Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katikati ya ukame, FAO Kenya yajengea uwezo kaya ili zisiyumbe kiuchumi na kijamii

Wafanyakazi wa FAO na mwanamume mmoja wa eneo hilo wanashughulikia mbuzi mmoja huko Isiolo, Kenya, wakiwa wamezungukwa na kundi la mbuzi katika mazingira ya vijijini.
© FAO Kampeni ya upatiaji mifugo dawa za minyoo na udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa nchini Kenya.

Katikati ya ukame, FAO Kenya yajengea uwezo kaya ili zisiyumbe kiuchumi na kijamii

Tabianchi na mazingira

Nchini Kenya katika kaunti za Isiolo, Garissa, Samburu na  Mto Tana, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limeendesha kampeni ya upatiaji mifugo dawa za minyoo na  udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa, sambamba na kupatia wananchi fedha taslimu bila masharti kama mojawapo ya kujengea jamii mnepo wakati wa ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. 

Tweet URL

Huko kaunti ya Isiolo, Kaskazini mwa Kenya hapa huduma inaendelea ya kupatia mbuzi dawa ikiwemo za minyoo na kinga dhidi ya vimelea vya magonjwa, mradi wa Mfuko Maalum wa Shughuli za Ukarabati wa Dharura, SFERA ambao unatekelezwa na FAO kupitia ufadhili wa dola 500,000 kutoka serikali ya Ubelgiji.

Miezi miwili iliyopita kabla ya hatua hii hali ilikuwa tete kwa wafugaji kama anavyoelezea Alfred Tulune mkazi wa hapa Isiolo.

“Kutokana na kiangazi, wanyama walikufa na ni kwa sababu mito yote ilikauka. Wanyama wanakwenda mbali kama sisi kutafuta maji. Ndama walikufa kwa sababu muda wanaotembea kwenda kusaka maji kati ya saa moja hadi saa sita, na wakifika wanakunywa maji  lakini tena inakuwa ni muda mrefu hadi warejee wapate chakula.”

Lakini kulikoni mifugo? Dkt. Joseph Mathooko ni Meneja wa Mradi huo kutoka FAO nchini Kenya.

“Mifugo ilitibiwa ili iendelee kuwa na hali nzuri ya mwili na izalishe maziwa, na pia kuwa na thamani sokoni kwa kupatia kipato.  Wakati huo huo, FAO ilitazama kaya zilizo hatarini zaidi ambazo zilikuwa zinakosa mapato na kushindwa kujikimu. Hivyo tuligawa fedha taslimu dola 84 bila masharti kwa kila kaya. Huu ulikua ni msaada wa kina, ukizingatia kwamba jamii za wafugaji hutumia mifugo kama benki na kama mashine ya kuchukua fedha au ATM."

Afisa huyo anaendelea kusema kuwa, "wanapohitaji pesa, wanaenda kuuza mifugo sokoni ili waweze kukidhi mahitaji ya familia. FAO iliwezesha kudumisha maisha ya kaya 2,000 katika kaunti nne za Samburu, Isiolo, Garisa na Mto Tana , ambazo zilikuwa miongoni mwa kaunti 9 zilizobainishwa kuwa hatarini zaidi na zilihitaji msaada wa haraka ili kuwalinda kabla Athari mbaya za ukame hazijaongezeka.”

Mnufaika wa mradi huu ni Leparakuo Lemirikicha anazungumza. Akisema shilingi 9210 ni takribani dola 71.

“Ninashukuru hii miradi wametusaidia, wametupatia shilingi 9210 ambayo tumeweza kununua chakula ambacho kitatufaa kwa wiki mbili.  Tunaomba msaada mwingine tena kama inawezekana watusaidie. Na leo pia wametusaidia kudunga mbuzi dawa na kuwaosha ili wasiliwe na kupe na mbuzi wawe na afya nzuri. Ni hicho tu ninaomba muendelee kutusaidia.

Kikundi cha wachungaji Waafrika wakichunga kundi kubwa la mbuzi huko Isiolo, Kenya.
© FAO Kampeni ya upatiaji mifugo dawa za minyoo na udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa nchini Kenya.

Mtaalamu kutoka FAO ambaye ameshuhudia kampeni hii ni Rina Wangila yeye anasema kuwa ,"“wafugaji wana furaha sana na wanapokea vyema msaada unaotolewa na FAO pamoja na serikali ya Ubelgiji. Shughuli hizi zinalenga kupunguza athari mbaya za ukame. Tunatarajia kuwa kupitia huduma tulizotoa na kuunga mkono hapa, ufugaji bora wa mifugo utaendelea kusaidia kaya katika masuala ya chakula, lishe na kipato katika ngazi ya kaya.”