Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkwamo wa sasa wa mabaharia katika eneo la vita hakuna mfano wake tangu baada ya Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia

Wanamaji wanne wakiwa wamevaa mavazi ya rangi ya machungwa na kofia ngumu wakipumzika kwenye bodi ya meli, wakinywa kutoka kwenye vikombe na kunywa chupa moja.
© IMO Mabaharia wakili kiamsha kinywa ndani ya meli ya usafirishaji wa baharini.

Mkwamo wa sasa wa mabaharia katika eneo la vita hakuna mfano wake tangu baada ya Vita Vikuu Vya Pili Vya Dunia

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO), limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya maelfu ya mabaharia waliokwama katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kufuatia kuongezeka kwa mvutano wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, likisema hali hiyo haina mfano katika enzi ya baada ya Vita Vikuu Vya Pili ya Dunia, WW2.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, takribani mabaharia 20,000 wanaendelea kubaki ndani ya meli zipatazo 2,000 katika Ghuba ya Uajemi, wakishindwa kuondoka kutokana na hatari ya mashambulizi katika njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafiri wa baharini.

Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz, unaounganisha Ghuba ya Oman na Ghuba ya Uajemi, na kutenganisha Iran na Oman, UAE, na Qatar.
© NASA Njia ya meli muhimu ya kimkakati ya Mlango-Bahari wa Hormuz imeoneshwa ikitenganisha mataifa ya Falme za Kiarabu na Iran.

Meli zakwama katika njia muhimu ya kimataifa

IMO imesema kabla ya kuanza kwa mzozo huo, wastani wa meli 150 zilikuwa zinapita kila siku katika Mlango wa Hormuz, lakini kwa sasa ni meli nne au tano pekee zinazoweza kuvuka kwa tahadhari kubwa.

Hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa mapigano katika eneo hilo, huku Iran ikieleza kuwa itaruhusu kupita kwa meli “zisizo na uhasama” pekee, jambo linaloongeza taharuki na sintofahamu kwa sekta ya usafiri wa baharini.

Mashambulizi dhidi ya meli yazua hofu

Kwa mujibu wa IMO, tangu kuanza kwa mzozo huo mwezi mmoja uliopita, mashambulizi 19 dhidi ya meli yameripotiwa katika eneo hilo. Mabaharia 10 wamepoteza maisha huku wanane wakijeruhiwa kufuatia mashambulizi hayo.

Tukio la hivi karibuni lilihusisha shambulio dhidi ya meli kubwa ya mafuta karibu na pwani ya Dubai, ambalo linadaiwa kufanywa kwa kutumia ndege isiyo na rubani yenye silaha. Hata hivyo, sababu za kulengwa kwa meli hizo bado hazijabainika wazi.

Ingawa mashambulizi yameonekana kupungua katika siku za hivi karibuni, hali inaendelea kuwa tete huku jitihada za kidiplomasia za kutafuta suluhu zikiendelea.

Meli ya mizigo inasafiri katika bahari ya wazi.
IMO/Pankaj Gautham Meli ya mizigo inasafiri katika bahari ya wazi. (Maktaba)

Usalama wa mabaharia watiliwa mkazo

Akizungumzia hali hiyo, Mkurugenzi wa IOM, Damien Chevallier amesema kuwa ukubwa wa tatizo hilo haujawahi kushuhudiwa katika historia ya kisasa.

Amesema mabaharia hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira hatarishi ya vita kwa zaidi ya mwezi mmoja, hali inayowaweka katika msongo mkubwa wa mawazo na hatari ya kiafya na kiusalama.

IMO imetoa wito kwa pande zote zinazohusika kupunguza mashambulizi na kuwezesha uhamishaji salama wa mabaharia hao kutoka eneo la hatari.

Wakati huo huo, Shirikisho la Kimataifa la Wafanyakazi wa Usafirishaji (ITWF) Limeripoti kupokea zaidi ya ujumbe 1,000 kutoka kwa mabaharia waliokwama wakielezea hofu na kuomba kurejeshwa nyumbani.

Changamoto za uokoaji na usambazaji

Licha ya changamoto hizo, meli zilizokwama zinaendelea kupatiwa mahitaji muhimu kama chakula, maji na mafuta kupitia kampuni zinazofanya kazi kutoka Saudi Arabia na Oman.

Hata hivyo, IMO imeeleza kuwa si salama zaidi kwa meli kubaki bandarini, hivyo nyingi zinaendelea kuzunguka ndani ya Ghuba ya Uajemi zikisubiri hali ya usalama itengemae.

Aidha, shirika hilo limeitaka Iran kufafanua vigezo vinavyotumika kutambua “meli yenye uhasama” ili kupunguza hatari kwa meli zinazopita katika eneo hilo.

Picha ya satelaiti ya Mlango-Bahari wa Hormuz, ikionyesha njia nyembamba ya maji kati ya Peninsula ya Arabia na Peninsula ya Musandam ya Oman.
© NASA/GSFC/Jacques Descloitres Picha ya satelaiti ya mlango wa bahari wa Hormuz

Athari kwa biashara ya kimataifa

Mlango wa Hormuz ni moja ya njia muhimu zaidi za usafiri wa baharini duniani, ukipitisha takribani asilimia 20 ya mafuta na gesi ya dunia. Hivyo, hali ya sasa ina athari kubwa kwa biashara ya kimataifa na uchumi wa dunia kwa ujumla.

Wasiwasi wa muda mrefu

IMO imeonya kuwa hali hiyo inaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa sekta ya ubaharia, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya watu wanaotaka kuingia katika taaluma hiyo.

Amesisitiza kuwa usalama wa mabaharia ni msingi wa uendelevu wa biashara ya kimataifa, kwani bila wao, minyororo ya usambazaji wa dunia haiwezi kufanya kazi.

Kwa ujumla, IMO imetoa wito wa hatua za haraka za kidiplomasia na kiusalama ili kulinda maisha ya mabaharia na kuhakikisha usafiri salama katika moja ya njia muhimu zaidi za kimataifa.