Mauaji ya Kimbari: Kamwe tena itasalia maneno matupu iwapo hakuna vitendo – Balozi Ngoga
Mauaji ya Kimbari: Kamwe tena itasalia maneno matupu iwapo hakuna vitendo – Balozi Ngoga
Wakati leo ni kumbukizi ya miaka 32 tangu mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi ya mwaka 1994, nchini Rwanda, Martin Ngoga, Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, amemulika juhudi za nchi hiyo za kujijenga upya huku akizihimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuacha maneno matupu na kuchukua hatua madhubuti kuzuia maafa kama hayo siku zijazo.
Katika mahojiano na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Balozi Ngoga ameelezea mabadiliko makubwa ya Rwanda katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, akisisitiza uongozi wa kisiasa, maridhiano, ushiriki wa vijana, na umoja wa kitaifa kama nguzo kuu za kujenga upya jamii iliyowahi kuharibiwa na mauaji ya kimbari.
“Nguzo muhimu ya mafanikio ya Rwanda imekuwa uwekezaji kwa vizazi vijana. Kwa kuwa idadi kubwa ya wananchi walizaliwa baada ya mwaka 1994, nchi imeweka kipaumbele katika elimu na kumbukumbu ili kuhakikisha kuwa historia ya mauaji ya kimbari haisahauliki wala kujirudia. Juhudi hizi zinalenga kuondoa mgawanyiko wa kikabila na kuimarisha utambulisho wa kitaifa unaoshirikisha wote,” amesema Balozi Ngoga.
Ukanushaji wa mauaji ya kimbari yaliyotokea
Kuhusu tabia za watu kukanusha uwepo wa mauaji ya kimbari, Balozi Ngoga amesema, “kukanusha ni hatua moja wapo ya maandalizi ya kufanya mauaji mengine. Watu ambao wametafiti mauaji ya kimbari wanasema kwamba hatua ya mwisho ya maandalizi huwa ni kuandaa utaratibu wa kukanusha yakishafanyika.”
Mkataba upo lakini hata walioridhia wanausigina
Akizungumzia maendeleo ya Rwanda, Ngoga pia ametoa ujumbe mkali kwa jumuiya ya kimataifa. Akisisitiza kuwa kuzuia mauaji ya kimbari kunahitaji zaidi ya ahadi za kisheria kama Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari. “Licha ya nchi nyingi kuridhia mkataba huo, ukosefu wa dhamira ya kisiasa bado unadhoofisha utekelezaji na ushirikiano wa kimataifa, hasa katika kuwafikisha mbele ya sheria washukiwa waliokimbilia nchi nyingine.”
Wakati wa kujitathmini
Balozi Ngoga ameonesha wasiwasi wake juu ya baadhi ya mambo yanayoendelea sasa ikiwem kauli za chuki akisema ni viashiria vya machafuko. “Labda ni wakati wa kujitafakari upya sisi kama jumuiya ya kimataifa. Na hapa tulipo Umoja wa Mataifa tujiangalie upya tujisahihishe kwa sababu tulikosea huko nyuma na tunaendelea kukosea. Na Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mauaji ya kimbari uliwekwa baada ya Vita Kuu ya Dunia, na hii siku ambayo tunaadhimisha Aprili 7 iliwekwa baada ya mauaji yaliyotokea Rwanda. Sasa ni mara ngapi tunakosea na ni mara ngapi tutaendelea. Wakati umefika sasa tujitathimini.”
Hatua kwa vitendo
Ngoga amehizima nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za vitendo kufuatia kumbukizi hiyo ya kila mwaka, akionya dhidi ya kuifanya kauli mbiu ya “Kamwe Tena” kuwa maneno ya ishara tu.
Balozi Ngonga ametoa wito wa kuimarishwa kwa utekelezaji wa sheria za kimataifa, uwajibikaji zaidi, na hatua za haraka pale dalili za hatari zinapoonekana.
“Kamwe Tena lazima liambatane na dhamira thabiti zaidi,” amesema Balozi Ngoga, akiitaka jumuiya ya kimataifa kuendana kati ya maneno na vitendo endelevu.