JARIDANI LEO: Msaada wa kibinadamu DRC, Usalama Ziwa Victoria, Elimu kwa wanafunzi wa kike Tanzania
JARIDANI LEO: Msaada wa kibinadamu DRC, Usalama Ziwa Victoria, Elimu kwa wanafunzi wa kike Tanzania
- Ufinyu wa ufadhili umelazimisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya kibinadamu, OCHA kupunguza idadi ya wanaopatiwa misaada DR Congo
- Mafunzo ya kukabili uhalifu Ziwa Viktoria yafanikisha uvuvi salama Ziwa Viktoria
- CAMFED yasongesha Malengo ya maendeleo endelevu kwa kuwajengea uwezo wanafunzi wa kike nchini Tanzania
1. Idadi ya wanaopatiwa msaada DRC yapunguzwa kutokana na ukata
Kutokana na ufinyu wa ufadhili unaolazimisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada ya kibinadamu, OCHA kupunguza idadi ya wanaopatiwa misaada nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, serikali ya DRC kwa kushirikiana na OCHA wamezindua ombi la dola za kimarekani bilioni 1.4 ili kuokoa hali.
Ripoti ya Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) iliyotolewa leo Januari 28, 2026 mji mkuu wa DRC, Kinshasa, imebainisha kuwa kutokana na ukata sasa usaidizi utaelekezwa kwa watu milioni 7.3 pekee, licha ya kuwa karibu watu milioni 15 wanahitaji msaada wa kuokoa maisha.
Hii imekuwa punguzo kubwa ikilinganishwa na watu milioni 11 waliopewa kipaumbele mwaka 2025, huku wastani wa gharama kwa kila mnufaika ukishuka kutoka Dola 231 hadi Dola 192.
Ombi la mwaka huu linalenga kupatia wahitaji msaada wa chakula, maji safi, na ulinzi kwa wale walio hatarini zaidi, hasa wanawake na watoto.
Athari mbaya za upungufu wa fedha zimejionesha wazi tangu mwaka 2025, ambapo vituo vya lishe zaidi ya 1,000 vimefungwa na kuacha watoto 390,000 wenye utapiamlo mkali bila matibabu muhimu.
Aidha, takriban watu milioni 1.5 wamepoteza uwezo wa kupata huduma za afya ya msingi, huku malengo ya msaada wa chakula ya kila mwezi yakipunguzwa kwa asilimia 73 kutokana na ukosefu wa rasilimali.
Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu nchini DRC, Bruno Lemarquis, ameelezea uzito wa hali hiyo akisema: "Mchanganyiko wa mahitaji makubwa na rasilimali chache unatulazimisha kufanya maamuzi magumu sana, wakati mwingine yasiyowezekana."
Ameongeza kuwa msaada wa kibinadamu pekee si suluhu ya kudumu,"Hatuwezi kuendelea kufanya kazi kama hapo awali. Msaada wa kibinadamu ni wa lazima kwa sababu unaokoa maisha, lakini si suluhu la matatizo ya kibinadamu."
Lemarquis ametoa wito wa mabadiliko ya mfumo akisisitiza kuwa "ufumbuzi wa kisiasa" na amani lazima iwe kitovu cha juhudi zote.
2. IOM, Marekani na wadau washirikiana kukabili uhalifu Ziwa Viktoria
Ziwa Viktoria barani Afrika, licha ya kuwa mhimili muhimu wa maisha kwa zaidi ya watu milioni 40 nchini Kenya, Uganda na Tanzania, bado linakabiliwa na vitisho vihusianavyo na biashara haramu za magendo, usafirishaji haramu binadamu na uvuvi haramu. Ili kupatia suluhu changamoto hiyo Ofisi ya Masuala ya Kimataifa ya kupambana na dawa za kulevya na utekelezaji wa sheria (INL) ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, (IOM), na walinzi wa pwani wa Kenya wamechukua hatua.
Simulizi yangu inaanzia kwenye Ziwa Viktoria la pili kwa ukubwa duniani, ambapo George Otieno ambaye ni mvuvi anatupatia taswira kabla ya hatua za wadau.
