Mafuriko Msumbiji: Mambo 10 ya kufahamu
Tabianchi na mazingira
Kwamujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM, mafuriko makubwa yaliyoikumba Msumbiji hivi karibuni yamesababisha vifo, watu kufurushwa makwao, miundombinu kuharibika na changamoto nyingine lukuki ikiwa ni pamoja na hofu ya kuzuka magonjwa ya mlipuko. Haya ni mambo 10 muhimu ya kugfahamu kuhusu mafuriko hayo
1. Zaidi ya watu 724,000 wameathirika
Mvua kubwa zilizonyesha kwa wiki kadhaa na zikiambatana na mafuriko zimeathiri zaidi ya watu 724,000 kote nchini Msumbiji, zikivuruga maisha, kuharibu makazi na kuangamiza vyanzo vya kipato.
Mafuriko nchini Msumbiji yanaathiri zaidi ya watu 724,000.
2. Watu zaidi ya 38,250 wamekimbia makazi yao
Zaidi ya watu 38,250 kwa sasa wamepoteza makazi na wanaishi katika vituo vya malazi ya muda.
Wengi walikimbia bila mali yoyote na sasa wanategemea msaada wa kibinadamu kutoka kwa wahisani.
Mwanamke amebeba mtoto na kifurushi cha misaada akipita katika eneo lililoathiriwa na mafuriko nchini Msumbiji.
3. Jimbo la Gaza ndio limeathirika vibaya zaidi
Jimbo la Gaza ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi, ambapo mafuriko hayo makubwa yamelazimisha familia kuondoka majumbani mwao na kuharibu miundombinu muhimu kama vile barabara, shule na vituo vya afya.
Wakazi wakitembea katikati ya maji ya mafuriko nchini Msumbiji.
4. Mamia kwa maelfu ya watu wanahifadhiwa na jamii wenyeji
Inakadiriwa kuwa mamia kwa maelfu ya watu wanaishi na familia za wenyeji au katika makazi yasiyo rasmi, mara nyingi katika hali ya msongamano mkubwa na upatikanaji mdogo wa huduma za msingi.
Watu walioathiriwa na mafuriko nchini Msumbiji wanapokea misaada ya kibinadamu.
5. Upatikanaji wa misaada umeathirika vibaya
Barabara zilizofurika na miundombinu iliyoharibika vinaendelea kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, hali inayochelewesha kufikishwa kwa msaada kwa jamii zilizo katika uhitaji mkubwa.
Watu waliofurushwa kwenye makazi yao kutokana na mafuriko nchini Msumbiji wanaishi katika mahema.
6. Maelfu ya nyumba na miundombinu vimeharibiwa
Mafuriko yameharibu makumi ya maelfu ya nyumba, baadhi kwa uharibifu wa sehemu na nyingine kuanguka kabisa.
Zaidi ya nyumba 166,806 zimezingirwa au kujaa maji, na kuacha familia nyingi bila makazi salama.
Msumbiji. Jiji la Gaza kukabiliana na mafuriko
7. Upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi umevurugika
Vyanzo vya maji vimechafuliwa na miundombinu ya usafi kuharibiwa, hali inayoongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko yanayoenezwa kwa maji na changamoto nyingine za afya ya umma.
Msumbiji. Jiji la Gaza kukabiliana na mafuriko
8. Wanawake na watoto wako katika hatari kubwa zaidi
Takribani watu wanne kati ya watano waliokimbia makazi yao ni wanawake na watoto.
Msongamano katika makazi ya muda unaongeza hatari za ulinzi, pamoja na kuvuruga upatikanaji wa elimu na huduma za afya.
Mnamo Januari 17, 2026, barabara zinafurika baada ya mvua kubwa huko Buzi, Mkoa wa Sofala, Msumbiji.
9. Mahitaji ya kibinadamu ni ya dharura
Familia zilizoathirika zinahitaji kwa haraka makazi ya dharura, vifaa muhimu vya nyumbani, maji safi, huduma za usafi wa mazingira, huduma za afya na msaada wa ulinzi.
Timu ya Umoja wa Mataifa ya tathmini ya maafa inatoa msaada kwa watu walioathiriwa na mafuriko huko Xai Xai, Msumbiji.
10. Hatua za dharura na ujenzi mpya lazima viende sambamba
Ingawa msaada wa haraka ni muhimu, juhudi za muda mrefu za ujenzi mpya na kuimarisha mnepo ni za lazima.
Kusaidia familia kujenga upya makazi, kurejesha vyanzo vya riziki na kuimarisha maandalizi kutasaidia jamii kujikwamua na kukabiliana vyema na mafuriko yajayo.