Mambo 6 yenye ukweli mchungu kuhusu afya ya mwanamke
Mambo 6 yenye ukweli mchungu kuhusu afya ya mwanamke
Wanawake wanaishi miaka mingi zaidi kuliko nyakati zilizopita, lakini hawaishi maisha bora. Ikiwa kuna mtu anasema "tayari tumefikia usawa wa kijinsia," au anauliza "hivi huu usawa tayari umevuka kiwango?", Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women linashauri mwelekeze mtu huyo kwenye sekta ya afya, haki ya msingi ya binadamu ambayo bado haijatengenezwa kwa ajili ya kila mtu.
Kwa mujibu wa ufafanuzi wa UN Women uliochapishwa katika wavuti wake Aprili 6, 2026, shirika hilo limeeleza kuwa kote ulimwenguni, wanawake wanashuhudia kwa kiasi kikubwa maumivu yao yakipuuzwa, dalili zao zikitafsiriwa vibaya, na hali zao za kiafya kugunduliwa zikiwa zimechelewa sana. Haya ni matokeo ya mfumo wa matibabu ambao haukubuniwa kwa kumfikiria mwanamke. Kuanzia vifaa vinavyotumika katika vipimo hadi takwimu zinazotoa mwelekeo wa utambuzi na matibabu, kasoro hizi zimejengwa ndani ya mifumo ya afya na zinahatarisha usalama na ubora wa maisha ya wanawake.
Hivi ndivyo ukosefu wa usawa wa kijinsia unavyoonekana katika maisha yetu ya kila siku, na ni lazima vibadilike: tunahitaji utafiti unaoakisi miili ya wanawake, huduma za afya zinazochukulia maumivu ya mwanamke kwa uzito, na mifumo inayozingatia utu, utambuzi sahihi, na heshima kwa miili ya wanawake na wasichana.
1. Kipimo chako cha uzazi hakijabadilika kwa miaka 150
Kifaa kinachoitwa speculum kinachotumiwa katika vipimo vya nyonga (pelvic exams) kinaonekana karibu sawa kabisa na kilivyobuniwa kwa mara ya kwanza katika karne ya 19. Hii ilikuwa kabla ya ugunduzi wa dawa za vijiuvijasumu (antibiotic). Kabla ya dawa za ganzi kuwa kitu cha kawaida. Kabla hata wanawake hawajapata haki ya kupiga kura katika nchi nyingi duniani.
Kwa vizazi vingi, wanawake wamekuwa wakiambiwa kuwa maumivu au hali ya kutojihisi vizuri wakati wa vipimo hivi ni jambo la kawaida, ni sehemu tu ya kuwa mwanamke. Ingawa sasa mambo yanaanza kubadilika kupitia kampuni zinazoongozwa na wanawake na wabunifu wa teknolojia ya afya ya wanawake wanaofikiria upya kipimo hiki kwa kuzingatia kuondoa maumivu na utu, mabadiliko ni ya kusuasua. Utumiaji wa vifaa hivi vipya vilivyoboreshwa bado ni mdogo sana katika mifumo ya afya ya umma.
2. Wanawake wanaishi maisha marefu lakini wanatumia muda mwingi katika hali duni ya afya
Takwimu zinaonesha kuwa wanawake wanaishi muda mrefu kuliko wanaume, wastani wa miaka 73.8 ikilinganishwa na miaka 68.4 kwa wanaume. Hata hivyo, wanawake wanatumia asilimia 25 zaidi ya maisha yao wakiwa katika hali duni ya afya. Hii ina maana kwamba wanawake wanatumia miaka mingi wakikabiliana na maumivu sugu, uchovu, magonjwa yasiyotibiwa, na utambuzi usio sahihi.
Mara nyingi wanawake huambiwa kuwa dalili zao zinatokana na matatizo ya kisaikolojia. Maisha marefu hayamaanishi maisha bora. Kwa wanawake wengi, inamaanisha kutumia muda mrefu wakipuuzwa, kutoaminiwa, na kutelekezwa, hata na mifumo ya matibabu inayopaswa kuwalinda.
3. Ikiwa inawaathiri wanawake, inapuuzwa; Ikiwa inawaathiri wanaume, inapewa ufadhili
Matatizo ya kabla ya hedhi, yanayojulikana kwa lugha ya kiingereza Premenstrual Syndrome, yanawaathiri idadi kubwa ya wanawake na wasichana. Kwa wengi, hii inamaanisha maumivu ya mara kwa mara, uchovu, na msongo wa kisaikolojia unaovuruga maisha ya kila siku kwa siku kadhaa kila mwezi. Kwa upande mwingine, tatizo la upungufu wa nguvu za kiume linawaathiri wanaume wachache zaidi, lakini hali hii inapewa umakini mkubwa wa utafiti na fedha nyingi zaidi.
