Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro Palestina watumbukiza wasichana kwenye hatari na dharura ya afya ya akili.

Msichana Mpalastini mwenye mkia wa farasi amesimama juu ya paa katika Jiji la Gaza, akitazama mandhari ya majengo yaliyoharibika.
© WFP/Maxime Le Lijour Msichana akiwa anatazama kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mashambulizi huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli

Mgogoro Palestina watumbukiza wasichana kwenye hatari na dharura ya afya ya akili.

Na Abdelmonem Makki
Afya
  • Watoto wahofia kifo ki karibu
  • Ndoa za utotoni zilipungua sasa zinashamiri
  • Asilimia 10 ya visa vya kujiua ni vya waliopitia ukatili wa kimwili

Zaidi ya miaka miwili ya vurugu zisizokoma, uhamishaji wa watu, na upotevu wa maisha imesukuma watoto na vijana huko Palestina, eneo linalokaliwa kimabavu na Israeli katika kile ambacho afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa anakielezea kama “dharura kubwa ya afya ya akili,” huku wasichana wakikabiliwa na hatari kubwa zaidi, ikiwemo kuongezeka tena kwa ndoa za utotoni.

Sima Alami, Afisa wa Programu ya Vijana na Barubaru katika shirika la Umoja wa Matiafa la Idadi ya Wat una Afya ya Uzazi, (UNFPA), ametia taswira ya kusikitisha inayodhihirishwa na takwimu za kutisha.

Watoto wahofia kifo ki karibu

“Tuna zaidi ya watoto milioni moja hapa Gaza wanaohitaji huduma za msaada wa afya ya akili na msaada wa kisaikolojia,” ameiambia Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa katika mahojiano maalum.

Kiwango cha msongo wa mawazo ni kikubwa sana. Kwa mujibu wa takwimu za UNFPA zilizotajwa na Bi. Alami, asilimia 96 ya watoto huko Gaza wanahisi kwamba kifo kiko karibu. “Hii inaonesha kina cha hofu na maumivu ya kisaikolojia wanayopitia kila siku,” amesisitiza.

Mwanamke mmoja huko Gaza, akiwa amevaa hijabu, anashiriki kikamilifu katika kikao cha kupanga jamii kwa kuandika kwenye ubao mkubwa uliofunikwa na noti za rangi. Mwanamke mwingine anaonekana nyuma, akiashiria juhudi za pamoja za kukabiliana na changamoto za mitaa.
© UNFPA/Jukwaa la Maendeleo ya Jamii Ili kuhakikisha watoto wa kike na wasichana wana mazingira salama ya kupata msaada wa haraka na wa muda mrefu dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, UNFPA imetenga maeneo salama, vituo vya vijana na mahema ya wasichana kote Ukanda wa Gaza..

Vijana balehe wana fikra za kujiua

Miongoni mwa vijana balehe—ambao mara nyingi hupuuzwa katika migogoro ya kibinadamu—athari za kisaikolojia ni kubwa pia. Takribani asilimia 61 wanakabiliwa na msongo wa mawazo baada ya tukio la kutisha (PTSD), asilimia 38 wanaugua unyogovu, na asilimia 41 wana wasiwasi mkubwa. “Cha kusikitisha zaidi, mtu mmoja kati ya watano wazima hufikiria kujiua karibu kila siku,” ameongeza.

“Hii si hali ya kawaida ya msongo wa mawazo,” amesisitiza Bi. Alami. “Ni dharura kubwa ya afya ya akili.”

Wasichana wako hatarini zaidi

Ndani ya mgogoro huu, wasichana ni miongoni mwa walio hatarini zaidi. Katika Ukanda wa Gaza, ndoa za utotoni—ambazo hapo awali zilikuwa zinapungua—zimeanza kuongezeka tena kwa kasi. 

Viwango vilishuka kutoka asilimia 25.5 mwaka 2009 hadi asilimia 11 mwaka 2022, lakini sasa vinaongezeka tena huku familia zikihangaika kuishi.

Utafiti wa hivi karibuni wa UNFPA umebaini kuwa asilimia 71 ya waliohojiwa Gaza wameripoti kuongezeka kwa shinikizo la kuwaozesha wasichana walio chini ya miaka 18. 

Katika kipindi kifupi cha ufuatiliaji pekee, zaidi ya leseni 400 za ndoa zilitolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 hadi 16 katika mahakama za dharura—idadi ambayo huenda ni ndogo kuliko hali halisi.

“Baadhi ya familia zinaona ndoa kama mkakati wa kuishi katikati ya uhamishaji, umaskini, na ukosefu wa usalama,” ameeleza Bi. Alami. Wengine wanaamini kuwa ndoa inatoa ulinzi katika makazi yenye msongamano au hupunguza mzigo wa kiuchumi baada ya kupotea kwa vyanzo vya kipato.

Wasichana wawili vijana wa Kipalestina wamesimama kati ya mabomoko ya saruji na mabomoko ya chuma yaliyopotoka katika mji wa Gaza, wakitabasamu huku wakicheza chini ya jua.
UN News Wasichana wawili wa Palestina wanacheza katikati ya uharibifu katika mji wa Gaza

Wasichana balehe wanabeba ujauzito, ni hatari.

Madhara yake ni makubwa, inasema UNFPA kwani mwaka 2025, takribani asilimia 10 ya mimba mpya zilizosajiliwa Gaza zilikuwa za wasichana balehe—ongezeko kubwa ukilinganisha na kabla ya vita.

Wakati huo huo, upatikanaji wa huduma za afya umepungua sana. Ni asilimia 15 tu ya vituo vya afya Gaza vinavyoweza kutoa huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga, hali inayoongeza hatari kwa mama wadogo na watoto wao.

Ndoa za utotoni pia zinawaweka wasichana katika hatari ya ukatili. “Ushahidi unaonesha kuwa asilimia 63 ya wasichana walioolewa katika umri mdogo wamepitia ukatili wa kimwili, kisaikolojia au kingono,” amesema.

 Ripoti pia zinaonesha ongezeko la talaka na matatizo makubwa ya afya ya akili kwa watoto walio kwenye ndoa. Katika hali mbaya zaidi, madhara yanaweza kuhatarisha maisha. “

Familia hazipatii kipaumbele afya ya akili

Zaidi ya matukio 100 ya kutaka kujiua yamerekodiwa miongoni mwa manusura wa ukatili,” amebainisha, akisisitiza kuwa ndoa za utotoni ni aina ya ukatili wa kijinsia.

“Familia nyingi zinaweka kipaumbele kuishi kuliko afya ya akili,” amebainisha Bi. Alami, akisisitiza umuhimu wa kuunganisha huduma za msaada wa kisaikolojia na huduma za chakula, afya, na elimu.