UNICEF na Benki ya Dunia warejesha matumaini ya elimu kwa watoto Sudan kupitia programu mbadala za kujifunza
UNICEF na Benki ya Dunia warejesha matumaini ya elimu kwa watoto Sudan kupitia programu mbadala za kujifunza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF kwa kushirikiana na Benki ya Dunia linaendelea kurejesha matumaini ya elimu kwa maelfu ya watoto katika Jimbo la Mto Nile nchini Sudan kupitia Programu za Elimu Mbadala (ALP), baada ya miaka mingi ya vurugu na kusitishwa kwa masomo kuathiri mustakabali wao. Feissal Kirwa anaangazia zaidi.
Katika jimbo la River Nile nchini Sudan video ya UNICEF na Benki ya Dunia inaanza kwa kumuonesha mwanafunzi Hayat akiwa ndani ya darasa lililo kuukuu yeye na wanafunzi wenzake.
Mwalimu anaendelea kufundisha na wote wanafurahi kuendelea na masomo yao. Wao ni miongoni mwa wanafunzi 9,500 wanaonufaka na Programu hizo za Elimu Mbadala kwani wamepata fursa ya kurejea katika masomo na kujenga upya ndoto zao.
Programu zinalenga kuwasaidia watoto waliokatiza masomo kurejea katika mfumo wa elimu kwa kuwapatia mtaala wa haraka unaowawezesha kufikia kiwango cha kujiunga tena na shule rasmi.
“Baada ya vita kuanza, sikudhani nitapata tena nafasi ya kusoma. Lakini sasa niko kwenye programu ya elimu mbadala na ninaendelea vizuri.”
Masomo yakiendelea mwalimu anawauliza maswali huku kila mmoja akitaka kujibu. Kurejea shuleni hakika kumeleta furaha na matumaini mapya. Shaza, mwenye umri wa miaka 13, anaeleza:
“Ninahisi furaha kuwa shuleni tena kwa sababu inanirejeshea kumbukumbu za nilivyokuwa ninasoma nyumbani kabla ya vurugu.”
Naye Mulhim, pia mwenye umri wa miaka 13, anazungumzia stadi alizopata akisema, …sasa ninajua kusoma na kuandika, na ninawapenda walimu wangu. Hapa ninajisikia salama, hakuna tena vita wala hofu.”
Um Al Hassan, mmoja wa walimu, anaeleza jinsi programu hiyo imeleta mabadiliko makubwa kwa watoto waliokuwa wamekatishwa masomo kwa muda mrefu:
“Baadhi ya watoto waliokuja kutoka maeneo ya magharibi hawakuwa na elimu kabisa. Lakini sasa wanaweza kuandika majina yao, kusoma na kuelewa masomo ya msingi.”
Kupitia programu hizi, watoto wamefundishwa masomo muhimu kama Kiarabu, Hisabati, Elimu ya Dini na Kiingereza kwa mtindo wa kasi ili kuwawezesha kujiunga tena na shule rasmi.
Watoto hao pia wanaendelea kuwa na ndoto kubwa za maisha yao ya baadaye. Hayat anasema..nataka kuwa daktari nitibu wagonjwa! Shaza anasema..nataka kuwa mhandisi ili nijenge upya nyumba yetu. Na kwa Mulhim …nikikua nataka kuwa daktari ili nisaidie wengine.