Kwa miongo kadhaa, usawa huu mbovu umejenga hali ambayo maumivu ya wanawake yanaeleweka vibaya na kuhalalishwa kama jambo la kawaida. Hata hivyo, mambo yanaanza kubadilika kidogo. Mwaka 2023, Hispania ilikuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuweka likizo ya hedhi yenye malipo, ikijiunga na nchi ya Japani, Indonesia, Korea Kusini, Taiwan, na Zambia. Sheria hii inatambua kuwa maumivu ya hedhi yanaweza kuwa makali na yanastahili msaada wa matibabu na muda wa kupumzika. Lakini sheria kwenye makaratasi hazibadili maisha ya kila siku mara moja; tangu sheria hiyo ianzishwe, matumizi yake yamebaki kuwa madogo kutokana na aibu na unyanyapaa unaozuia wanawake kuchukua likizo hiyo wanayostahili.
4. Inaweza kuchukua takribani muongo mmoja kugundua chanzo cha maumivu yako
Ugonjwa wa Endometriosis unaathiri mwanamke 1 kati ya 10 duniani kote, takriban wanawake milioni 190. Hata hivyo, utambuzi na matibabu huchukua kati ya miaka 4 hadi 12 kwa wastani. Hiyo ni miaka mingi ya kuishi na maumivu makali sugu na uchovu huku ukiambiwa kuwa "hakuna tatizo" na kwamba "maumivu hayo ni ya kawaida."
Matatizo kama endometriosis sio magonjwa adimu; tatizo ni kwamba maumivu ya wanawake bado yanapuuzwa au kucheleweshwa kufanyiwa utambuzi. Wakati maumivu hayachukuliwi kwa uzito, utambuzi unakuja ukiwa umechelewa sana, jambo linalovuruga mipango ya maisha ya mwanamke.
5. Wanawake walikosekana katika tafiti za matibabu hadi miaka ya 1990
Hadi kufikia mwaka 1993, wanawake walikuwa wakitengwa kwa kiasi kikubwa katika majaribio ya kitabibu ya dawa na matibabu. Hii ina maana kwamba kwa miongo mingi, dozi za dawa na matibabu zilitengenezwa kwa kuzingatia miili ya wanaume pekee na hazijawahi kufanyiwa majaribio sahihi kwa wanawake. Matokeo yake ni:
· Dozi za dawa zilitegemea biolojia ya mwanaume.
· Dalili za magonjwa zilifafanuliwa kupitia miili ya wanaume.
· Madhara ya dawa kwa wanawake mara nyingi yalipuuzwa.
Leo hii, wanawake wana uwezekano mkubwa wa kupata madhara baada ya kutumia dawa. Hata zana za kisasa za Akili Mnemba ama AI, zinazotumika hospitalini zinaendelea kutumia takwimu ambazo haziwakilishi wanawake vizuri. Vilevile, wanawake hawapo kwa wingi katika nafasi za uongozi kwenye sekta ya afya. Uchunguzi unaonesha kuwa madaktari na viongozi wanawake mara nyingi hupata matokeo bora zaidi kwa wagonjwa wao, kwani wanazingatia zaidi mahitaji ya mgonjwa na sera jumuishi zinazookoa maisha.
6. Dalili zako hazifanani na za kwenye vitabu, na hiyo inaweza kukugharimu maisha
Ugonjwa wa moyo ni kisababishi kikuu cha vifo kwa wanawake. Lakini dalili "rasmi" kama vile maumivu ya kifua yanayosambaa kwenye mkono, zinategemea zaidi jinsi shambulio la moyo linavyotokea kwa wanaume. Kwa wanawake, dalili zinaweza kuwa tofauti: uchovu, kichefuchefu, upumuaji wa tabu, au maumivu kwenye taya au mgongo.
Kwa sababu dalili hizi hazitambuliki haraka, wanawake wana uwezekano mdogo wa kupata matibabu ya dharura ya kuokoa maisha kama vile upasuaji wa kuzibua mishipa (angioplasty).
Matokeo yake, wanawake wana hatari kubwa zaidi ya kufa baada ya kupata shambulio la moyo ikilinganishwa na wanaume, na katika hali nyingine, wanarudishwa nyumbani badala ya kutibiwa kwa sababu dalili zao "hazieleweki."
Suluhisho la hali hii ni kwamba, lazima mifumo ya afya ifanyiwe marekebisho makubwa ili kuondoa upendeleo wa kijinsia. Kuwekeza katika uongozi wa wanawake kwenye sekta ya afya na kufanya tafiti zinazojumuisha miili ya wanawake siyo tu jambo la usawa, bali ni jambo linalookoa maisha ya mamilioni ya watu duniani kote.