Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto milioni 26 Ethiopia wafikiwa na kampeni ya chanjo ya polio: WHO

Mfanyakazi wa afya kutoka Shirika la Afya Ulimwenguni anamtolea mtoto chanjo ya polio wakati wa kampeni ya kitaifa ya chanjo nchini Ethiopia, huku mama akimshika mtoto na maofisa wengine wakimtazama.
© WHO Zaidi ya watoto milioni 24 waliwasili kupitia Kampeni ya hivi karibuni ya NOPV2.

Zaidi ya watoto milioni 26 Ethiopia wafikiwa na kampeni ya chanjo ya polio: WHO

Afya

Serikali ya Ethiopia, kupitia Wizara ya Afya na Taasisi ya Afya ya Umma ya Ethiopia (EPHI) kwa kushirikiana na washirika wa Mpango wa Kimataifa wa kutokomeza Polio (GPEI) na Shirika la Afya la Umoja wa Mtaifa WHO, leo hii, imetangaza kuwa zaidi ya watoto milioni 26 wamefikiwa katika kampeni ya kitaifa ya duru ya nne ya chanjo jumuishi ya polio iliyotekelezwa mwaka 2025 kote nchini, kwa kutumia chanjo mpya ya matone ya polioaina ya pili (nOPV2).

WHO inasema katika kanda 22 za mikoa saba yaAmhara, Oromia, Somali, Kusini mwa Ethiopia, Harari, Dire Dawa na  Afar, chanjo hiyo imefanyika kwa njiia ya chanjo ya matone ya polio yenye aina mbili (bOPV), kwa lengo la kuimarisha kinga ya jamii na kukatiza maambukizi ya virusi vya polio.

Sherehe ya uzinduzi wa kitaifa ilifanyika tarehe 12 Desemba 2025 mjini Hawassa, mkoa wa Sidama, ikihudhuriwa na mheshimiwa Dkt. Mekdes Daba, waziri wa afya wa Ethiopia, Bwana. Beyene Berasa, naibu rais wa mkoa wa Sidama,  Dkt. Messay Hailu, mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Afya ya Umma ya Ethiopia (EPHI), pamoja na washirika wa mpango wa kimataifa wa kutokomeza polio (GPEI).

Dkt. Mekdes Daba amethibitisha upya dhamira ya Ethiopia ya kukomesha maambukizi ya virusi vya polio.
Kama nchi iliyoidhinishwa kuwa huru dhidi ya virusi pori vya poliomwaka 2017, tutashirikiana kukamilisha hatua ya mwisho ya kutokomeza polio na kutimiza ahadi za kimataifa. Hakuna mtoto atakayeachwa bila kuchanjwa. Katika kampeni ya nyumba kwa nyumba, tutaunganisha huduma za kuokoa maisha zikiwemo ufuatiliaji ulioimarishwa wa ugonjwa wa Kupooza Ghafla (AFP), utambuzi na uunganishaji wa watoto wasio na dozi na waliopata chanjo pungufu, uchunguzi wa lishe, ufuatiliaji wa ukuaji, na ufuatiliaji wa Marburg. Kwa kushirikiana na washirika, jamii na wahudumu wa afya, tutaongeza kinga, kuboresha ufuatiliaji na kuwalinda watoto wetu.” 

Usimamizi wa chanjo utasaidia kukomesha polio

Akizungumza kwa niaba ya washirika wa GPEI, Prof. Francis Kasolo, Mwakilishi wa WHO nchini Ethiopia, amepongeza Serikali ya Ethiopia kwa uongozi wake hasa uamuzi wa kusimamia kwa pamoja bOPV na nOPV2 katika kanda 22 za kipaumbele ili kuimarisha kinga ya jamii dhidi ya virusi vya polio. 

Amesisitiza kuwa usimamizi huo wa pamoja utaharakisha kukomesha maambukizi ya polio aina ya pili na pia kuimarisha uwezo wa Ethiopia kupambana na aina nyingine mseto za virusi vya polio.

Ethiopia ilikamilisha kwa mafanikio duru nne za kampeni za chanjo mpya ya matone ya polio aina ya pili (nOPV2)  katika mwaka wa  2025 (moja ya kitaifa na tatu za kikanda). 

Dru hizo, zilizotekelezwa kati ya Februari na Desemba 2025, ziliendeshwa na Wizara ya Afya/EPHI kwa msaada wa WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, Rotary International, Muungano wa Chanjo Gavi, Taasisi ya Gates, na washirika wengine wa chanjo.

Kampeni hizi zilikuwa nguzo kuu ya mkakati wa Ethiopia wa kukatiza maambukizi ya polio mseto, kuziba mapengo ya kinga na kuimarisha ufuatiliaji.

Kwa kuendelezamafanikio ya duru zilizotangulia, Ethiopia inaendelea kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa yanayozuilika kwa chanjo, kuimarisha uratibu na ushirikiano wa mipakani, na kuimarisha mifumo ya chanjo ya kawaida ili kuhakikisha kila mtoto analindwa. 

Washirika chini ya GPEI wamethibitisha kuendelea kutoa msaada wao, wakisisitiza kuwa juhudi za pamoja zitahakikisha mustakabali wa dunia usio na polio.