Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Gaza huko Palestina wahaha kumudu mlo wakati wa mfungo wa Ramadhani

Picha ya karibu ya taa iliyopambwa ya Ramadhani huko Gaza, iliyo na maandishi ya Kiarabu na wahusika wa katuni wenye rangi, ikiwakilisha mila za sherehe za mwezi mtakatifu.
UN News
Mojawapo ya shughuli wakati wa mwezi mtakatifu wa Ramadhani ni kupamba nyumba kwa taa ambazo hubaki zikiwaka wakati wote wa mwezi wa kufunga.

Wakazi wa Gaza huko Palestina wahaha kumudu mlo wakati wa mfungo wa Ramadhani

Amani na Usalama

Waumini wa dini ya kiislamu duniani kote wameanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, kipindi kinachoambatana na sio tu ibada bali pia mlo kama vile futari na daku. Hata hivyo kwa wakazi wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na kimabavu na Israeli hali si hali kwani mlo na mengine yanayoambatana na kipindi hiki vinasalia kuwa ndoto.

Video ya Umoja wa Mataifa inaanzia kitongoji cha Al-Zarqa kilichoko eneo la kati la jiji la Gaza, taswira hapa ni vifusi vya majengo ya makazi yaliyobomolewa katika mapigano yaliyoanza Oktoba 7, 2023.

Amal Al-Samri, mama, anatabasamu pamoja na watoto wake wanapokuwa wameketi nje ya hema yao kando ya nyumba iliyoharibiwa huko Gaza wakati wa Ramadhani.
UN News
Amal Al-Samri na watoto wake wanakaa nje ya hema lao, wakiwa wamepiga kambi kando ya nyumba yao iliyoharibiwa katika kitongoji hichohicho, huku wakijishughulisha na kazi rahisi za kila siku kwa kukosekana kwa huduma za msingi.

Pembeni kidogo ni mahema ambamo familia ikiwemo ya Walid Al- Asi wamejihifadhi.

“Kabla ya vita, tuliishi kwenye nyumba yetu kwa furaha. Tulikula na kunywa, tukifurahia matikiti maji na kila kitu. Leo hii tumenyimwa vyote hivyo. Naona vitu madukani, lakini nageukia upande mwingine kwa kuwa sina pesa. Ninaugua shinikizo la damu na kisukari na siwezi kutembea. Tunaoishi kwenye mahema tusaidiwe.”

Kando ya hema lingine amesimama Bi. Amal Al-Samri, naye nyumba yao ilibomolewa. Anaingia ndani ya hema akiwa na watoto wake huku akiendelea na shughuli za nyumbani anakumbuka ya zamani akisema,

“Kabla ya vita maisha yalikuwa mazuri, tunatembelea wazazi, ndugu na hata kwenda sokoni kujiandaa na Ramadhani. Leo hii ni janga, hakuna umeme wala maji. Tumehama mara kwa mara, na kwenye eneo moja maji ya baharí yalisomba mahema yetu.”

Mwanamume katika Gaza anashikilia taa ya mapambo na sanduku la dhahabu wakati wa sherehe za Ramadhani katika soko.
UN News
Louay Al-Jamasi, mmiliki wa duka katika Jiji la Gaza linalouza mapambo ya Ramadhani.

Tumeingia kwenye soko la kihistoria la Zawiya hapa jiji la Gaza, kukurukakara za hapa na pale mauzo ya bidhaa mbali mbali za Ramadhani ikiwemo taa za kandili mahsusi kwa mwezi huu mtukufu.

Bei hapa ya bidhaa ni maradufu. Mfano taa za kandili za kupamba wakati wa Ramadhani zimeongezeka kutoka dola 10 hadi dola 20.

Sauti hii ni ya Maher Tarazi yeye ni mkristo hapa akiburudika na nyimbo za Ramadhani anasema watu hapa wanataka furaha. Tumepitia siku za machungu na ni vema bado tuko hai. Watu wanajitazama na kuhoji iweje bado tuko hai? Wanafika sokoni, kuna baadhi ya waajiriwa wana fedha kiasi, lakini ukitazama uwezo wa manunuzi, hali sasa sio kama ilivyokuwa zamani.”