Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pengo la ufadhili latishia maisha ya wakimbizi wa Sudan nchini Chad

Kikundi cha wanawake wa wakimbizi wa Sudan na watoto wanapokea msaada wa chakula katika kituo cha wakimbizi cha Koulbus nchini Chad, wakiungwa mkono na Shirika la Chakula Duniani (WFP).Wao wameketi chini ya miti, wakiwa na mifuko ya vyakula ikiwa ni pamoja na sorghum na vyakula maalum vyenye lishe kwa akina mama na watoto.
© WFP/Lena von Zabern Wanawake wakimbizi wa Sudan wanasubiri msaada katika kambi ya wakimbizi ya Koulbus nchini Chad.

Pengo la ufadhili latishia maisha ya wakimbizi wa Sudan nchini Chad

Msaada wa Kibinadamu

Wakati mgogoro nchini Sudan ukikaribia kutimiza miaka mitatu, zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Sudan walioko nchini Chad wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupunguzwa kwa mgao wa misaada muhimu ya kibinadamu. 

Onyo hilo limetolewa leo na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wakitanabaisha kuwa huduma za msingi kama chakula, maji, malazi, ulinzi na huduma za afya zitalazimika kupunguzwa zaidi katika miezi ijayo iwapo pengo la ufadhili la dola milioni 428 halitazibwa haraka.

Katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa leo mashirika hayo yameeleza kuwa, Chad ambayo inapakana na Sudan imepokea wakimbizi milioni 1.3, huku zaidi ya 900,000 wakiwasili tangu vita vilipoanza mwaka 2023. Tangu Januari 2026 pekee, wakimbizi wapatao 15,000 wameingia nchini humo licha ya rasilimali kuwa haba.

UNHCR

Hivi sasa, UNHCR ina uwezo wa kutoa msaada wa msingi kwa wakimbizi wanne tu kati ya kumi, hali inayowaacha wengi bila makazi, maji ya kutosha na huduma za afya. Takriban familia 80,000 hazina makazi, huku katika maeneo kama Oure Cassoni, wakimbizi wakipata chini ya nusu ya kiwango cha chini cha maji kinachohitajika kwa siku.

Aidha, zaidi ya watu 243,000 bado wamekwama katika maeneo ya mpakani mashariki kutokana na ukosefu wa fedha za kuwahamishia katika makazi salama zaidi. Wengi hulazimika kulala nje au kwenye vibanda duni vinavyowaweka hatarini kukumbwa na magonjwa, ukosefu wa usalama na hali mbaya ya hewa.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Chad, Patrice Ahouansou, amesema hali hiyo inaonesha gharama halisi ya upungufu wa ufadhili, akionya kuwa bila msaada wa haraka kutoka kwa wafadhili, mateso yataongezeka zaidi kwa familia zilizokimbia vita.

WFP

Kwa upande wake, WFP imesema imeathiriwa pia na uhaba wa fedha, ikiwa na chini ya nusu ya rasilimali zinazohitajika. Shirika hilo tayari limepunguza mgao wa chakula kwa zaidi ya nusu ya wakimbizi, huku wanawake na watoto wadogo wakiwa miongoni mwa wanaoathirika zaidi.

Mkurugenzi wa WFP nchini Chad, Sarah Gordon-Gibson, amesema bila ufadhili wa kutosha, shirika hilo haliwezi kutoa chakula cha kutosha kwa wanaohitaji zaidi, hali inayoweza kulazimisha familia kuchukua hatua hatari za kujinusuru.

Mashirika hayo mawili yamewataka wafadhili kuchangia fedha haraka ndani ya miezi sita ijayo ili kuendelea kutoa msaada muhimu, yakisisitiza kuwa ukarimu wa Chad kwa wakimbizi unapaswa kuungwa mkono na juhudi za kimataifa kabla hali haijazidi kuwa mbaya.