepuka maji ya Mto Nile yaliyoongezeka.
Barabara hiyo mpya sasa inawezesha jamii kusafiri kwa usalama, kuimarisha biashara na kusaidia juhudi za kujenga amani.
Video inaonesha kazi ikiendelea, huku mashine nzito za ujenzi zikitumika kutengeneza barabara. Katika eneo hili pia, wakazi wanaonekana wakisafiri pamoja na mifugo yao. Daniel anarejea tena.
“Kulikuwa na nyumba nyingi katika eneo hili, lakini mafuriko yamekuwa hivi kwa miaka mitano sasa na watu hawana furaha.”
Magari maalum ya kuvuka maeneo magumu (ATVs) yanaonekana yakipita katika maji, yakionesha changamoto ya usafiri katika mazingira hayo.
Mwanajamii mwingine anaelezea manufaa ya barabara hiyo mpya akisema…. “Barabara hii mpya ni fupi zaidi kuliko ile ya zamani ya majini. Ikiwekewa udongo mweupe juu, magari yataweza kupita bila shida hata wakati wa mvua.”
Hapo awali, uharibifu wa barabara kutokana na mafuriko ulikwamisha walinda amani kufikia maeneo yenye mzozo.
Mkuu wa ofisi ya UNMISS mjini Malakal, Alfred Orono Orono, anasisitiza umuhimu wa barabara hii inayokarabatiwa katika kudumisha amani:
“Barabara hii ni ya amani. Ni ishara kuwa amani imerejea Upper Nile, na UNMISS ina jukumu muhimu kuhakikisha amani inaendelea kudumishwa, watu wanarejea makwao na biashara pamoja na huduma zinaanza kusafirishwa kati ya Malakal na Renk hadi maeneo mengine.”
Picha zinaonesha wanawake na watoto wakitembea kwenye barabara mpya, huku wahandisi wakiendelea na kazi chini ya ulinzi wa walinda amani.
Ingawa miundombinu kama hii huonekana ya kawaida katika nchi zilizoendelea, nchini Sudan Kusini ambako vita vya muda mrefu na ukosefu wa uwekezaji vimeathiri sana maendeleo, juhudi hizi za UNMISS zinachangia kuokoa maisha na kuboresha hali ya maisha ya wananchi.