Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake walinda amani wa UN kutoka Tanzania wasongesha haki na usawa huko DRC

Wanawake wawili wa Tanzania wanaofanya kazi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa wakiwa wamevaa mavazi ya kujificha pamoja na kofia za UN za bluu wamesimama pamoja na wanawake wawili wa eneo hilo katika mazingira ya vijijini.
MONUSCO/Habibu Shabani
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanatembelea wanawake na wasichana huko Beni-Mavivi, jimbo la Kivu Kaskazini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuelimisha kuhusu haki na sheria dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Wanawake walinda amani wa UN kutoka Tanzania wasongesha haki na usawa huko DRC

Wanawake

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC walinda amani aw Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu kwenye kikosi cha 5 cha utayari, TANZQRF-5 wameelezea ni kwa vipi wanasongesha ujumbe wa mwaka huu wa siku ya wanawake duniani, wa “Haki, Sheria, Hatua kwa wote Wanawake na Wasichana.”

Tweet URL

TANZQRF-5 inahudumu chini ya mwamvuli wa Brigedi ya kujibu mashambulizi, FIB ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, huko Beni-Mavivi, jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu.

Tunawasikiliza na changamoto tunawasilisha dawati la jinsia

Miongoni mwao ni Kapteni Zidina Ngililea ambayeni Afisa wa Masuala ya Jinsia jinsia, anasema “jukumu langu kubwa ni kwenda kujenga mahusiano na kusikilizana na raia ambao wako katika eneo letu la uwajibikaji, kuwasikiliza, kugundua shida mbalimbali au changamoto mbalimbali ambazo zinawapata na kwa namna ambayo tunaenda kuzungumza nao.”

Zaidi ya hapo wanawaelimisha jinsi ya kutambua haki na nafasi zao kwenye jamii. “Tunazipokea changamoto zote ambazo zinahusiana na hayo mambo ya unyanyasaji wa kingono na udhalilishaji wa kijinsia tunazipeleka kwenye ofisi husika ambalo ni dawati la jinsia  hapa MONUSCO.”

Haki imeniwezesha kuwa Daktari wa Kinywa na Meno

Mlinda amani Praiveti Diana Kimambo yeye ni daktari wa kinywa na meno amemulika kauli mbiu hiyo katika muktadha wa sheria akisema, “sheria ndio mlinzi wa haki na mimi binafsi nililindwa na sheria. Nikapata haki ya elimu ya udaktari wa kinywa na meno na baadaye kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Na mpaka sasa nipo hapa nchini DRC kama mlinzi wa amani mwanamke kutoka Tanzania nikiendelea kutoa huduma ya udaktari wa kinywa na meno katika kikundi changu.”

Kumnyima mwanamke haki ni kuchelewesha maendeleo ya  jamii

Pamoja na majukumu hayo, walinda amani hawa wanawake pia wamekuwa wakitekeleza majukumu mengine kwa kushirikiana na walinda amani wa kiume. 

Mwanajeshi wa Tanzania wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa amevaa yunifomu anawasiliana kwa uchangamfu na wanawake wawili wa eneo hilo wakati wanapokula pamoja nje.
MONUSCO/Habib Shaban
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania akizungumza na wanawake huko Beni-Mavivi jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) huku wakiandaa chakula, kama sehemu ya kusongesha haki na sheria kwa wanawake.

Praiveti Zulfa Mwita ni dereva wa magari katika kikosi cha TANZQRF-5 na katika suala zima la usawa wa kijinsia anasema, “kwa muda mrefu jamii imekuwa ikifahamu kwamba wanawake hawawezi kutekeleza majukumu yao kama wanavyoweza kutekeleza wanaume katika nyanja mbalimbali. Nikitolea mfano, mimi mwenyewe ni dereva mwanamke ambaye ninatekeleza majukumu yangu sawa sawa na wanavyotekeleza wanaume. Hivyo basi, kumnyima mwanamke haki ya usawa ni kuchelewesha maendeleo katika jamii.”

Wanawake walinda amani wametusaidia sana Oicha

Tangu mwezi Mei mwaka 2013,  vikosi vya Tanzania vimekuwa sehemu ya kulinda amani nchini DRC ambapo Dasisi Kibondo ambaye ni mwanamke mkazi wa eneo hili ametoa tathmini ya utendaji wa walinda amani watanzania.

Tangu zamani tumekuwa tunasumbuliwa na ukosefu wa usalama, kuna akina mama  ambao wanabakwa wakienda kufanya kazi za shamba. Kuna wengi ambao wanapitia shida mbalimbali kutoka na ukosefu wa usalama. Tangu vikundi vya watanzania vimefika huko, tumeanza kuona mabadiliko kidogo kwani ni watu ambao walikuja kutusaidia na tuna imani kama wataendelea kutusaidia, na sisi kwa pamoja tutaweza kurudisha usalama katika nchi ya DRC na hata huku kwetu Oicha.”

Walinda amani wanawake wa UN kutoka Tanzania wanavyosongesha haki nchini DRC

Uwepo wa walinda amani wanawake unajengea imani jamii

Swali la kujiuliza je, ni nini umuhimu wa walinda amani wanawake katika jukumu la ulinzi wa amani? Kamanda wa TANZQRF-5 Luteni Kanali Daudi Nkungu anafafanua akisema, “wamekuwa na mchango mkubwa sana hasa katika kuifikia jamii ambayo imeathirika vibaya na machafuko haya yaliyopo kwenye eneo hili la uwajibikaji.”

Mathalani amesema wanawake wamekuwa na msaada mkubwa sana kwenye kupata taarifa mbalimbali kutoka kwa jamii inayowazunguka. “Tukitambua ya kwamba waathirika wakubwa wa haya machafuko ni wanawake na watoto. Hivyo katika kikundi changu wamekuwa wakitumika wanawake kuwafikia wanawake wenzao kwa sababu mwanamke akiona mlinda amani mwanamke inamjengea imani kuzungumza na kutoa taarifa tofauti na ilivyo kwa walinda amani wa kiume. Utaona kwamba wanawake wanayo nafasi kubwa na msaada mkubwa wa majukumu.”

Ujumbe wa Kamanda wa TANZQRF-5 kwa wanawake

“Waoneshe kwamba sasa uaminifu kweli unawekwa juu yao, wahakikishe kwamba wanatekeleza majukumu ipasavyo kwa kadiri walioaminiwa,” amesema Luteni Kanali Kyungu akiongeza kuwa, “jamii pia ambayo tunaihudumia kwenye hili eneo la uwajibikaji iendelee kuwaamini hawa wanawake ambao wameaminiwa kushiriki kwenye ile jukumu la ulinzi wa amani.”