Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kijana Ahmad Omar aongoza mabadiliko ya kijani shule ya Kisiwandui Zanzibar

Kikundi cha watoto wa shule za Kiafrika wakiwa wamevaa sare, baadhi yao wakiwa wamevaa hijabi, wakitunza mimea katika bustani ya shule huko Zanzibar, Tanzania.
© UNICEF Utunzaji wa Mazingira kwa wanafunzi Zanzibar.

Kijana Ahmad Omar aongoza mabadiliko ya kijani shule ya Kisiwandui Zanzibar

Tabianchi na mazingira

Elimu imepata maana mpya kwa wanafunzi wa shule ya msingi Kisiwandui iliyopo Zanzibar nchini Tanzania, ambapo sasa masomo ya uhifadhi wa mazingira hayajaishia darasani pekee bali yamegeuka kuwa vitendo. Kupitia mradi wa ROTA unaotekelezwa na Shirika la Wakfu wa Elimu juu ya Mengine Yote kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF nchini humo. Rashid Malekela anatupeleka visiwani Zanzibar kufahamu jinsi kijana Ahmad Omar Mohammed anavyoongoza wenzake katika mabadiliko haya.

"Kwangu mimi mazingira yana umuhimu mkubwa tena sana." Anasema Ahmad, kijana mdogo anayesoma katika shule ya msingi Kisiwandui. Video ya UNICEF inaonesha mimea ya kijani iliyostawi na kupendeza imeizunguka shule hii, kisha Ahmad aliyezungukwa na wanafunzi wenzake wenye furaha, anawaongoza kumwagilia maji kwenye bustani ya maua.

Kila asubuhi, Ahmad huanza siku yake kwa kuangalia ustawi wa bustani. Kwake, kila ua linalochanua ni ishara ya uhai. Baada ya kumwagilia bustani Ahmad anasema amekuwa akijihisi mwenye amani anapoona majani yakiwa na rangi ya kijani kibichi.

"Mazingira ambayo ni miti yanatupatia sisi hewa. Kwa hiyo nikiangalia mfano kama hapa majani yameota kijani kibichi, maua yanapendeza ya kila aina ya rangi"

Mvulana mdogo wa Kiafrika aliyevaa sare nyeupe ya shule anatabasamu mbele ya kamera akiwa na mikono kwenye kifua chake, akiwa amevaa kipaza sauti kidogo. Yeye yuko nje huko Zanzibar, Tanzania, kama sehemu ya mpango wa UNICEF wa uhifadhi wa mazingira na elimu.
© UNICEF Ahmad, kijana mdogo anayesoma katika shule ya msingi Kisiwandui anahamasisha wanafunzi katika utunzaji wa mazingira Zanzibar.

Ahmad hajaishia kupanda miti pekee, anawakusanya wanafunzi wenzake na kutukaribisha kufahamu mengi Zaidi.

"Njooni tuwaoneshe jinsi tunavyotunza mazingira katika skuli yetu ya Kisiwandui"

Wanafunzi wanaokota taka na kung’oa majani yaliyoota ndani ya bustani, kisha wanaelekea kwenye bwawa la samaki lililopo shuleni hapo, Ahmad amejikita zaidi katika usimamizi wa bwawa hilo, anasema kazi hiyo imeongeza ujuzi wa kutunza viumbe hai.

"Bwawa hili tunafuga samaki na tunawalisha. Pia tumejifunza mengi jinsi ya kufuga samaki. Kitu ambacho nakipenda zaidi katika shule yangu ni kutunza mazingira. Kama unavyoona sasa hivi tunapata mvua nzuri, afya iko vizuri. "

Akizungumzia changamoto, Ahmad amewataja watu wanaokata miti na kutupa taka hovyo, jambo ambalo analipinga.

"Kuna watu wengine wanakuwa wanatupa taka ovyo, wanakata miti ovyo. Yaani anakata anaacha, hajui huku analeta ukame. Ukitunza mazingira utajitoa katika maradhi."

Juhudi hizi za Ahmad ni kielelezo cha matokeo chanya, ambapo sasa wanafunzi wanajifunza kwa vitendo jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.