Umoja wa Mataifa wakaribisha tangazo la Marekani na Iran la kusitisha mapigano
Umoja wa Mataifa wakaribisha tangazo la Marekani na Iran la kusitisha mapigano
- Pande husika zizingatie vipengele vya makubaliano
- Türk asema amani ya kuhudumu izingatie haki za binadamu za kila mtu
- UNOPS yasema uharibifu wa miundombinu utapumzika
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha tangazao la Marekani na Iran la kusitisha mapigano kwa wiki mbili, wakati huu ambapo vita hiyo iliyoanzishwa na Marekani na Israeli dhidi ya taifa hilo la Ghuba ya Uajemi ikiingia siku ya 40.
Taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo na Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric jijini New York, Marekan inamnukuu Guterres akitoa wito kwa pande zote kwenye mzozo huo wa sasa Mashariki ya Kati kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa.
Zingatieni vipengele vya makubaliano
Halikadhalika wazingatie vipengele vya sitisho hilo la mapigano, ili hatimaye kufungua njia ya kuwa na amani ya kudumu na ya kina kwenye ukanda huo.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa kumalizika kwa uhasama ni jambo linalohitajika kwa dharura ili kulinda rai ana kuondoa machungu wanayokabiliana nayo binadamu.
Guterres ameelezea shukrani zake kwa Pakistani na mataiga mengine yaliyoshiriki katika kufanikisha makubaliano hayo ya sitisho la mapigano.
Kauli za viongozi wengine wa UN
Viongozi wengine waandamizi wa Umoja wa Mataifa waliounga mkono tangazo la sitisho la mapigano ni pamoja na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu Volker Türk ambaye kupitia mtandao wa X zamani Twitter amesema “ni matumaini ya dhati kwamba tangazo la kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran litaleta nafuu kwa raia wote ambao wamekuwa wakiteseka kwa wiki kadhaa sasa na bado wako katika hatari kubwa.”
Amani ya kudumu inayoheshimu haki ya kila mtu
Amehimiza pande zote kutenda kwa nia njema na kuhakikisha kwamba hatua hii ya kwanza inatafsiriwa kuwa makubaliano ya kina. “Ni muhimu pia kumaliza maumivu na mateso yaliyosababishwa na vita nchini Lebanon,” amesema Kamishna Mkuu Türk, akiongeza kuwa, “amani ya kudumu ya kikanda, inayolinda haki za binadamu na kuheshimu sheria za kimataifa, ni ya lazima.”
Ahueni itapatikana na miundombinu itapona
Naye Jorge Moreira da Silva, Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na huduma za miradi, (UNOPS) amesema “ninakaribisha tangazo la kusitisha mapigano la wiki mbili kati ya Marekani na Iran. Hili litaleta pumziko linalohitajika sana kwa watu — wiki sita zilizopita zimeleta maangamizi na huzuni, huku maelfu wakiuawa na kujeruhiwa.”
Amemulika pia uharibifu uliosababishwa na vita hivyo akisema “miundombinu ya kiraia ikiwemo madaraja, barabara, shule na vituo vya afya imeharibiwa. Athari zake zimeenea kwa upana, kwani mamilioni ya watu nje ya eneo hilo wamekumbwa na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu na changamoto za upatikanaji wa chakula, mafuta na dawa.”
Tayari Mjumbe Binafsi wa Katibu Mkuu kwenye mzozo huo Jean Arnault yuko kwenye eneo hilo kuunga mkono juhudi za kuleta amani.
Lebanon
Pamoja na habari hizo njema, kwa nchi jirani ya Lebanon hali ni tofauti. Mashambulizi ya anga ya Israeli kusini mwa Lebanon yameendelea kuripotiwa huku Israeli ikisema tangazo la sitisho la mapigano lililotolewa jana usiku halikujumuisha Lebanon, licha ya mpatanishi mkuu ambaye ni Pakistan kusisitiza kwamba lilijumuisha.
Katika mahojiano ya Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP nchini Lebanon Blerta Aliko aliyeko Beirut lakini mahojiano hayo yalibidi kukatwa kwani kulikuwa na mashambulizi ya mabomu, na baadaye Idhaa ilifanikiwa kumpata tena hewani ameeleleza kuwa yuko salama amejificha chini lakini mashambulizi ni ya hali ya juu akiongeza kuwa..
“Sote tuko salama na wafanyakazi wenzangu wote wanahesabiwa. Tumejificha kwenye chumba kilicho chini ya ardhi ndani ya Ofisi za Umoja wa Mataifa hapa Beirut…. Hali ni mbaya sana kwani tangu tulipozungumza mara ya mwisho, kulikuwa na mashambulizi tisa ambayo nilikuwa nikiyasikia, na kisha zaidi ya 40 huko Beirut na kuna mamia ya mashambulizi nchini kote. Na hadi sasa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu amethibitisha kwamba kuna zaidi ya watu 300 wamepoteza maisha. Kwa hivyo hatuna habari njema. Inaonekana kama migomo utaendelea mchana na usiku. Kwa hivyo hebu tuone wazimu huu, unatupeleka wapi leo.”
Na mapema hii leo Mkurugenzi wa Kanda ya Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO wa Mashariki mwa Mediterania Hanan Balkhy ameonya kwamba mfumo wa afya wa Lebanon una hali tete wakati huu ambapo watu wengi wanakimbia mapigano sasa na kwa hali hii tuliyoelezwa na UNDP ni Dhahiri hali inazidi kuwa tete.
Dkt. Balkhy amesisitiza kwamba sitisho la mapigano linahitajika haraka nchini Lebanon, akionya kwamba vurugu zinazoendelea na watu kuyahama makazi yao kuna hatari ya mifumo ya afya kuzidiwa nguvu kwani tayari mifumo hiyo ni dhaifu.