“Tulipokuwa majini mashua ikipinduka, zamani tulikuwa tunang’ang’ania mabaki ya mashua. Wakati mwingine ungekaa juu ya mabaki kuanzia asubuhi hadi jioni, au hata usiku kucha hadi siku inayofuata bila msaada wowote.”
Hatua za wadau zilihusisha mafunzo ya usalama wa majini, uokoaji wa maisha na ushirikiano wa karibu na jamii, hatua zilizowezesha kujenga utamaduni wa kinga, uaminifu na uhamaji salama unaoanzia ngazi ya jamii.
Parvati Sankar, Mwakilishi wa INL ambayo ni Ofisi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anasema hatua zote ni kukabiliana na uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka ili kuboresha usalama wa majini Ziwa Victoria.
“Kwa kushirikiana na serikali za Kenya, Tanzania na Uganda, tunaimarisha uwezo wao wa kupambana na uhalifu wa kimataifa katika Ziwa Victoria. Mpango huu hauwawezeshi tu washirika wetu, bali pia unaimarisha usalama wetu wenyewe. Kwa kuvuruga shughuli haramu kama usafirishaji wa binadamu na biashara ya dawa za kulevya nje ya mipaka yetu, tunazuia vitisho hivi kufikia mipaka na jamii zetu.”
Kupitia mafunzo ya usalama wa majini na uokoaji wa maisha, IOM na walinzi wa pwani ya Kenya wanaimarisha usalama, kinga na uhamaji salama, huku wakishirikiana na jamii za wavuvi kujenga uelewa, imani na usalama unaoanzia ngazi ya jamii. Lucas Otieno, mvuvi kutoka kaunti ya Siaya nchini Kenya anasema
“Kumekuwa na mabadiliko makubwa. Zamani tulikuwa tunawaona walinzi wa pwani kama maadui. Lakini sasa tunaona ni watu wazuri wanaojali usalama wetu majini.”
Kwa mujibu wa viongozi wa mradi, uendelevu ndio nguzo kuu ya juhudi hizi. Parvati Sankar anatamatisha akisema
“Hatuleti suluhisho la muda mfupi. Tunajenga mfumo imara na wa kudumu wa uratibu na kubadilishana taarifa kati ya mashirika ya mipakani. Hii inahakikisha kuwa ushirikiano na kasi tuliyojenga vinaendelea hata baada ya mradi kukamilika.”
Lengo kuu la mradi huu ni kuwawezesha washirika wa kikanda kukabiliana kwa kujitegemea na changamoto zijazo, huku wakijenga mahusiano ya muda mrefu yanayochangia usalama wa kikanda na kuunga mkono maslahi ya Marekani kwa miaka ijayo.
3. CAMFED yaendelea kujengea uwezo wanafunzi wa kike nchini Tanzania
Nchini Tanzania shirika la kiraia la kuendeleza elimu kwa watoto wa kike, CAMFED limeendelea kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kwa kuwezesha wanafunzi wa kike kuimarika sio tu kimasomo darasani bali pia stadi za maisha na hatimaye wawajengee uwezo wenzao.
Miongoni mwa wanufaika ni Habe Kitambara mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mikese iliyoko mkoani Morogoro, Mashariki mwa Tanzania ambaye simulizi yake inaonesha nguvu ya mafunzo ya CAMFED katika kuboresha elimu ya mtoto wa kike nchini Tanzania.
Kupitia msaada wa kielimu na stadi za maisha, wasichana wengi wanapata nafasi ya kuendelea na masomo yao bila kukatishwa tamaa na changamoto za kijamii na kiuchumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la CAMFED nchini Tanzania Anna Sawaki, anasema mwaka 2025 wamepata waweza kuandaa kitabu cha muongozo wa stadi za maisha kinachojulikana kwa jina la “Dunia yangu Bora” kilichopitishwa na Serikali kutumika katika Shule za Sekondari.
Kupitia mipango kama Dunia Yangu Bora na uwezeshaji wa wahitimu kama Eva John, CAMFED inaendelea kujenga kizazi cha wasichana na wanawake wanaojiamini, wanaojitegemea na walio tayari kuchangia maendeleo ya jamii, sambamba na dira ya elimu jumuishi inayoongozwa na UNESCO.