Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti: Mgawanyiko wa dunia unazidisha uhaba wa fedha za maendeleo

Wafanyakazi wawili waliovaa vazi la usalama na kofia wanafanya kazi kwenye njia ya udongo kando ya mfereji wa umwagiliaji katika shamba la kilimo la kijani huko Ambondromisotra, Madagaska, kama sehemu ya mradi wa HIMO wa ILO.
© ILO/Zoll Rabe Wanaume wanafanya kazi kwenye bomba la maji la Ambondromisotra nchini Madagaska

Ripoti: Mgawanyiko wa dunia unazidisha uhaba wa fedha za maendeleo

Ukuaji wa Kiuchumi

Hizi ndizo changamoto nchi zinazoendelea wanakabiliana nazo

• Mzigo mkubwa wa madeni

• Kupungua kwa misaada ya kifedha

• Kupungua kwa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI)

Ripoti mpya iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa imeonya kuwa mwenendo wa ufadhili wa maendeleo duniani unaelekea katika mwelekeo mbaya, hali inayotishia kurudisha nyuma mafanikio yaliyopatikana kwa miongo kadhaa.

Ripoti hiyo ya ufadhili wa miradi ya maendeleo Financing for Sustainable Development Report 2026 (FSDR 2026) iliyotolewa na Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UNDESA) imeeleza kuwa ushirikiano wa kimataifa unaendelea kudhoofika kutokana na ongezeko la mivutano wa kisiasa, vikwazo vya biashara, pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi, hali inayozorotesha juhudi za kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hasa katika nchi zinazoendelea barani Afrika.

Janga la deni
UNCTAD

Gharama kubwa za kukopa

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi nyingi zinazoendelea zinakabiliwa na pengo kubwa la fedha za kutekeleza SDGs, huku zikikumbwa na kupungua kwa misaada, gharama kubwa za kukopa, pamoja na mzigo mkubwa wa madeni. 

Takwimu zinaonesha kuwa huduma ya madeni ilifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka 20 mwaka 2024, wakati misaada ya maendeleo ilipungua kwa asilimia 6 na inatarajiwa kushuka zaidi mwaka 2025.

Akizungumzia ripoti hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, amesema mshikamano wa kimataifa ni muhimu ili kuzuia hali hiyo kuzidi kuwa mbaya. “Maendeleo ya kimataifa yanahitaji kufanya kazi pamoja kwa malengo ya pamoja ili kuepuka kurudisha nyuma mafanikio ya kile kilichojengwa kwa bidii.”

Bi. Mohammed ambaye ndio muangalizi mkuu wa utekelezaji wa Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu SDGs ambayo dunia imejiwekea lengo la kuyafikia ifikapo mwaka 2030 ameongeza kuwa utekelezaji wa makubaliano ya Sevilla ni fursa muhimu ya kuhamasisha rasilimali zinazohitajika kufikia SDGs.

Ongezeko la kasi la ushuru kwa nchi masikini

Ripoti hiyo pia inaonesha kuwa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) ulipungua kwa asilimia 11 mwaka 2024, huku ushuru wa bidhaa kutoka nchi maskini ukiongezeka kwa kasi, jambo linaloathiri biashara na ukuaji wa uchumi katika mataifa hayo.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa -UNDESA, Li Junhua, amesema: “Huu ni wakati hatari sana kwa ushirikiano wa kimataifa, kwani masuala ya kijiografia na kisiasa yanazidi kuunda uhusiano wa kiuchumi na sera za kifedha.”

Hata kabla ya usumbufu wa hivi karibuni wa kiuchumi uliosababishwa na kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz, (baada ya Marekani na Israel kuishambulia Iran na kisha Iran kujibu mashambulizi na mzozo huo kusambaa eneo zima la Mashariki ya Kati) mvutano wa kibiashara na kijiografia ulikuwa umesababisha ongezeko kubwa la ushuru na kuweka gharama za kiuchumi kwa nchi zinazoendelea.

Wanaume wanaweka paneli za jua katika Jimbo la Borno, Nigeria.
© UNICEF/Damilola Onafuwa Wanaume wanaweka paneli za jua katika Jimbo la Borno, Nigeria.

Mafanikio yaliyoanishwa

Ripoti hiyo imebaini kuwa bado kuna mafanikio katika baadhi ya maeneo, ikiwemo uwekezaji katika nishati jadidifu ambao ulifikia kiwango cha juu zaidi duniani mwaka 2024, ukiwa dola trilioni 2.2.

Pamoja na changamoto hizo, Umoja wa Mataifa unasisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na kutekeleza kikamilifu makubaliano ya Sevilla, makubaliano yaliyolenga kuziba pengo la dola trilioni 4 kwa mwaka la ufadhili wa maendeleo.

“Tunahitaji kuja pamoja na kutumia makubaliano ya Sevilla kama chachu ya kuchukua hatua na kuhakikisha tunafanikisha mustakabali endelevu kwa wote,” amesema Li Junhua.

Ripoti hiyo itajadiliwa zaidi katika mkutano wa Baraza la Uchumi na Jamii la Umoja wa Mataifa (ECOSOC) utakaofanyika baadae mwezi huu wa Aprili 2026, ukilenga kutafuta suluhisho la kuongeza rasilimali za maendeleo kwa nchi zinazoendelea.

Unaweza kusoma ripoti hii kwa urefu kwa kutembelea hapa