UNFPA Burundi yasaka usadizi kunusuru afya za wazazi na watoto kambini Busuma
UNFPA Burundi yasaka usadizi kunusuru afya za wazazi na watoto kambini Busuma
Uhaba wa vifaa na maji safi na salama katika kambi ya muda ya wakimbizi ya Busuma iliyoko mashariki mwa Burundi umekuwa changamoto kubwa kwa wanawake wajawazito wanaojifungua kambini hapo, wakati huu ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, (UNFPA) nchini Burundi linasema katika kipindi cha mwezi mmoja takribani watoto 200 wamezaliwa.
Ni Julien Ouedraogo, Afisa wa masuala ya Maendeleo ya vijana na barubaru wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi (UNFPA) nchini Burundi akielezea kuwa yuko Busuma kambi inayohifadhi zaidi ya wakimbizi elfu 60.
Ni kupitia video ya UNFPA Burundi iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, zamani Twitter ambako leu tunamulika masuala ya kujifungua kwenye kambi hii inayohifadhi wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) na baadhi ya warundi wanaorejea nyumbani kutoka DRC na kwingineko.
Mahema mawili hapa yamegeuzwa kuwa wodi; moja ya wajawazito na nyingine ya wazazi.
Daktari Raymond Bizimana, Mratibu wa shirika la kiraia la afya ya familia au ABUBEF linaloshirikiana na UNFPA anasema,
“Takribani wajawazito kati ya 5 hadi 6 wanajifungua kila siku. Mfano leo katika hema la wazazi tuna wanawake saba waliojifungua usiku, hii ikimaanisha kuwa tuna uhitaji mkubwa wa eneo kubwa la kuwaweka. Kila mara tumezungumzia umuhimu wa kuwa na mashine ya kuchunguza ujauzito au Ultrasound kwa lugha ya kiingereza. Na kwa wodi ya wazazi, maji ni muhimu, kwa sababu pindi tu mama anajifungua, tunahitaji maji kusafisha chumba na kitanda cha kujifungulia.”
Video inaonesha pia wafanyakazi wengine wakiendelea na kazi ya kuchimba ili kusimika mahema mengine kwani shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR hivi karibuni lilieleza kuwa kasi ya wakimbizi wa Burundi kutoka Tanzania kurejea nyumbani ni kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Kwa Ouedraogo, afisa wa UNFPA, uhaba wa maji unakwamisha huduma za shirika hilo, hususan huduma kwenye wodi ya wazazi akisema, mama kujifungua na kisha kupitisha siku kadhaa bila maji ni jambo lisilokubalika. Kwa hiyo tunahitaji msaada. Tunahitaji msaada angalau tuweze kutoa huduma za msingi kwa wakimbizi hawa waliopoteza kila kitu, na sasa wanaishi hapa katika maisha yasiyo na staha.
Licha ya changamoto, video inaonesha sura ya mama mzazi akitabasamu baada ya kukabidhiwa mwanae mikononi.
Kwa sasa UNFPA Burundi, kwa msaada wa shirika la kiraia la kusaidia manusura wa ukatili wa kingono, FONAREV, linaweza kutoa huduma za wajawazito, wazazi na watoto wachanga lakini bado mahitaji yanazidi uwezo.