Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ITU na UNHCR zatunukiwa tuzo ya GLOMO kwa ujumuishaji wakimbizi kidijitali

Kikundi cha wanafunzi wa shule za msingi wenye tabasamu katika sare za rangi ya waridi wanakusanyika karibu na kompyuta kibao katika kituo cha jamii katika kambi ya wakimbizi nchini Kenya, sehemu ya mradi wa UNHCR Instant Network Schools.
UNHCR/Catherine Wachiaya
Wanafunzi wakitumia kompyuta mpakato katika mraddi wa shule wa (INS) kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya. Mradi wa INS ni wa ushirikiano baina ya UNHCR na wakfu wa Vodafone.

ITU na UNHCR zatunukiwa tuzo ya GLOMO kwa ujumuishaji wakimbizi kidijitali

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR na  na Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU wamepokea Tuzo ya Mwenyekiti katika Tuzo za Kimataifa za Simu (GLOMO) kwa ajili ya mpango wao wa “Kuwaunganisha Kidijitali Wakimbizi” , unaolenga kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa watu waliokimbia makazi yao. 

Tuzo hiyo ya kifahari, iliyotangazwa mjini Barcelona Hispania, inatambua ubunifu unaoleta Athari chanya za kijamii katika sekta ya mawasiliano. 

Kaulimbiu ya mwaka huu kwenye tuzo hizo zilizokabidhiwa jana tarehe 2 Machi ni “Kuiunganisha Dunia Wakati wa Migogoro” inaonyesha mchango wa teknolojia katika hatua za kibinadamu.

Mawasiliano kama njia ya maisha

Akipokea tuzo hiyo, Doreen Bogdan-Martin Katibu Mkuu wa ITU amesisitiza maana pana ya upatikanaji wa mtandao. “Tunaposhirikiana kuwasaidia wakimbizi kupata njia za kidijitali, tunafungua milango ya utu na matumaini,” amesema. “Utambuzi huu unaonesha nguvu ya ushirikiano katika kuhakikisha watu waliokimbia makazi na jamii zinazowahifadhi haziachwi nyuma.” 

Maneno yake yamedhihirisha lengo la mpango huo la kuunganisha watu milioni 20 waliokimbia makazi na jamii zinazowahifadhi ifikapo 2030 kupitia huduma za intaneti za gharama nafuu na zenye uhakika.

Mabadiliko kupitia ujumuishaji wa kidijitali

Mpango wa kuwaunganisha kidijitali wakimbizi au Connectivity for Refugees tayari umefikia zaidi ya watu milioni moja katika nchi zaidi ya 15 kufikia 2026, ukitoa fursa za elimu, ajira na huduma muhimu. 

Licha ya changamoto za ufadhili na miundombinu, mpango unaendelea kupanuka kwa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi. 

“Mawasiliano ni njia ya maisha, si anasa,” amesema Kelly T. Clements Naibu Kamishina Mkuu wa Wakimbizi wa UNHCR akiongeza kuwa  “Ishara ya simu inaweza kuwa tofauti kati ya utegemezi na kujitegemea, kati ya kutengwa na fursa.”

Utambuzi wa sekta na athari za ushirikiano

Tuzo za GLOMO zinaandaliwa na chama cha sekta ya mawasiliano GSMA na hutambua ubunifu unaobadilisha mazingira ya kidijitali. Majaji wamepongeza mpango wa “Kuwaunganisha Kidijitali Wakimbizi” kwa kushughulikia vikwazo kama gharama na ujuzi wa kidijitali huku ikikuza suluhisho endelevu. 

UNHCR na ITU wameshukuru kwa heshima hiyo na kuitaka jamii ya kimataifa kuimarisha ushirikiano. “Tuzo hii ni ya mamilioni ya wakimbizi wanaojitahidi kujenga upya maisha yao,” taasisi hizo zimesema.

Mwelekeo wa baadaye

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yamesisitiza kujitolea kwa ujumuishaji wa kidijitali kama nguzo ya mnepo na fursa za kiuchumi. Kwa kupanua mifano bunifu na kusaidia mageuzi ya sera, mpango unalenga kuhakikisha jamii zilizokimbia makazi haziachwi nyuma katika mapinduzi ya kidijitali. Wakati idadi ya watu wanaokimbia makazi ikifikia viwango vya juu, watetezi wanasema mawasiliano ni sehemu ya msingi ya hatua za kibinadamu na maendeleo ya muda mrefu. Tuzo hiyo ni utambuzi na pia wito wa kupanua juhudi ili kuhakikisha hakuna anayesalia nyuma katika dunia inayozidi kuwa ya kidijitali.