Botswana yajiunga na mikataba ya kimataifa ya maji kuimarisha ushirikiano: UNECE
Botswana yajiunga na mikataba ya kimataifa ya maji kuimarisha ushirikiano: UNECE
Nchi ya Botswana imechukua hatua kubwa katika kuimarisha ushirikiano wa rasilimali za maji baada ya kujiunga rasmi na mikataba miwili ya kimataifa ya maji ya Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa iliyotolewa Januari 26, 2026 huko Dakar, Senegal, na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa ajili ya Ulaya UNECE, wakati wa mkutano wa maandalizi ya Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 2026, hatua hiyo imetajwa kama ushindi mkubwa kwa diplomasia ya maji barani Afrika.
Botswana sasa imekuwa mwanachama wa 58 wa Mkataba huo, ikiungana na mataifa mengine duniani katika usimamizi endelevu wa vyanzo vya maji vinavyounganisha nchi zaidi ya moja.
Kwa mujibu wa UNECE, uamuzi huo umekuja wakati muafaka kwani karibu eneo lote la Botswana lipo ndani ya mabonde ya mito inayovuka mipaka, ikiwemo mito ya Okavango, Limpopo, Orange-Senqu, na Zambezi.
Mito hii ni muhimu kwa maisha ya watu, mfumo wa ikolojia, na uchumi wa taifa hilo ambalo halina bahari lakini limeunganishwa na maji. Kwa kujiunga na mikataba hii, Botswana imedhamiria kutumia mifumo ya kisheria inayotambulika kimataifa ili kuzuia migogoro, kukuza amani, na kubadilishana uzoefu wa takwimu za maji na nchi jirani.
Botswana imeonyesha Imani kwa ushirikiano wa kimataifa
Katibu wa Mkataba wa Maji, Sonja Koeppel, amepongeza hatua hiyo akisema kuwa Botswana imeonesha imani kubwa katika ushirikiano wa kimataifa wakati huu ambapo dunia inaelekea kwenye Mkutano wa Maji wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika Abu Dhabi mwezi Desemba 2026.
Amesisitiza kuwa kujiunga kwa Botswana kunaimarisha maono ya pamoja ya usimamizi wa maji barani Afrika na kutoa mfano kwa nchi nyingine zinazounganishwa na vyanzo vya maji kuongeza kasi ya kujiunga na mikataba hiyo ili kudhibiti janga la mabadiliko ya tabianchi.
Botswana sasa imekuwa moja ya nchi mbili pekee barani Afrika, ikiungana na Namibia, ambazo zimefanikiwa kuwa na makubaliano ya kiutendaji katika vyanzo vyake vyote vya maji vinavyovuka mipaka.
Maafisa wa serikali ya Botswana wamebainisha kuwa kuripoti kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 6.5.2) imesaidia kukuza nia ya nchi hiyo kujiunga na mikataba hiyo ya kimataifa. Hatua hii imelenga kuimarisha ugawanaji wa maji kwa usawa na kusaidia utekelezaji wa miradi ya pamoja ya maji katika kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Uanachama huu mpya umeifungulia Botswana milango ya kupata msaada wa kiufundi, mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wake, na ushiriki wa karibu katika jumuia ya kimataifa ya usimamizi wa maji.
Huu ni uthibitisho wa utashi wa kisiasa wa taifa hilo katika kuharakisha upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira ambalo ni lengo la sita la Malengo ya Maendeleo Endelevu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amekuwa akihimiza mataifa yote kujiunga na mikataba hii ili kuhakikisha rasilimali za maji zinatumika kama chombo cha amani na maendeleo badala ya mzozo.