Ndoa za utotoni zaongezeka Gaza huku vita ikikandamiza haki za mabinti
Ndoa za utotoni zaongezeka Gaza huku vita ikikandamiza haki za mabinti
- Watoto wa kike wanaozwa ili familia iondokane na umaskini
- Wakiwa kwenye ndoa shida ni maradufu ya zile walizokumbana nazo kwenye familia
- UNFPA imechukua hatua kunusuru watoto wa kike na zahma hiyo
Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi UNFPA limesema ndoa za utotoni zimeongezeka kwa kasi kote ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, huku kuhama makazi, umasikini, na kuporomoka kwa mifumo ya sheria na ulinzi kukizilazimisha familia kufanya maamuzi magumu.
Makala ya UNFPA kutoka Gaza iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika hilo, Machi 4, 2026, inasema “kwa familia nyingi, kumwozesha binti huonekana kama njia ya kupunguza mzigo wa kifedha au kumlinda msichana dhidi ya unyanyasaji wa kingono ambao hufanywa kuwa jambo la kawaida kwenye maeneo yenye mizozo.”
*Katika makala hii, majina ya wahusika yamebadilishwa ili kuhakikisha ulinzi wao na miongoni mwao ni Amal.
Amal mwenye umri wa miaka 15, kutoka Khan Younis, akizungumza kwa uchungu baada ya kuozeshwa akiwa na umri wa miaka 14 anasema, “niliolewa kukimbia ugumu wa maisha, nikakutana na shida nyingine," akiongeza kuwa, "shangazi yangu aliponiomba niolewe na mwanawe, baba yangu alikubali mara moja. Hakukuwa na harusi, hakuna gauni, hakuna sherehe. Ilionekana kama mpango wa kujiondoa kwenye mzigo. Niliolewa ili kukimbia shida moja, nikakuta nyingine.”
Vita vinarudisha nyuma maendeleo yaliyopatikana
Vita hivi vinarudisha nyuma maendeleo ya miongo kadhaa, kwani mwaka 2022 ndoa za wasichana chini ya miaka 18 zilikuwa zimepungua hadi asilimia 17.9, lakini sasa maofisa wa kijamii wanaripoti kuwa viwango hivyo vinapanda kwa kasi kubwa.
Hali hii inasababisha hatari kubwa za mimba za utotoni, ambapo mwezi Desemba 2025, takriban asilimia 10 ya wajawazito wapya walikuwa ni wasichana balehe ambao wengi wao wana utapiamlo na upungufu wa damu.
Hiba, aliyekimbia kutoka Beit Hanoun, aliolewa akiwa na miaka 16 amesimulia, “daima nilikataa wazo la ndoa. Nilitaka kufanikiwa kwenye mradi wangu wa saluni na kujenga maisha yangu ya baadaye. Lakini maisha niliyoota yalitoweka. Nilipata mimba zilizokuwa zinaharaibika mara kwa mara ndani ya miezi sita. Vita ilichukua nyumba yangu, kazi yangu, na hata ujauzito wangu.”
Mifumo ya haki na ulinzi imeporomoka kabisa
Familia nyingi zinatumia ndoa kama aina ya hifadhi au "Sutra" dhidi ya unyanyasaji, lakini ndoa hizo huleta tishio la ukatili kutoka kwa wenza na kunyimwa haki. Safa mwenye umri wa miaka 16 aliyekubali kuolewa akiwa na miaka 15 akidhani atapata utulivu, ameeleza, “Nilikubali kuolewa nikiwa na umri wa miaka 15 kwa sababu mwanaume huyo alisema ana nyumba, nilifikiri nitakuwa salama na utulivu. Hakukuwa na nyumba, hakuna sherehe, bali hema tu. Nilijihisi mzee kuliko umri wangu, nikibeba majukumu yaliyo mazito sana kwangu. Sasa nasubiri kujifungua nikiwa kwenye chumba kilichoharibiwa, baada ya kupoteza kila kitu.”
Kuharibiwa kwa shule pia kumechangia ongezeko hili kwani elimu ilikuwa kinga kuu dhidi ya ndoa za utotoni, lakini sasa shule nyingi zimekuwa kambi za wakimbizi. Manal mwenye umri wa miaka 17, ameeleza kwa masikitiko akiwa kwenye kituo cha msaada, “kwa sababu ya vita, nililazimika kuacha shule. Leo nimekaa katika moja ya shule iliyogeuka kuwa eneo la hifadhi, nikiishi kama mke chini ya paa la maumivu, si kama mwanafunzi anayebeba vitabu vyake na kuvuta picha ya maisha yake ya baadaye.”
UNFPA inafanya nini?
UNFPA kwa sasa inaunga mkono vituo 20 vya usalama na mahema 11 ya wasichana kote Gaza ili kutoa msaada wa kisaikolojia, afya ya uzazi, na elimu ya kuzuia ndoa hizi za mapema. Licha ya changamoto hizi, jitihada za kuwajengea wasichana uwezo wa uongozi na stadi za maisha zinaendelea kupitia vituo hivyo ili kuwapa matumaini ya kesho iliyo bora.
Yasmine, kijana anayefanya kazi ya kujitolea, amesisitiza umuhimu wa vituo hivyo akisema, “hema la wasichana ni muhimu si kwa sababu tu linasaidia wasichana balehe, bali pia kwa sababu linahamasisha kujitunza katika nyakati hizi ngumu. Idadi kubwa ya watu wanaojitokeza na kuuliza maswali ya msingi inaonesha jinsi msaada huu unavyohitajika sana."