Tanzania: Ushirikishwaji wa vijana waimarisha elimu jumuishi
Tanzania: Ushirikishwaji wa vijana waimarisha elimu jumuishi
- Ushirikishwaji wa vijana katika kupanga na kuboresha elimu
- Utekelezaji wa kauli mbiu ya UNESCO kuhusu elimu jumuishi nchini Tanzania
- Uundaji wa mitaala inayozingatia mahitaji ya vijana na soko la ajira
Vijana ni zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani na wanatambulika kama injini muhimu ya uvumbuzi, mabadiliko ya kijamii na maendeleo endelevu. Hata hivyo, vijana wengi bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyozuia uwezo wao wa kuchagiza maisha wanayoyataka, kuanzia kujiondoa kwenye umasikini na kupunguza ukosefu wa usawa, hadi upatikanaji mdogo wa elimu bora na ajira zenye staha.
Kwa kuwa maisha na fursa za vijana zinategemea kwa kiasi kikubwa elimu, ni muhimu wao kuwa washirika hai katika kufikiria upya namna mifumo ya elimu inavyofanya kazi. Ndiyo maana mwaka huu, katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Elimu iliyofanyika tarehe 24 Januari, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) lilikuja na kauli mbiu isemayo “Nguvu ya vijana katika kuunda elimu jumuishi”, ikiwa na lengo la kuhakikisha ushirikishwaji wa vijana katika sekta ya elimu.
Nchini Tanzania, utekelezaji wa kauli mbiu hii unaonekana kwa vitendo. Daktari Bonny Betson, Daktari Bingwa wa Kinywa na Meno katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na pia Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS), anaeleza jinsi taasisi yao inavyowashirikisha vijana katika kupanga na kuboresha mafunzo ya elimu ya juu.
Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Betson anasema wanafunzi ni wadau wakuu katika mchakato wa elimu. “Kwanza niseme kwamba tunatambua kuwa wanafunzi ni wadau wakubwa sana katika mafunzo, ni wadau namba moja kwa sababu wao ndiyo wanaopokea mafunzo. Mafunzo yoyote yanayotolewa lazima yazingatie mahitaji yao,” anasisitiza.
Anaongeza kuwa chuo kimeweka mkazo maalum katika kuwashirikisha vijana tangu hatua za awali za upangaji wa mitaala. “Kama chuo, tumeshaanza tangu awali kuwashirikisha vijana kushiriki moja kwa moja katika kupanga ni aina gani ya mafunzo wanayohitaji, mafunzo ya vitendo, na katika kila hatua ya mchakato wa mafunzo. Hii inawasaidia kuandaliwa kikamilifu kulitumikia taifa lao,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Dkt. Betson, ushirikishwaji wa wanafunzi katika mifumo ya uongozi wa chuo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarika kwa ubora wa elimu. “Tumetambua mapema umuhimu wa kuwahusisha wanafunzi katika serikali zao, vikao vya pamoja na uongozi wa chuo pamoja na walimu. Ushirikishwaji huu unasaidia kuamua namna bora ya utoaji wa mafunzo na umeleta matokeo chanya, ikiwemo kuongezeka kwa ufaulu mzuri na wahitimu wanaotoa huduma bora zinazokubalika katika jamii,” anasema.
Si wanafunzi pekee wa MUCOHAS wanaoshirikishwa katika mchakato huu, bali pia waajiri. Dkt. Betson anaeleza kuwa chuo hupokea maoni kutoka kwa waajiri kuhusu aina ya wahitimu wanaohitajika sokoni. “Tunawahusisha pia waajiri ili kuelewa wanahitaji wahitimu wa namna gani. Maoni yao, pamoja na yale ya wahitimu na wanafunzi waliopo, yanatusaidia kuboresha mitaala yetu. Wahitimu hutueleza changamoto wanazokutana nazo wanapoanza kazi, na maeneo ambayo wangetamani yangefundishwa wakiwa chuoni,” anafafanua.
Kwa njia hiyo, chuo kinafanikiwa kuwa na mitaala inayoakisi mahitaji halisi ya vijana na soko la ajira, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kuunda elimu jumuishi, yenye tija na inayomuwezesha kijana kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.