Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW70 yang’oa nanga ikisisitiza haki, haki ya kisheria na hatua kwa wanawake na wasichana

Mwigizaji Michelle Williams akizungumza kwenye jukwaa wakati wa tukio katika Umoja wa Mataifa. Skrini kubwa nyuma yake inaonyesha neno 'FEARLESS' mara kwa mara.
UN Wanawake/Ryan Brown Michelle Williams, mwimbaji mshindi wa tuzo ya Grammy na mwigizaji wa Broadway, anazungumza katika Ukumbi wa Baraza Mkuu la Umoja wa Mataifa wakati wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake ya 2026.

CSW70 yang’oa nanga ikisisitiza haki, haki ya kisheria na hatua kwa wanawake na wasichana

Na Leah Mushi
Wanawake

Kikao cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70 kimefungu pazia hii leo jijini New York Marekani, mwaka huu kikibeba maudhui “Haki, haki ya kisheria na Hatua kwa wanawake na wasichana wote”. Zaidi ya washiriki 9000 wakiwemo wawakilishi wa serikali, asasi za kiraia, Umoja wa Mataifa na mashirika yake na wadau wengine wanatarajiwa kushiriki jukwaa hili litakalokunja jamvi 19 Machi likijumuisha mikutano ya kando 750.

CSW70 yang’oa nanga ikisistiza haki, haki ya kisheria na hatua kwa wanawake na wasichana

Ufunguzi Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 umefanyika katika ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na mgeni rasmi ni Katibu Mkuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ambaye ameeleza furaha yake kuwa katika ukumbi uliojaa viongozi waliokataa kukubali ukosefu wa usawa kama jambo lisiloepukika

Katika hotuba yake Guterres amesema dunia bado inaongozwa zaidi na mfumo dume unaowapa wanaume nafasi kubwa ya mamlaka. 

“Tunaishi katika ulimwengu unaotawaliwa na wanaume, na utamaduni unaotawaliwa na wanaume. Usawa wa kijinsia ni suala la mamlaka. Hakuna hatua hata moja mbele kwa haki za wanawake ambayo imewahi kutolewa. Bali imeshinda. Wameshinda vizazi vya wanawake na wasichana, watetezi na wanaharakati, viongozi wa jamii na watafuta haki. Umeshinda wewe wewe.”

Amesema hali hiyo imekuwa changamoto kubwa katika jitihada za kufikia usawa wa kijinsia katika taasisi nyingi duniani. Hata hivyo, ndani ya UN kumekuwa na maendeleo muhimu katika kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za uongozi.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, wakati alipoanza uongozi wake, alijiwekea lengo la kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume katika ngazi za juu za uongozi wa Umoja wa Mataifa. Leo, amesema lengo hilo limefikiwa.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa, wanawake sasa wanaunda nusu kamili ya nguvu kazi ya Umoja wa Mataifa katika vitengo vya kitaaluma na vya juu zaidi. Na kwa mara ya kwanza, tulifikia usawa katika uongozi mkuu. Tumefanya hivyo ikiwa ni miaka miwili kabla ya ratiba - lakini pia natambua imekuwa ni miaka 80 imechelewa.”

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa António Guterres amesisitiza kuwa kufikia usawa wa kijinsia si suala la haki kwa wanawake pekee, bali ni hatua muhimu kwa maendeleo ya dunia nzima. Amesema jamii ambazo wanawake wanapata haki na fursa sawa huwa na maendeleo ya haraka zaidi, uchumi imara na taasisi zenye uwajibikaji zaidi, akisisitiza kuwa kuimarisha usawa wa kijinsia ni msingi muhimu wa kufikia maendeleo endelevu duniani.

Katibu Mkuu UN akizungumza kwenye jukwaa wakati wa hafla ya Siku ya Wanawake Duniani katika Makao Makuu ya UN jijini New York.
UN Wanawake/Ryan Brown Balozi Maritza Chan Valverde wa Costa Rica akizungumza katika Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati wa ufunguzi wa Kikao cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wanawake wanapata haki na fursa sawa katika jamii duniani.

Ametaja maeneo matano muhimu ya kuharakisha haki na usawa kwa wanawake ambayo ni kuhakikisha haki sawa za kiuchumi kwa wanawake, kuimarisha uwakilishi wao katika maamuzi ya kisiasa, kupanua upatikanaji wa elimu na fursa za kazi, kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, pamoja na kulinda haki za wanawake katika dunia ya kidijitali.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Kikao hicho cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani CSW70 Maritza Chan Valverde amezungumzia maudhui ya mwaka huu ambayo ni  “Haki, haki ya kisheria na Hatua kwa wanawake na wasichana wote nakusema kila mtu anajukumu la kufanya “Ondoa vikwazo na uhakikishe kwamba haki inakuwa ukweli halisi kwa kila mwanamke na msichana. Hakuna nchi yenye usawa kamili wa kisheria, na wanawake duniani kote bado wanashikilia 2/3 ya haki za kisheria ambazo wanaume wanazifurahia.” 

Annalena Baerbock akizungumza kwenye jukwaa wakati wa ufunguzi wa kikao cha sabini cha Tume ya Hali ya Wanawake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.
Picha ya UN/Evan Schneider Rais wa Mkutano Mkuu Annalena Baerbock akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa kikao cha 70 cha Tume ya Hali ya Wanawake..

Naye Rais wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock katika hotuba yake ameelezea mapambano ya haki za wanawake hayawezi kutenganishwa na kutafuta haki kwenyewe - kisheria, katika utekelezaji, na madarakani.

Bi. Baerbock amesema kuwa “Haki ulimwenguni kote inahitaji chaguo hai la kuwaamini manusura kila mahali duniani, kuwawajibisha wahalifu kila siku, na kubomoa mifumo inayoendeleza unyanyasaji na ubaguzi.” 

Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, akitoa hotuba kwenye jukwaa wakati wa ufunguzi wa kikao cha sabini cha Tume ya Hali ya Wanawake katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York.
Picha ya UN/Evan Schneider Sima Sami Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha 70 cha Tume ya Hali ya Wanawake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women Sima Bahous alionya kwamba kikao hicho kinafanyika wakati dunia inashuhudia migogoro inayozidi kuwa mibaya. “Tunakutana wakati wa migogoro mingi ya kimataifa. Amani inatuepuka. Na dunia imegawanyika sana na inazidi kuwa na migawanyiko.”

Ukosefu wa usawa wa kijinsia ni suala jingine alilolizungumzia na kueleza namna unavyozidi kuwa mbaya kutokana na migogoro kuanzia Afghanistan, Haiti, Iran, Myanmar, Palestina, Sudan Kusini, Sudan, Syria, Ukraine, Yemen “na kwingineko.”

Mkuu huyo wa UN Women ameunga mkono wito wa kurejea kwa diplomasia na mazungumzo na “kukomesha mauaji kote Mashariki ya Kati, Afrika na kwingineko.”