Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Lebanon: Idadi ya watoto wanaouawa au kujeruhiwa ni sawa na darasa moja kwa kila siku

Wavulana wanne wadogo wanakaa katika duara kwenye sakafu ya chumba kikubwa ambacho hutumika kama makazi ya muda. Nyuma yao kuna mahema ya kambi ya kijani kibichi, na nyuma, watu wengine wanaweza kuonekana. Hii ni shule ya umma huko Beirut, Lebanon, iliyobadilishwa kuwa makazi ya watu waliohamishwa kwa sababu ya mgogoro, ambapo Mpango wa Chakula Ulimwenguni (WFP) unatoa chakula moto.
© WFP/Mustapha Ghabris WFP inasaidia familia za wakimbizi na chakula cha moto huko Beirut, Lebanon.

Lebanon: Idadi ya watoto wanaouawa au kujeruhiwa ni sawa na darasa moja kwa kila siku

Amani na Usalama

Hali ya kibinadamu nchini Lebanon imeendelea kuwa mbaya kufuatia kuongezeka kwa mapigano huko Mashariki ya kati tangu mwanzoni mwa Machi 2026 baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran na kisha Iran kujibu mashambulizi na kisha athari za vita hiyo kusambaa katika nchi jirani.

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu OCHA imeeleza kuwa mashambulizi ya anga, mizinga na operesheni za kijeshi zimeathiri kwa kiasi kikubwa raia na miundombinu muhimu.

Taarifa hiyo imeeleza zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine 2,584 kujeruhiwa, huku watoto wakiathirika zaidi.

Vifo

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya watoto UNICEF, Ted Chaiban, amesema ongezeko hilo la vurugu linasababisha “idadi ya watoto wanaouawa au kujeruhiwa kufikia sawa na darasa moja kila siku.”

Mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya na misaada yameongezeka, ambapo wahudumu wa afya 31 wameuawa tangu tarehe 2 Machi.

Hospitali tano na vituo 49 vya afya vimefungwa kutokana na uharibifu, hali inayozuia upatikanaji wa huduma muhimu. Pia, mfanyakazi wa misaada na watoto wawili waliuawa katika shambulio moja, huku mwandishi wa habari na mke wake wakipoteza maisha katika tukio jingine.

Moshi ukiongezeka kutokana na mashambulizi ya ndege juu ya mji wa Beit Mery, Lebanoni, na Bahari ya Mediterania nyuma.
© World Vision Mashambulio ya anga kwa Beit Mery, Lebanon.

Wakati huohuo, zaidi ya watu milioni 1.2 wamelazimika kuyahama makazi yao, huku 134,439 wakihifadhiwa katika makazi ya muda 636, hasa katika maeneo ya Beirut na Mount Lebanon. Makazi hayo yanakabiliwa na msongamano mkubwa na upungufu wa huduma muhimu kama maji, umeme na faragha.

Elimu

Sekta ya elimu pia imeathirika vibaya, ambapo shule 472 zinatumika kama makazi ya wakimbizi, na kuwanyima maelfu ya watoto haki ya elimu.

Mashirika ya kibinadamu yanatoa wito wa kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu, yakisisitiza ulinzi wa raia, wahudumu wa afya na waandishi wa habari ili kuzuia kuongezeka kwa maafa.