Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Picha ya satelaiti kutoka kwa satelaiti ya Aqua ya NASA inayoonyesha Ghuba ya Uajemi ikiwa na vimbunga vya algae za rangi ya tan, bluu, na kijani kibichi zikichanua kando ya pwani za Iran na Peninsula ya Arabia.

Sitisho la mapigano Iran laibua matumaini ya kufunguliwa mlango wa baharí wa Hormuz

© NASA/Jeff Schmaltz Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz.(Kulia kabisa)

Sitisho la mapigano Iran laibua matumaini ya kufunguliwa mlango wa baharí wa Hormuz

Na Daniel Dickinson
Amani na Usalama

Tangazo la Marekani na Iran la sitisho la mapigano kwa wiki mbili, yatarajiwa kuwa litawezesha kufunguliwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz, njia muhimu ambamo kwayo moja ya tano ya nishati ya mafuta na gesi duniani hupitia kwa kutumia meli.

Mlango huu umegeuka kuwa hatari na umechochea ongezeko la bei ya mafuta, na kutishia pia usalama wa meli na mabaharia huku ukihatarisha usalama wa kikanda.

Kwa nini ni muhimu?

Mlango wa bahari wa Hormuz ni ushoroba mwembamba wa baharini kati ya Iran na Oman ambao unaunganisha Ghuba ya Uajemi na Ghuba ya Oman ambayo kwayo nchi kadhaa zikiwemo Saudi Arabia, Iran na Umoja wa Falme za Kiarabu huitumia kusafirishia nje ya nchi mafuta na gesi.

Hata usumbufu mdogo tu unaweza:

Kuongeza bei za nishati ya mafuta

Kuchelewesha mnyororo wa usambazaji bidhaa duniani

Kuongeza mvutano wa kijiografia na kisiasa

Sasa ni nini kinfanyika kwenye usafirishaji kwa meli hivi sasa?

Usafirishaji kwa njia ya meli kupitia mlango huo wenye urefu wa kilometa 39 (sawa na maili 21 za baharini) katika eneo jembamba zaidi – umevurugika kwa kiasi kikubwa tangu kuanza kwa vita tarehe 28 mwezi Februari 2026.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la usafirishaji baharini, (IMO) kabla ya mzozo, takribani vyombo vya majini 150 vilipita kwenye mlango huo kila siku.

Kufuatia tishio la mashambulizi baada ya mapigano kuanza, idadi hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa na kuwa meli nne au tano kwa siku, na zinazoruhusiwa ni zile ambazo mamlaka za Iran zinaona kuwa hazina uhasama au si hatarishi.

Hadi sasa haifahamiki kama au lini mlango huo utafunguliwa tena kwa mel izote, licha ya tangazo la sitisho la mapigano.

Kiwango cha hatari dhidi ya meli?

IMO imekadiria kwamba kuna takribani meli 2,000 zikiwemo meli za mafuta na gesi, meli za kubeba mizigo mikubwa, meli za mizigo—pamoja na meli sita za watalii —zilizokwama katika Ghuba ya Uajemi, zikiwa haziwezi kupita kwenye mlango huo.

Inakadiriwa kuwa takribani mabaharia 20,000 kwa sasa wako ndani ya vyombo hivyo.

Kumekuwa na mashambulizi 21 yaliyothibitishwa dhidi ya usafirishaji wa kimataifa katika eneo hilo, yakisababisha vifo vya mabaharia 10 na wengine kadhaa wamejeruhiwa, kulingana na IMO.

baharia wawili katika jumpsuits bluu na kofia nyeupe ngumu juu ya bodi ya meli, karibu railing na bahari katika background.
© IMO Mabaharia wawili wakiwa kwenye kazi zao melini. (Maktaba)

“Makubaliano ya kusitisha mapigano ni habari njema kwa mabaharia 20,000 wanaosubiri kuhamishwa kutoka kwenye meli ambazo bado ziko katika Ghuba ya Uajemi,” amesema Damien Chevallier, Mkurugenzi wa Kitengo cha Usalama wa Baharini cha IMO, akiongeza kuwa “wamekaa zaidi ya mwezi mmoja katika hali ya wasiwasi na hatari, wakiwa hawawezi kuondoka kwenye meli zao.”

Uhamishaji mabaharia kwa usalama

IMO tayari inafanya kazi na wahusika kutekeleza “utaratibu unaofaa wa kuhakikisha upitishaji salama wa meli kupitia mlango wa bahari wa Hormuz,” amesema Chevallier.

“Kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha usalama wa kupita ili kuwezesha uhamishaji. Hatutaki kuona hali ikirudi kuwa ya mvutano mkali. Kwa hiyo, kwa sasa, tunahitaji kuzingatia uhamishaji,” ameongeza.

Sheria ya kimataifa inasemaje?

Mfumo wa kisheria wa shughuli zote za baharini umeainishwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa sheria ya bahari au UNCLOS.

Kanuni kuu

 

  • Meli zina haki ya “kusafiri kupiti” milango ya Bahari ya kimataifa
  • Nchi za pwani hazipaswi kuzuia au kuvuruga safari za meli

 

Kwa lugha rahisi, mlango huo  lazima ubaki wazi kwa usafirishaji wa kimataifa.

Hata hivyo, kuna tahadhari moja muhimu. Iran si mwanachama wa UNCLOS, lakini mfumo wa kupita kwa usafiri kwa ujumla unachukuliwa kuwa sehemu ya sheria ya kimataifa ya kijadi.

Je, usafirishaji utaanza tena—na vipi?

Kuna nia ya kimataifa ya kufungua tena mlango huo lakini “waendeshaji wa meli watahitaji kutathmini kwa makini hali ya hatari,” amesema Damien Chevallier wa IMO, akiongeza kuwa “kuanza tena kwa biashara ya kawaida kutategemea hali ya usalama wa baharini.”

Ramani inayoonyesha Mpango wa Kutenganisha Trafiki katika Mlango-Bahari wa Hormuz, inayoelezea kwa undani njia za usafirishaji, maeneo ya trafiki, na maeneo muhimu ya kijiografia kama Kisiwa cha Qeshm na Peninsula ya Musandam.
© IMO Mfumo wa kutenganisha safari za meli katika mlango wa bahari wa Hormuz.

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa na washirika wake wanaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia ili kupata njia salama, yenye ulinzi na yenye ufanisi kwa meli kupita katika mlango huo wa bahari.

Inatarajiwa kuwa usafirishaji utaanza tena kupitia njia zilizodumu kwa muda mrefu, ambapo mfumo muhimu ni Mpango wa Kutenganisha Mzunguko wa Meli au TSS.

Je mpango wa TSS unahusisha nini?

Mpango huo ulipendekezwa na Iran na Oman na kupitishwa na IMO mwaka 1968, mfumo huo huainisha njia za meli ili:

  • Kupunguza migongano
  • Kuboresha usalama
  • Kudumisha upitishaji unaotabirika hata wakati wa mvutano wa kimataifa

Meli chache ambazo zimefanikiwa kupita kuelekea Ghuba ya Oman katika mwezi uliopita zimechukua njia ya kaskazini karibu na Iran, ikiripotiwa kuwa ni ili mamlaka huko ziweze kufuatilia mienendo yao kwa karibu zaidi.

Nini kinafuata?

Kufanikiwa kufunguliwa tena kwa mlango wa bahari wa Hormuz hatimaye kutategemea kudumu kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, mafanikio ya diplomasia, uratibu wa baharini, na kuheshimiwa kikamilifu kwa kanuni za njia za usafiri wa meli zilizokubaliwa kimataifa.