Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa waonya juu ya ongezeko la vitisho vya AI kwa watoto, ikiwemo matumizi ya picha zilizobadilishwa

Mwanafunzi wa kike aliyevaa sare na miwani anaangalia simu yake ya mkononi wakati wanafunzi wengine wanaonekana nyuma.
UNICEF/Estey Watoto wasichana wakifuatilia taarifa kwa kutumia simu za mkononi

Umoja wa Mataifa waonya juu ya ongezeko la vitisho vya AI kwa watoto, ikiwemo matumizi ya picha zilizobadilishwa

Masuala ya UM

Umoja wa Mataifa (UN), leo, umetoa onyo kuhusu kuongezeka kwa vitisho vinavyotokana na matumizi ya Akili Mnemba (AI) kwa watoto katika mazingira ya mtandaoni duniani kote, kufuatia ongezeko kubwa la maudhui hatarishi yanayotengenezwa na AI ambayo yanasababisha unyanyasaji, unyonyaji na madhara ya kisaikolojia kwa watoto. 

Onyo hilo limetolewa kupitia wito wa haraka wa kuchukuliwa hatua na mapendekezo mahsusi ya kulinda watoto dhidi ya madhara yanayoletwa na matumizi mabaya ya teknolojia ya AI.

Umoja wa Mataifa umetolea mfano wa deepfakes kwa ainisho la kiswahili, picha mnato au picha mjongeo ya mtu iliyobadilishwa kidijitali ili aonekane kama mtu mwingine, mara nyingi kwa nia mbaya au kwa lengo la kusambaza taarifa za uongo. Halikadhalika matumizi ya grooming ambao ni mkakati unaotumiwa lugha kwa ajili ya upotoshaji wa taarifa na propaganda.

Cosmas Zavazava, Mkurugenzi wa Ofisi ya Maendeleo ya Mawasiliano katika Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) ambayo ni  mojawapo ya mashirika muhimu yaliyoandaa tamko hilo linalojumuisha miongozo na mapendekezo,  anaelezea mbinu nyingi na tata zinazotumiwa kuwalenga watoto.

Mbinu hizo zinaanzia kwa kutumia lugha mtandaoni kuwavutia watoto kimtandao kwa nia ya unyanyasaji, matumizi ya picha zilizobadilishwa kidijitali, uwekaji wa vipengele hatarishi katika mifumo ya kidijitali, unyanyasaji wa mtandaoni hadi maudhui yasiyofaa.

Tuliona kuwa wakati wa janga la coronavirus">COVID-19, watoto wengi, hasa wasichana na wanawake vijana, walinyanyaswa mtandaoni na mara nyingi hali hiyo iligeuka kuwa madhara ya kimwili,” Cosmas Zavazava, amesema.

Mashirika yanayotetea haki za watoto yanaripoti kuwa wanyanyasaji wanaweza kutumia AI kuchambua tabia za mtoto mtandaoni, hali yake ya kihisia na maslahi yake, ili kubuni mikakati mahsusi ya grooming.

Akili mnemba  pia inawawezesha wahalifu kutengeneza picha bandia za kingono za watoto halisi, hali inayochochea aina mpya ya unyang’anyi wa kingon.

Taasisi ya kimataifa ya usalama wa watoto ya Childlight Global Child Safety Institute, taasisi huru ya kimataifa iliyoanzishwa kukusanya takwimu sahihi kuhusu unyonyaji na unyanyasaji wa kingono kwa watoto, ilibaini katika ripoti ya mwaka 2025 kuwa visa vya unyanyasaji wa watoto vilivyorahisishwa na teknolojia nchini Marekani viliongezeka kutoka 4,700 mwaka 2023 hadi zaidi ya visa 67,000 mwaka 2024.

Australia inaongoza katika kulinda watoto mtandaoni.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinaanza kuchukua hatua kali zaidi kadri zinavyoelewa ukubwa na uzito wa tatizo hili.

Mwishoni mwa mwaka wa 2025, Australia ikawa nchi ya kwanza duniani kupiga marufuku akaunti za mitandao ya kijamii kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 16, ikieleza kuwa hatari zinazotokana na maudhui wanayoshiriki zinazidi kwa kiasi kikubwa faida zinazoweza kupatikana.

Serikali ya Australia ilinukuu ripoti iliyoagizwa na serikali, iliyoonesha kuwa karibu theluthi mbili ya watoto wenye umri wa miaka 10 hadi 15 walikuwa wameona maudhui ya chuki, vurugu au yanayosababisha msongo wa mawazo, na zaidi ya nusu walikuwa wamekumbwa na unyanyasaji wa mtandaoni. Maudhui mengi yalionekana kupitia mitandao ya kijamii.

