CSW70 imenifanya niamini mimi ninastahili kutatua changamoto - Imelda
CSW70 imenifanya niamini mimi ninastahili kutatua changamoto - Imelda
Mikutano hii inayokutanisha Umoja wa Mataifa watetezi wa haki za wanawake dunia inawapa ujasiri vijana wa kuona kuwa nao wana uwezo na fursa ya kusaka majawabu katika jamii zao. Ni kauli ya kijana wa kike kutoka nchini Uganda anayeshiriki mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake Duniani (CSW70 ) unaoendelea hapa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
Kanyesige Imelda ni mmjoa wa vijana anayehudhuria CSW70 akiwakilisha shirika lake liitwalo UPLIFT West Nile na anasema amekuja kuleta simulizi ya msichana wa West Nile nchini Uganda.
Anasema katika jamii yake wasichana wengi wanakumbana na ukatili wa kijinsia, mimba katika umri mdogo na wengi hawajui kusoma na kuandika. Na shirika lao limejikita kutatua changamoto hizo.
“Tunatoa elimu ya afya ya uzazi, na kuwafundisha wanawake na wasichana kuhusu maumbile yao. Pia tunawafundisha wakina mama kusoma na kuandika katika lugha zao wanazozielewa. Wasichana wengi wanadhani elimu ya uzazi ni suala ni suala nyeti kuzungumziwa na wengi hujizuia kuzungumza kwa uwazi, lakini kwa kazi kubwa tunayofanya tumeweza kuwafundisha na kujielewa wao na maumbile yao na jinsi ya kujilinda. Hii imewafanya wengi wao kuelewa haki zao na pia wamekuwa watetezi wa jamii, na marafiki zao ambao wameacha shule kwa sababu ya unyanyasaji wa kijinsia.”
Pamoja na juhudi hizo Imelda anasema changamoto kubwa wanayokabiliana nayo sasa ni ukata wa fedha.
“Hivi sasa, nadhani hii ni changamoto ya jumla kwa kila asasi za kiraia ambayo tunakabiliwa nayo, kupungua kwa ufadhili. Kwa bahati nzuri, tuna mawazo mengi ambayo tungependa kuyatekeleza, lakini tunakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na kupungua kwa ufadhili hivi sasa. Tunaona sera nyingi zinazotengenezwa na serikali yetu nchini Uganda, lakini kwa bahati mbaya hatuzioni zikifanya kazi halisi ambazo zimekusudiwa.”
Pamoja na changamoto hizo Kijana huyu kutoka Uganda anasema anafurahi kuhudhuria mkutano huu wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani kwani unampa nguvu ya kuendelea kupigania wanawake na wasichana.
“CSW ni mkutano ambao unaweza kumletea athari chanya kwa kila mtu anayehudhuria. Kwangu mimi binafsi, nitaukumbuka mkutano huu, umenifanya nitazame changamoto ninazokabiliana nazo nchini kwangu kwamba mimi ndiye mtu sahihi wa kukabiliana nazo na kuleta suluhisho ambazo zitawaletea manufaa wasichana na wanawake wenzangu. Mkutano huu umenio nesha kwamba mimi ndiye mtu sahihi wa kufanya mabadiliko duniani. Nitauchukua msukumo huu nyumbani, kwamba sote tunaweza kufanya kazi pamoja ili kuweka kipaumbele kwenye sera za usawa wa kijinsia ambazo zinaweza kubadilisha maisha ya msichana huko West Nile.”