Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kukumbuka pekee mauaji ya Rwanda 1994 haitoshi, tuchukue hatua – Guterres

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na washiriki waliwasha mishumaa katika Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kukumbuka miaka 32 ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.
Picha ya UN/Loey Felipe Maafisa wa Umoja wa Mataifa na washiriki wengine wa Umoja wa Mataifa waliwasha mishumaa katika tukio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kukumbuka miaka 32 ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Kukumbuka pekee mauaji ya Rwanda 1994 haitoshi, tuchukue hatua – Guterres

Amani na Usalama

Leo ni miaka 32 tangu mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994 ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anatoa wito wa dhati wa kukumbuka, kuwajibika, na kuimarisha upya dhamira ya kimataifa ya kuzuia ukatili mkubwa dhidi ya binadamu.

Katika ujumbewake wa kumbukizi hiyo Guterres ametafakari tukio hilo alilolielezea kama “moja ya zama za kiza zaidi katika historia ya binadamu,” ambapo zaidi ya watu milioni moja waliuawa ndani ya siku 100 tu.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa idadi kubwa ya manusura walikuwa Watutsi, pamoja na Wahutu na wengine waliopinga mauaji hayo, akibainisha kuwa “familia nzima zilitokomezwa kwa ukatili mkubwa.”

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na washiriki wa Umoja wa Mataifa wamesimama hadharani kwenye Kwibuka Flame of Hope kwa ajili ya sherehe ya kuweka ua wa mauaji ya kuadhimisha maadhimisho ya miaka 32 ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, na mandhari ya jiji nyuma.
Picha ya UN/Manuel Elías Maafisa wa Umoja wa Mataifa na washiriki wengine wanahudhuria ua wa kifahari uliowekwa kwenye Mwenge wa Tumaini wa Kwibuka kuadhimisha miaka 32 ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuheshimu kumbukumbu za waliopoteza maisha huku wakitambua uimara wa manusura. “Tunaomboleza waathiriwa na kuheshimu utu wao ulioporwa,” amesema Guterres. “Tunawatunuku manusura, ambao uthabiti wao unaonesha nguvu ya roho ya mwanadamu.”

Aibu kwa jumuiya ya kimataifa

Wakati huohuo, amekiri kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti wakati huo, akisisitiza kuwa dunia lazima ikumbuke historia hii “kwa unyenyekevu na aibu.”

Guterres amesisitiza kuwa kukumbuka pekee hakutoshi huku akizihimiza nchi kuchukua hatua za vitendo ili kuzuia ukatili wa siku zijazo kwa kukabiliana na kauli za chuki, kukataa uchochezi wa vurugu, na kuwekeza katika jamii zilizo imara na zenye mshikamano.

“Haitoshi kukumbuka waliokufa. Lazima tujifunze kutokana na kushindwa kuwalinda walio hai,” amesema.

Wahudhuriaji wakiwa wameketi kwenye ibada ya ukumbusho wakiwa na mishumaa na maua meupe mezani.
Picha ya UN/Loey Felipe Washiriki wanawasha mishumaa katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wa kuadhimisha miaka 32 ya mauaji ya kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Nini kifanyike?

Sehemu muhimu ya juhudi hizo, amebainisha, ni kuimarisha mifumo ya kisheria ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na nchi zote kuridhia na kutekeleza Mkataba wa Kimataifa kuhusu Kuzuia na Kuadhibiti Uhalifu dhidi ya Mauaji ya Kimbari.

Akithibitisha mshikamano na Rwanda, Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kujitolea kuunga mkono juhudi za kukuza umoja, uthabiti na amani—nchini Rwanda na kote duniani.

“Umoja wa Mataifa unasimama pamoja na watu wa Rwanda,” amesema. “Na tunashikamana na wote, kila mahali, wanaokataa kusalimisha mustakabali wetu kwa hofu, mgawanyiko au ukimya.”

Ametamatisha akisema, “na siku hii ithibitishe upya dhamira yetu ya kukumbuka, kusikiliza na kuchukua hatua. “Tukiwa na historia kama mwongozo wetu, na kuzuia mauaji ya kimbari kama lengo letu.”

Ukuta wa Majina ya wahasiriwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda katika Kituo cha Makumbusho cha Kigali nchini Rwanda.
UN Ukuta wa Majina ya wahasiriwa wa Mauaji ya Kimbari ya Rwanda katika Kituo cha Makumbusho cha Kigali nchini Rwanda.

Kumbukizi Umoja wa Mataifa

Katika kukumbuka siku hii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na tukio maalum, kwa kuanzia kuweka shada la maua kwenye mnara wa kumbukumbu ulioko katika bustani za Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Kisha kwenye  ukumbi wa Baraza Kuu kutakuwa na tukio maalum, hotuba kutoka kwa viongozi wa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia yanayowakilisha manusura pamoja na shuhuda za manusura na hatua wanazochukua kusaidia waathiriwa pamoja na kuepusha mauaji ya aina hiyo yasitokee tena.

Tukio hilo litarushwa moja kwa moja na televisheni  ya mtandaoni ya Umoja wa Mataifa.