WHO yaboresha miongozo ya matibabu ya uraibu wa dawa za kupunguza maumivu
WHO yaboresha miongozo ya matibabu ya uraibu wa dawa za kupunguza maumivu
- Dawa hizo ni pamoja na morphine, fentanyl na tramadol
- Hutumika kupunguza maumivu lakini wengine hugeuza za kulevya
- Matumizi kupindukia husababisha vifo na magonjwa
- Mapendekezo ni pamoja na kila aliyeathirika vibaya apatiwe matibabu stahiki
Baada ya kubaini kuwa uraibu wa dawa za kupunguza maumivu ni moja ya sababu za magonjwa na vifo ulimwenguni, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, limechukua hatua mpya ambayo ni kutangaza maboresho ya mapendekezo kadhaa katika miongozo ijayo ya matibabu ya utegemezi wa dawa hizo kwa lugha ya kiingereza Opioid sambamba na usimamizi kwa wale walioongeza dozi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika wavuti wa WHO, Aprili 2, 2026 inakadiriwa kuwa watu milioni 316 duniani kote walitumia dawa za kulevya mwaka 2023, ikiwa ni pamoja na takribani watu milioni 61 waliojihusisha na matumizi ya dawa za kupunguza maumivu lakini si kwa lengo la matibabu.
Hivi sasa dawa hizo za kupunguza maumivu zinaendelea kuchangia sehemu kubwa zaidi ya mzigo wa kiafya unaotokana na dawa za kulevya, ikiwemo vifo vitokanavyo na kuzidisha dozi, ambapo kati ya vifo takriban 600,000 vinavyotokana na matumizi ya dawa duniani, karibu vifo 450,000 vinasababishwa na matumizi yasiyo sahihi ya dawa za kupunguza maumivu.
Fahamu kwa kina dawa hizo za kupunguza maumivu
Dawa hizi hutumiwa mara kwa mara kwa ajili ya kupunguza maumivu, na zinajumuisha dawa kama vile morphine, fentanyl na tramadol. Matumizi yake yasiyo ya kimatibabu, matumizi ya muda mrefu, matumizi mabaya, na matumizi bila usimamizi wa daktari yanaweza kusababisha uraibu wake na matatizo mengine ya kiafya.
Upanuzi wa huduma za matibabu
Ingawa inakadiriwa kuwa watu milioni 64 duniani kote wanaishi na matatizo ya matumizi ya dawa hizo, ni chini ya asilimia 10 pekee ndio wanaopata matibabu kwa sasa, hali inayozifanya nchi kuhitaji miongozo hii ya WHO ili kupanua ufikiaji wa huduma bora na kupunguza vifo.
WHO inasema ni jambo la msingi kuhakikisha kuwa watu wenye utegemezi wa dawa hizi, na wale walio katika hatari ya kuzidisha kipimo, wanapata msaada na huduma za bei nafuu, za kimaadili, zenye ubora wa juu na zinazozingatia ushahidi wa kisayansi.
Mapendekezo haya yaliyoboreshwa yamezingatia mchakato thabiti uliozingatia uwiano wa faida na madhara, maadili, machaguo, unafuu wa gharama, usawa, na uwezekano wa utekelezaji baada ya mapitio ya kina yaliyofanywa na kikundi cha maendeleo ya mwongozo huo.
Mapendekezo
Katika miongozo hii iliyoboreshwa, WHO inasisitiza tena pendekezo lake la matibabu ya kudumu kwa kutumia dawa mbadala, ambayo ni utoaji wa dawa zilizofanyiwa tathmini na wataalamu waliosajiliwa kwa watu wenye utegemezi wa dawa hizi za kupunguza maumivu ili kufikia malengo maalumu ya matibabu.
Pamoja na mapendekezo thabiti ya kuendelea kutumia dawa aina ya methadone na buprenorphine za kumeza, WHO sasa imepanua mwongozo wake ili kujumuisha njia mpya za dawa za sindano za buprenorphine zinazokaa muda mrefu mwilini.
WHO inakusudia kuhakikisha kuwa kila binadamu anayehitaji msaada wa kurejea katika hali ya kawaida anapata huduma stahiki bila ubaguzi na kwa gharama zinazohimilika.
Chini ya usimamizi wa Kamati ya Mapitio ya Miongozo ya WHO, mwongozo kamili unatarajiwa kuchapishwa mwishoni mwa mwaka huu au mapema 2027, ukiwa na maelezo ya kina ya kitaalamu, misingi ya mapendekezo, na maelekezo ya utekelezaji.