Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu ya haki za kisheria inapaswa kutumia lugha inayoeleweka na jamii: Wakili Mengo

Mahojiano na watu wawili kwenye meza ya mviringo katika studio na nembo kubwa ya Umoja wa Mataifa kwenye skrini nyuma yao.
UN News/Feissal Kirwa Onyonge Mengo kijana mpigania haki za wanawake, mtafiti na wakili kutoka Mahakama Kuu ya Kenya ambaye pia anafanyakazi na shirika la kimataifa la maendeleo la Hivos.

Elimu ya haki za kisheria inapaswa kutumia lugha inayoeleweka na jamii: Wakili Mengo

Haki za binadamu

Onyonge Mengo kijana mpigania haki za wanawake, mtafiti na wakili kutoka Mahakama Kuu ya Kenya ambaye pia anafanyakazi na shirika la kimataifa la maendeleo la Hivos kupitia programu inayosaidia mashirika ya kiraia kuimarisha mifumo ya kisheria, amesema juhudi za kusaidia wanawake wanaodhulumiwa kijinsia bado zinakumbwa na changamoto nyingi hususan nchini Kenya.

Katika mahojiano na Flora Nducha wa UN News Wakili Mengo, amesema anafanya kazi ya kusaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kuhakikisha yanatekeleza majukumu yao ipasavyo hasa pale ambapo serikali haiwezi kuingilia moja kwa moja.

“Kuna mashirika mengi sana ambayo yanafanya kazi ya kuwasaidia wanawake waliodhulumiwa kijinsia kupata haki ya fidia,” amesema, akiongeza kuwa msaada huo unalenga kuhakikisha waathirika wanapata haki stahiki.

Hata hivyo, ameonya kuwa mfumo wa sheria nchini Kenya  bado una mapungufu makubwa. “Imekuwa ngumu zaidi kwa manusura kupata haki kwa sababu sheria haijatilia mkazo sana suala la mauaji ya wanawake,” amesisitiza, akieleza kuwa hali hiyo inawafanya waathirika wengi kupoteza imani na mfumo wa haki na kujitenga kimya kimya.

Elimu, lugha na mageuzi ya mfumo ni suluhisho

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Mengo amesema mawakili pamoja na taasisi kama Law Society of Kenya wanaendelea kufuatilia kesi na kushinikiza serikali pamoja na idara zake kuchukua hatua madhubuti.

Amesisitiza kuwa serikali ina jukumu kubwa hasa katika kushughulikia makosa ya jinai, lakini pia jamii inahitaji kuelewa mchakato wa sheria. “Ni muhimu kuelezea kuwa mtu akipewa dhamana haimaanishi haki haijatendeka, bali kesi bado inaendelea,” amesema.

Aidha, ameweka mkazo mkubwa kwenye umuhimu wa elimu ya kisheria inayolenga wananchi kwa lugha wanayoielewa vyema. “Kuna hitaji kubwa sana la elimu, lakini mara nyingi elimu inatolewa kwa lugha ya Kiingereza au Kiswahili ambazo wengi hawaelewi,” ameeleza, akiongeza kuwa wanawake wengi wanaokumbwa na ukatili wa kijinsia wanaishi maeneo ya vijijini na hutumia lugha za mama.

“Ni muhimu kuwafikia kwa lugha wanayoelewa na kuwaelekeza hatua za kuchukua, fanya moja, fanya mbili, fanya tatu,” amesema, huku akisisitiza kuwa ushahidi ni nguzo kuu katika kesi za ukatili wa kijinsia, ambazo mara nyingi ni nyeti na ngumu kuthibitisha.

Picha ya mwanasheria wa kike wa Kenya akiwa ameketi katika studio ya kitaalamu akiwa na kipaza sauti na skrini ya nembo ya Umoja wa Mataifa nyuma.
UN News/Feissal Kirwa Onyonge Mengo kijana mpigania haki za wanawake, mtafiti na wakili kutoka Mahakama Kuu ya Kenya ambaye pia anafanyakazi na shirika la kimataifa la maendeleo la Hivos.

Uelewa wa mchakato wa sheria na ushahidi

Wakili Mengo pia alisisitiza haja ya jamii kuelewa jinsi mfumo wa sheria unavyofanya kazi ili kuepuka kukata tamaa mapema.

“Ni muhimu kuelezea umma kuwa mtu akipewa dhamana haimaanishi haki haijatendeka, bali kesi bado inaendelea,” alisema.

Amebainisha kuwa kesi za ukatili wa kijinsia ni nyeti na mara nyingi hukosa ushahidi wa kutosha, hali inayoweza kuathiri matokeo ya kesi.

“Sheria inafuata ushahidi, na wakati mwingine ushahidi unaweza kukosekana kwa urahisi katika kesi hizi nyeti,” ameeleza, akihimiza juhudi zaidi za kuhakikisha waathirika wanapata msaada na haki wanayostahili.