Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa Sudan waingia mwaka wa nne huku mamilioni wakikabiliwa na njaa na ukosefu wa makazi

Watu wanaotafuta makazi katika eneo la uhamiaji la Tawila nchini Sudan. Wanawake na watoto wamesimama chini ya mahema ya muda katika eneo kavu na lenye vumbi huku UNHCR na washirika wake wakitoa msaada wa kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na makazi, vitu vya msingi, na ushauri kwa wale waliojilazimisha kuondoka El Fasher.
© HOPE Kambi ya wakimbizi wa ndani wa Sudan katika kituo cha muda huko Tawila baada ya kukimbia El Fasher na maeneo yake ya karibu ya Kaskazini mwa Darfur mnamo Oktoba 2025.

Mgogoro wa Sudan waingia mwaka wa nne huku mamilioni wakikabiliwa na njaa na ukosefu wa makazi

Amani na Usalama

Wakati vita nchini Sudan ikiingia mwaka wake wa nne, mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa mgogoro huo unaendelea kusababisha mateso makubwa kwa mamilioni ya watu, huku wengine wakikimbia makazi yao na njaa ikifikia viwango vya kutisha.

Akiongea na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Sudan, Marie-Helene Verney, amesema “tangu kuanza kwa vita mwezi Aprili 2023, takribani watu milioni 14 wamelazimika kukimbia makazi yao. Kati yao, milioni 9 bado wako ndani ya Sudan huku zaidi ya milioni 4.4 wakikimbilia nchi jirani, hali inayofanya mtu mmoja kati ya wanne nchini humo kuwa ameathirika na amekimbikia makazi yake.

Amesema mapigano yanaendelea katika maeneo mengi ikiwemo Darfur, Kordofan na Blue Nile, huku mashambulizi ya anga na matumizi ya ndege zisizo na rubani yakiongezeka na kusababisha watu zaidi kukimbia.

Athari kwa wanawake na watoto

Verney ameongeza kuwa “raia wanakumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ukiwemo ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, utekaji, mauaji na kukamatwa kiholela. Wanawake na wasichana wako katika hatari kubwa zaidi, hasa wanapopita katika maeneo yasiyo salama, wakati mifumo ya afya, sheria na haki ikidorora.”

Kwa mujibu wa UNHCR, watoto wameendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa, huku mamilioni wakikosa elimu kwa zaidi ya miaka mitatu na zaidi ya watoto 58,000 wakivuka mipaka wakiwa peke yao baada ya kutengana na familia zao wakati wa kukimbia mapigano.

WFP kurejea Khartoum

Kwa upande mwingine, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limetangaza kurejea kwa ofisi yake ya kitaifa katika mji mkuu Khartoum baada ya miaka mitatu tangu ofisi zake kuharibiwa mwanzoni mwa vita mwaka 2023.

“Tumeshuhudia mabadiliko makubwa Khartoum ikilinganishwa na ziara yangu ya mwisho chini ya miezi sita iliyopita. Kuna uhai zaidi, uwanja wa ndege unafanya kazi, na watu wanarejea nyumbani na kuanza kujenga upya maisha yao,” amesema Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau.

Hata hivyo, ameonya kuwa mapigano bado yanaendelea katika maeneo mengi ya Sudan, huku takribani watu milioni 19 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, na kuifanya Sudan kuwa na mgogoro mkubwa zaidi wa njaa duniani.

“WFP iko tayari kufanya zaidi, lakini tunahitaji haraka ufadhili. Tunataka kuwafikia watu wengi zaidi kwa msaada wa chakula unaookoa maisha na kusaidia watoto na akina mama wanaokabiliwa na utapiamlo,” ameongeza Skau.

Shirika hilo linahitaji zaidi ya dola milioni 600 za Marekani ili kuendeleza operesheni zake katika miezi sita ijayo, wakati akiba ya chakula ikitarajiwa kuisha ndani ya wiki chache zijazo.

Hali bado ngumu

Licha ya baadhi ya Wasudan kuanza kurejea katika maeneo yao, hasa katika majimbo ya Al Jazeera, Sennar na Khartoum, hali ya maisha bado ni ngumu kutokana na uharibifu mkubwa wa miundombinu, huduma za msingi na uchumi.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa bila msaada wa haraka na wa kutosha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, mateso ya mamilioni ya Wasudan yataendelea kuongezeka, na kuathiri pia utulivu wa ukanda mzima.