Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kipindupindu chaghubika eneo la Kusini mwa Afrika kufuatia mafuriko: WHO

Mama na mwanae wakisubiri huduma katika kituo cha matibabu ya kipindupindu katika jimbo la Kivu Kusini, DR Congo. (kutoka Maktaba)
© UNICEF/Jospin Benekire Mama na mwanae wakisubiri huduma katika kituo cha matibabu ya kipindupindu katika jimbo la Kivu Kusini, DR Congo. (kutoka Maktaba)

Kipindupindu chaghubika eneo la Kusini mwa Afrika kufuatia mafuriko: WHO

Afya

Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, leo limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la kasi la wagonjwa wa kipindupindu katika ukanda wa Kusini mwa Afrika mwanzoni mwa mwaka huu wa 2026, likihusisha hali hiyo na mafuriko makubwa, uharibifu wa miundombinu na kuongezeka kwa watu wanaohama makazi yao kutokana na majanga.

Katika uchambuzi wake uliotolewa tarehe 26 Februari 2026 mjini Brazzaville Jamhuri ya Congo, shirika la WHO limesema wagonjwa wa kipindupindu wameongezeka kwa zaidi ya mara saba katika wiki sita za mwanzo wa mwaka huu ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025

Kati ya tarehe 1 Januari hadi 15 Februari 2026, kumekuwa na jumla ya wagonjwa 4,320 na vifo 56 viliripotiwa katika nchi tano za Malawi, Msumbiji, Namibia, Zambia na Zimbabwe, ikilinganishwa na wagonjwa 586 na vifo 11 mwaka uliopita.

Watu wakitembea kupitia maji ya mafuriko nchini Msumbiji, wakibeba vitu vyao na kusaidiana wakati wa msiba.
© IOM/Burak Cerci Wakazi wakitembea katikati ya maji ya mafuriko nchini Msumbiji.

Nchi 13 zaripoti mlipuko wa kipindupindu

WHO imebainisha kuwa ongezeko hilo linatokea licha ya kupungua kwa ujumla kwa wagonjwa wa kipindupindu barani Afrika, ambapo kulikuwa na upungufu mkubwa katika miaka ya karibuni. 

Hata hivyo, nchi 13 bado zinaripoti milipuko ya ugonjwa huo, huku ukanda wa Kusini mwa Afrika ukiendelea kuwa kitovu kikuu tangu mwaka 2023, hasa wakati wa msimu wa vimbunga uliopita. Msumbiji imeelezwa kuchangia karibu asilimia 90 ya visa vyote katika ukanda huo mwaka huu, kufuatia mafuriko makubwa yaliyoathiri zaidi ya watu 700,000.

Shirika hilo limeeleza kuwa mvua kubwa kuliko kawaida na msimu wa vimbunga unaoendelea kati ya Januari hadi Aprili umeongeza hatari ya maambukizi, huku maeneo 27 yakitambuliwa kuwa katika hatari kubwa kutokana na changamoto za upatikanaji wa maji safi, huduma za usafi wa mazingira na milipuko ya mara kwa mara ya kipindupindu.

Kwa mujibu wa Marie Roseline Darnycka Belizaire wa WHO, ongezeko hilo limeonesha wazi namna majanga yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi yamezidisha hatari za afya ya umma, huku WHO ikiendelea kushirikiana na mamlaka za kitaifa kutoa msaada wa dharura na kuimarisha mifumo ya afya.

Mhudumu wa afya wa 'labo moto' anasafiri kwa pikipiki kumtembelea wagonjwa wa kipindupindu
© WHO/PAHO Mhudumu wa afya wa 'labo moto' anasafiri kwa pikipiki kumtembelea wagonjwa wa kipindupindu

Hatari ya kuongezeka kwa wagonjwa wa kipindupindu

WHO imeonya kuwa kati ya mwezi Machi hadi Agosti 2026, ukanda huo unaweza kushuhudia wagonjwa wapya kati ya 12,000 hadi 22,000 wa kipindupindu iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa. Sababu kuu zinazochangia ni pamoja na vimbunga vya kitropiki, mafuriko, migogoro, kuhama kwa watu pamoja na uhaba wa huduma za maji safi hususan katika maeneo ya mijini.

Kwa sasa, WHO na washirika wake wanaendelea kusaidia juhudi za kukabiliana na dharura hiyo kwa kusambaza vifaa vya afya, kuimarisha uratibu wa huduma, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa na kuongeza hatua za kinga. Shirika hilo pia limesisitiza umuhimu wa kuongeza kwa haraka hatua za afya ya umma, zikiwemo utoaji wa chanjo dhidi ya kipindupindu, upatikanaji wa maji safi na huduma bora za usafi wa mazingira.

WHO imekumbusha kuwa kipindupindu ni tishio kubwa la afya ya umma duniani na mara nyingi huashiria changamoto za ukosefu wa usawa na maendeleo duni ya kijamii na kiuchumi. Hivyo, imehimiza uwekezaji zaidi katika huduma za maji safi, usafi wa mazingira na mifumo ya afya ili kuzuia milipuko ya ugonjwa huo na kulinda maisha ya watu walio hatarini.