Guterres ahofia kuhatarishwa kwa sitisho la mapigano
Türk asema kiwango cha mauaji ya raia kinatisha
Kasi yaongezeka ya wanaokimbilia Syria-IOM
UN Women yaimarisha huduma za afya ya akili
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali mashambulizi makubwa ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya Lebanon tarehe 8 Aprili, mashambulizi ambayo ymesababisha mamia ya raia kuuawa na kujeruhiwa, wakiwemo watoto, sambamba na kuharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya kiraia.
Taarifa iliyotolewa New York, Marekani na Msemaji wa Umoja wa Mataifa inamnukuu Guterres akionesha wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la vifo miongoni mwa raia na kutoa pole kwa watu na Serikali ya Lebanon, akiwatakia nafuu ya haraka wale waliojeruhiwa.
Mashambulizi Lebanon yanatishia sitisho la mapigano - Guterres
Vyombo vya habari vinaripoti kuwa mashambulio hayo kutoka angani yalielekezwa kwenye viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut, maeneo ya kusini mwa Lebanon na jimbo la Bekaa na takribani watu 186 wameuawa.
Katibu Mkuu ameonya kuwa kuendelea kwa operesheni za kijeshi nchini Lebanon kunaweka hatarini makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yaliyotangazwa Aprili 7, pamoja na juhudi pana za kufikia amani, akisisitiza tena wito wake wa kusitishwa mara moja kwa mapigano.
“Sheria za kimataifa za kibinadamu lazima ziheshimiwe wakati wote, huku raia na miundombinu ya kiraia vikilindwa,” amenukuliwa Katibu Mkuu huku akisisitiza kwamba hakuna suluhisho la kijeshi kwa mzozo huo.
Naye Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amelaani mashambulizi hayo yaliyofanywa na Israeli nchini Lebanon, akielezea ripoti za mamia ya waliouawa na kujeruhiwa – wakiwemo raia – kuwa ni “za kutisha.”
Kwa mujibu wa mamlaka za Israel, takriban mashambulizi 100 yalifanywa ndani ya dakika chache, yakilenga vitongoji vya kusini mwa Beirut, kusini mwa Lebanon na Bonde la Bekaa.
Soundcloud
Timu za Umoja wa Mataifa zilizopo eneo la tukio ziliripoti hali ya uharibifu mkubwa, huku hospitali zikilemewa na idadi kubwa ya majeruhi.
Inaripotiwa pia kuwa mashambulizi yalilenga maeneo yaliyo karibu na vituo vya afya na huduma za dharura, jambo lililozua wasiwasi kuhusu ulinzi wa raia na huduma za afya.
Türk amesisitiza kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu lazima zizingatiwe wakati wote, akitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu madai ya ukiukwaji na kuwajibishwa kwa wale wanaohusika.
Idadi ya watu wanaovuka mpaka kuingia Syria kutokea nchini Lebanon imeongezeka kwa kasi tangu vita vilipoanza tarehe 28 Februari, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi, shirika hilo linasema hadi tarehe 6 Aprili, takribani watu 197,000 wameingia, wengi wao wakiwa raia wa Syria, huku idadi ndogo ya Walebanon pia wakivuka.
Wasyria wengi wanarejea katika hali zisizo na uhakika, bila mipango ya wazi iwapo watabaki au wataendelea kusonga mbele.
Waliowasili wapya wamesambaa katika majimbo yote 14 ya Syria, huku mahitaji muhimu yakijumuisha chakula, msaada wa fedha taslimu na makazi.
IOM inasema wengi wanategemea makazi ya muda au yasiyokidhi mahitaji, huku rasilimali zikiendelea kuwa chache kupita kiasi.
Upatikanaji bado ni mgumu, huku baadhi ya njia za kuvuka mpakani zikifungwa kwa kiasi au kuwekwa vizuizi, jambo linalozidisha ugumu wa usafiri na juhudi za misaada ya kibinadamu.
Wanawake na wasichana na mzigo mkubwa wa kutunza familia- UN Women
Tweet URL
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women inaripoti kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya anga ya Israel nchini Lebanon yamesababisha uharibifu mkubwa, huku nyumba zikigeuka vifusi na mamia ya raia kuripotiwa kuuawa au kujeruhiwa.
Taarifaya UN Women inasema familia zilikumbwa na mashambulio bila kutarajia, nyingi zikiwa na muda mchache au bila muda kabisa wa kukimbia, huku hospitali zikilemewa na watu kuendelea kuwatafuta wapendwa wao chini ya vifusi.
Wanawake na wasichana – ambao tayari wameathiriwa zaidi na mgogoro huu – wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi, ikiwa ni pamoja na kuhama makazi, kupoteza mali na wapendwa, pamoja na mzigo wa kutunza familia katika hali ngumu sana.
UN Women inasisitiza kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu ziko wazi: raia lazima walindwe wakati wote, na inatoa wito wa kupunguzwa kwa haraka kwa mvutano.
Makadirio yanaonesha kuwa takriban robo ya wanawake na wasichana wote nchini Lebanon wamekimbia makazi yao tangu mapema Machi, wengi wao wakiishi katika makazi yaliyojaa kupita kiasi au mazingira yasiyo rasmi huku wakiwatunza watoto na wazee.
Huduma za ushauri nasaha na afya ya akili
Kwa sasa UN Women inapanua huduma za afya ya akili na ulinzi zinazozingatia mahitaji ya kijinsia, ikiwa ni pamoja na maeneo salama ambapo wanawake wanaweza kupata ushauri nasaha, kupatiwa rufaa na msaada wa jamii.
Vituo hivi vinasaidia wanawake kukabiliana na madhara ya mshtuko wa kisaikolojia, kujenga tena hali ya utulivu na kuunganishwa na wengine wanaokabili changamoto zinazofanana.
Kadiri mahitaji yanavyozidi kuongezeka kwa kasi, wahudumu walio mstari wa mbele pia wanaongeza maeneo ya kutoa huduma.