Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kenya yajivunia hatua nzuri katika kuwaondolea wanawake changamoto ya maji

Picha ya karibu ya mikono ya mtu akinywa maji kutoka kwenye bomba la kioski.
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn Mradi wa maji unaondeshwa na UN-Hbaitat unahakikisha upatikanaji wa maji safi kwa wakazi huko Mtwapa, Mombasa Kenya.

Kenya yajivunia hatua nzuri katika kuwaondolea wanawake changamoto ya maji

Na Anold Kayanda
Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jana Machi 22, Ulimwengu umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Maji. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika nchi 53 na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya maji na usafi, UN Water, kwa makadirio, wanawake na wasichana hutumia saa milioni 250 kwa siku kusaka maji.

Katika mazungumzo yafuatayo yaliofanyika jijini New York, Marekani kati ya Anold Kayanda wa Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa na Hanna Wendot Cheptumo Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Maslahi ya Watoto wa Kenya, Nchi hiyo ya Afrika Mashariki inajivunia kupiga hatua katika kuitatua changamoto hiyo.
 
Waziri Hanna Wendot Cheptumo anaeleza kwamba Kenya kupitia mfuko ilioupa jina NGAAF yaani National Government Affirmative Action Fund, mfuko wa fecha mahususi kusaidia makundi maalumu katika jamii hususani wanawake kupitia wawakilishi wa wanawake.
 
Pesa hizo wanazopewa wanawake si mkopo hivyo hawarudishi lakini wanatakiwa kuzitumia kijiendeleza “na hizo nidizo wanatumia kununua matanki ya maji” anasema Bi. Cheptumo.
 

Visima vya jumuiya

 
Pia kupitia miradi ambayo iko vijijini, Serikali ya Kenya inachimba visima vya maji vya jumuiya na wanaweka sola au mashine za kuvuta maji kwa njia ya nishati ya jua kwa hiyo hakuna mzigo au gharama ya umeme kwa wanawake hao.
 
Waziri Hanna Wendot Cheptumo anakumbuka akisema, “hata mimi nikiwa mdogo nilikuwa ninaenda kilomita saba kwenda kutafuta maji lakini saa hizo ukienda kijijini unapata maji yako hapo na haulipishwi. Unaenda unachota maji yako na unaenda.”
 

Mabwawa

 
Aidha, kwa mujibu wa Bi. Cheptumo, Serikali ya Kenya imechimba mabwawa ya kusambaza maji katika vijiji na ni kazi ambayo inaendelea, “tunataka kusema hata kama maji hayajafikia kila mahali, lakini serikali iko na mikakati ambayo imewekwa ya kuhakikisha kila mtu anapata maji.Hupiti hata kilomita moja. Lakini sanasana weni sasa wana maji nyumbani.” Anahitimisha.