UN yazindua Mfuko wa Urejeshaji Palestina ukilenga kuharakisha ujenzi upya na matumaini
UN yazindua Mfuko wa Urejeshaji Palestina ukilenga kuharakisha ujenzi upya na matumaini
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezindua Mfuko wa Urejeshaji wa Palestina uliopewa jina la Horizon Fund, na akisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kusaidia wananchi wa Palestina kurejesha maisha yao na kujenga mustakabali bora.
Akizungumza kupitia ujumbe wa video wakati wa uzinduzi uliofanyika Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel, Guterres amesema mfuko huo ni sehemu muhimu ya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Taifa la Palestina.
Amesema “wananchi wa Palestina wanaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, pamoja na Ukanda wa Gaza, hali inayohitaji zaidi ya misaada ya kibinadamu pekee.”
Mkuu huyo wa UN amesema “Ingawa misaada ya kibinadamu ni muhimu, lakini haitoshi. Watu wanahitaji fursa ya kujenga upya maisha yao, kurejesha vyanzo vya kipato na kuamua mustakabali wao kwa heshima.”
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, Horizon Fund utaleta pamoja wadau mbalimbali chini ya jukwaa la pamoja la Umoja wa Mataifa ili kuharakisha urejeshaji wa awali, kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi, na kuimarisha taasisi za Palestina, kwa kuzingatia dira ya suluhisho la mataifa mawili.
Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa utafanya kazi kwa karibu na Mamlaka ya Palestina kuhakikisha mfuko huo unaendana na vipaumbele vya kitaifa na unaleta matokeo endelevu.
Guterres amesisitiza kuwa huu ni wakati muhimu kwa hatua za urejeshaji, akionya kuwa haziwezi kusubiri, huku akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuunga mkono mfuko huo kama uwekezaji katika uthabiti, ustahimilivu na amani ya kudumu.
Amehitimisha ujumbe wake kwa njia ya video kwa kauli mbiu: “Umoja wa Mataifa mmoja, Palestina moja, na mustakabali mmoja.”