CSW70 ikifunga pazia washiriki waeleza wanachoondoka nacho
CSW70 ikifunga pazia washiriki waeleza wanachoondoka nacho
- Tutoke kwenye vikao sasa tuingie kwenye utekelezaji
- IPU na mikakati ya kufanikisha mabadiliko ya Katiba, sheria na tamaduni
- Ushirikishaji wanaume ni jawabu mujarabu
- Kujumuika na majaji na mahakimu wanawake kumetupatia matumaini.
- Vijana wasiachwe nyuma kokote pale
Hatimaye baada ya takribani wiki mbili mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 unakunja jamvi leo hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani. Maudhui yalikuwa kuendeleza Haki, Sheria na Kuchagiza Hatua kwa ajili ya wanawake na wasichana. Je washiriki wanaondoka na nini?
Wanaume ni wadau katika usawa twende nao sambamba
Hilo ndilo tunamulika kwenye mada kwa kina na tunaanza na Chausiku Kafuti Kuya, Naibu Mrajisi Mahakama Kuu Zanzibar nchini Tanzania na anasema katika wiki mbili walizokuwa hapa, suala kubwa lililozungumzwa ni ushirikishwaji wa watu wote na hilo analibeba na kuondoka nalo.
Anasema, “pamoja na kwamba tunatafuta tunaelimishana masuala ya haki za wanawake na vitu vingine, lakini ushirikishwaji wa wanaume ni kitu ambacho kimesemwa karibu katika matukio mengi tuliyoshiriki.Hivyo muhimu ni kushirikiana kwa sababu tukizungumza peke yetu itakuwa ni sisi kwa sisi tukizungumza na wanaume tunakwenda pamoja na tunaamini tutafanikiwa kwa pamoja.
Vijana ndio dirisha la mabadiliko - ICCAO
Mshiriki mwingine ni Zahra Salehe Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ICCAO linalojihusisha na kuwakwamua vijana nchini Tanzania akihojiwa na Anold Kayanda wa Idhaa hii amesema kwa kushiriki mikutano hii amegundua kuwa changamoto nyingi zinakaribia kufanana kote ulimwenguni na kuna kundi moja katika jamii likizingatiwa linaweza kuwa mwisho wa changamoto ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikivuka kizazi kimoja hadi kingine.
“Kulitizama kundi la vijana kama ndio sehemu ya kufanya mabadiliko kwa sababu kuna matatizo yanayohama kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Tuwatazame vijana kimkakati kwani tukiwatumia kama kwenye masuala ya afya, basi wajumuishiwe kila sekta kama dirisha la mkakati.”
Majaji na mahakimu wametupa hakikisho chanya
Gertrude Micheni ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika la Kiraia la Jukwaa la Maendeleo ya Wanawake, Demokrasia na Haki, FODDAJ. Nchini Kenya anasema kilichomtia moyo ni kushiriki kwenye vikao na majaji na mahakimu wanawake kutoka Kenya akisema kuwa ushirikiano huo ni muarobaini wa vikwazo vya haki kwa mwanamke.
Bi. Micheni amesema, “tumejua kwamba tukiungana na hawa majaji na wabunge wale wote tumekuwa nao hapa tutasonga mbele kwani wametuambia tukiwa na shida tukiwaambia watapeleka huko mbele na tunaamini kwamba kaunti ya Kajiado haitakuwa kama hapo awali.”
Wakati wa vitendo sio vikao tena
Nasalia na mshiriki kutoka Kenya Elizabeth Waliuba ambaye ni Muasisi na Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Imarisha Usawa linalotumia mchezo wa mpira wa kikapu kusongesha haki za wanawake na wasichana. Yeye anasema “jambo kuu nililojifunza ni kwamba sasa ni wakati wa kutekeleza kwa vitendo waliyoafikiana na si kauli au vikao.
Wanawake tubadili fikra, tuwezeshwe na nani? - Dkt. Tulia
Kwa Dkt. Tulia Ackson - Rais wa Muungano wa Mabunge duniani (IPU), akizungumza nami amemulika mkutano walioshiriki kujadili nafasi ya mabunge kuendeleza haki za wanawake na wasichana kwa kubadili Katiba, sheria na tamaduni zinazomtazama mwanamke kama mtu asiyeweza kuongoza.
Dkt. Tulia amesema, “zama za kusema mwanamke akiwezeshwa anaweza zimepita, awezeshwe na nani? Ni wakati na wanawake nao tubadili mtazamo wa kuona kwamba lazima kwanza mwanaume aseme ndio tutekeleze.Kama mwanamke anaweza kuzaa nusu nyingine ya wakazi wa dunia, na pia nusu nyingine ya wao wenyewe wanawake, mwanamke anaweza pia kuwa kiongozi wa nchi.”