Nchi nyingine kadhaa, zikiwemo Malaysia, Uingereza, Ufaransa na Kanada, zinaonekana kujiandaa kufuata nyayo za Australia kwa kuandaa sheria na kanuni za marufuku au vikwazo kama hivyo.

Four young adults are seated on a vibrant pink couch, engrossed in their smartphones. The scene highlights youth engagement with digital technology and social media, reflecting themes of internet safety, cyberbullying prevention, and digital citizenship.
© UNICEF Vijana wanaangalia mitandao ya kijamii huko Macedonia Kaskazini.

Ukosefu wa uelewa wa Akili Mnemba

Mwanzoni mwa mwaka  huu, mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa yanayohusika na usalama wa watoto yalitoa tamko la pamoja kuhusu Akili Mnemba na haki za mtoto, lililochapishwa tarehe 19 Januari, likieleza wazi hatari zilizopo na kushindwa kwa jamii kwa ujumla kukabiliana nazo.

Tamko hilo linaainisha ukosefu wa uelewa wa AI miongoni mwa watoto, walimu, wazazi na walezi, pamoja na upungufu wa mafunzo ya kiufundi kwa watunga sera na serikali kuhusu mifumo ya AI, mbinu za ulinzi wa data na tathmini za athari kwa haki za mtoto.

Wajibu wa kampuni kubwa za teknolojia

Kampuni za teknolojia pia zimepewa wajibu mkubwa: tamko hilo linaeleza kuwa zana nyingi zinazotumia AI wanazotengeneza  pamoja na mifumo, mbinu na miundo yake ya msingi  kwa sasa hazijabuniwa kwa kuzingatia watoto na ustawi wao.

Tuna wasiwasi mkubwa, na tungependa sekta binafsi ihusishwe na iwe sehemu ya simulizi tunayoandika kwa pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa na wadau wanaoamini kuwa teknolojia inaweza kuwezesha maendeleo, lakini pia inaweza kuharibu,” amesema Bwana Zavazava.

Ameongeza kuwa, kwa matumizi yenye uwajibikaji ya AI, makampuni bado yanaweza kupata faida, kufanya biashara na kuongeza soko, huku yakihakikisha ulinzi wa watoto.

Suala la haki za watoto

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasisitiza kuwa bidhaa za kiteknolojia zinapaswa kubuniwa kwa kuheshimu haki za watoto, huku yakitoa wito kwa jamii nzima kuwajibika kuhusu matumizi ya teknolojia hizi.

Katika mwaka wa  2021, marekebisho yalifanywa kwenye mkataba wa haki za mtoto ili kuakisi hatari za zama za kidijitali, lakini Umoja wa Mataifa unaona bado kuna haja ya mwongozo zaidi kwa nchi ili kudhibiti kwa ufanisi zaidi.

Bwana. Zavazava ameeleza kuwa watoto wanaanza kutumia mtandao wakiwa na umri mdogo, na wanapaswa kulindwa,  akisisitiza kuwa miongozo ya ulinzi wa watoto mtandaoni imeandaliwa mahsusi kwa wazazi, walimu, wasimamizi wa sheria na sekta binafsi.

Mapendekezo kwa ufupi

  • Nchi ziimarishe mifumo ya utawala wa AI ili kulinda haki za watoto
  • Haki za watoto zijumuishwe katika sera zote zinazohusiana na AI
  • Serikali na makampuni yahakikishe AI ina uwazi na uwajibikaji
  • Hatua zichukuliwe kuzuia unyanyasaji wa watoto unaochochewa na AI
  • Ulinzi wa data unaomlenga mtoto uimarishwe
  • Maamuzi ya AI yazingatie maslahi bora ya mtoto
  • AI jumuishi isiyo na upendeleo ihakikishe watoto wote wananufaika
  • Maoni ya watoto yahusishwe katika sera na usanifu wa AI
  • Maendeleo ya AI yazingatie uendelevu wa mazingira

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanayounga mkono tamko hili ni pamoja na:

  • Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU)
  • Kamati ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Mtoto (CRC)
  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF)
  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO)
  • Muungano wa Mabunge Duniani (IPU)
  • Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO)
  • Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Utafiti wa Uhalifu na Haki ya Jinai ya Kikanda (UNICRI)
  • Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Uondoaji wa Silaha (UNODA)
  • Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu (OHCHR)
  • Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto na Migogoro ya Kivita (SRSG-CAAC).
  • Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto (SRSG-VAC).
  • Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uuzaji, unyonyaji wa kingono na unyanyasaji wa kingono dhidi ya Watoto (UN SR on SEA of Children).
  • Safe Online (jukwaa la uwekezaji linaloungwa mkono na UNICEF kwa ajili ya kuondoa maudhui ya mtandaoni yanayohusisha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto)